MAREKANI YAISHTAKI KAMPUNI YA HUAWEI

 

MAREKANI imeishtaki kampuni kubwa ya mawasiliano ya China, Huawei,  na ofisa mkuu wake wa fedha, Meng Wanzhou.

 

Mashataka hayo ni pamoja na ubadhirifu wa fedha, kupinga utekelezaji wa haki na wizi wa teknolojia.

 

Kesi hiyo huenda ikazua mgogoro wa kibiashara kati ya Marekani na China hali ambayo itaathiri biashara ya kampuni hiyo.

 

Kampuni ya Huawei imekanusha madai hayo.

 

Katika taarifa, Huawei imesema kuwa “imeghadhabishwa na mashtaka dhidi ya yake”.

 

Imesema kuwa haikufanya makosa yote “yanayodaiwa ilitekeleza” na kwamba”haina ufahamu wa kosa alilotekeleza Bi Meng”.

 

Meng ambaye ni binti wa mwanzilishi wa Huawei, alikamatwa nchini Canada mwezi uliyopita kufuatia ombi la Marekani kwa madai ya kukiuka vikwazo vyake dhidi ya Iran.

 

“Kwa miaka sasa, kampuni za China zimekiuka sheria zetu za biashara ya kimataifa, hatua ambayo inahujumu vikwazo vyetu na mara nyingine kutumia mfumo wa fedha wa Marakani kuendesha shughuli zao haramu. Hili lazima likomeshwe,” alisema waziri wa biashara wa Marekani, Wilbur Ross.

 

 

Mashtaka hayo yanadai kuwa Huawei iliipotosha Marekani na benki ya kimataifa na kufanya biashara na Iran kupitia kampuni zake mbili za mawasiliano,Huawei Device USA na Skycom Tech.

 

Utawala wa Rais Donald Trump ulirejesha vikwazo vyote dhidi ya Iran vilivyokuwa vimeondolewa chini ya mkataba wa kimataifa wa nuklia uliofikiwa mwaka 2015.

 

Kesi ya pili inadai kuwa Huawei iliiba teknolojia kutoka kwa T Mobile kufanyia majaribio ya kudumu kwa ajili yake, pamoja na kupinga sheria na ubadhirifu wa fedha kupitia mtandao.

 

Huawei ni mojawapo ya kampuni kubwa za mawasiliano na usambazaji wa simu duniani, ambayo hivi karibuni iliishinda Apple na kuwa ya pili kwa uundaji wa simu aina ya smartphone baada ya Samsung.

 

Marekani na mataifa mengine ya magharibi yana hofu kuwa serikali ya China huenda ikatumia teknolojia ya kampuni ya Huawei kuimarisha uwezo wake wa kijasusi, japo kampuni hiyo inasisitiza kuwa haina ushirikiano wowote wa kibiashara na serikali.

 

Hatua ya kukamatwa kwa Bi Meng, binti wa mwanzilishi wa Huawei iliikasirisha China.

 

 

 

 

Mengi alikamatwa Desemba mosi mwaka jana nchini Canada katika mji wa magharibi wa Vancouver kufuatia ombi la Marekani.  Baadaye mahakama ilimuachiliwa kwa dhamana ya dola milioni 76.

 

Loading...

Toa comment