The House of Favourite Newspapers

Marekani Kupeleka Mabomu 1,800 Ya MK-84 Kwenda Israel

Marekani imetangaza kusafirisha mabomu 1,800 ya aina ya MK-84 kwenda Israel katika siku chache zijazo, mabomu hayo yenye uzito wa pauni 2,000 yamehifadhiwa nchini Marekani na sasa yataruhusiwa kusafirishwa kwa amri ya Ikulu ya White House chini ya Rais Donald Trump.

Kwa mujibu wa maafisa watatu wa Israeli waliozungumza na Axios, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imeondoa marufuku ya kusafirisha mabomu hayo.

Hatua hii inakuja baada ya utawala wa Rais Joe Biden kusitisha usafirishaji wa mabomu hayo mwezi Mei mwaka jana, jambo lililoibua mgogoro mkubwa kati ya Marekani na Israel wakati wa vita vya Gaza vilivyodumu zaidi ya miezi 15.

Pentagon imeripotiwa kuiarifu serikali ya Tel Aviv kuhusu uamuzi wa kuondoa marufuku hiyo siku ya Ijumaa.

Utawala wa Biden ulikuwa na wasiwasi kwamba matumizi ya mabomu hayo katika maeneo yenye wakazi wengi, kama Gaza, yangesababisha vifo vya raia kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na wafuasi wake walidai, kimakosa, kwamba hatua ya Biden ilikuwa ni vikwazo vya silaha dhidi ya Israel.