Marioo: Ujio Wangu na Mondi Lazima Watupishe
UKISIKIA ngoma hii ambayo haikosekani kwenye laptop za MA-DJ, lazima utauliza inaitwaje na ni ya mwanamuziki gani?
Usipate taabu. Ngoma inaitwa Unanikosha. Ni ya dogo mmoja ambaye kwa sasa ni moto wa kuotea mbali, wanamuita Toto Bad. Wengi tunamjua kama Marioo.
Jina kamili ni Omari Ali Mwanga. Ni bonge moja la kipaji kilichojaa utunzi wa mashairi na melodi tamu ndani yake.
Mbali na Unanikosha, Marioo anasikika vizuri mno kwenye midundo ya ngoma zake kali kama Raha, Aya, Manyaku, Ifunanya, Inatosha, Anyinya na nyingine kibao ambazo zimetazamwa na mamilioni kwenye YouTube.
Nikukumbushe tu, Marioo kabla ya kuingia kwenye tasnia hii, alipata vikwazo vingi katika safari yake ya muziki, wakati huo akiwa fundi magari kwenye gereji.
Inatosha, ni ngoma yake ambayo bado inasikika na kuteka vichwa vya mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva.
OVER ZE WEEKEND imekaa kitako na Marioo ambapo anafunguka mambo kibao kuhusu muziki wake, kubwa zaidi ni ujio wa kolabo kati yake na mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’, kwani ni lazima watoto wawapishe.
OVER ZE WEEKEND: Unanikosha ni ngoma inayofanya poa kwa sasa, mapokeo yake yako vipi?
MARIOO: Nashukuru sana, nafurahi mashabiki wangu wameipokea na kuifanya kuwa bora miongoni mwa ngoma zilizotoka hivi karibuni.
OVER ZE WEEKEND: Ngoma zako zimekuwa zikikubalika sana kwa mashabiki, nini siri ya mafanikio?
MARIOO: Nimekuwa nikifanya mwendelezo wa muziki mzuri, sijawahi kuwaza kutoa ngoma mbaya, ndiyo sababu ngoma zangu huwa zinakubalika, namshukuru Mugu kwa hilo.
OVER ZE WEEKEND: Mondi ni mwanamuziki ambaye jitihada zenu zinaendana, je, mashabiki wategemee kolabo kutoka kwenu?
MARIOO: Ni kitu kizuri kufanya kazi na Diamond, mashabiki wangu wakae tayari kupokea kazi yetu, wajue kwamba ujio wangu na Mondi, si wa kitoto, watu lazima watupishe.
OVER ZE WEEKEND: Mipango yako iko vipi katika kuachia Extended Playlist (EP) au album?
MARIOO: Kwa upande wangu kutoa Ep au album ni kitu kizuri sana, kwa sababu hizo ni stepu za mwanamuziki, kwa hiyo nilikuwa naangalia ni kwa namna gani nitafanya kitofauti.
OVER ZE WEEKEND: Umeshika nafasi ya mwisho kwenye listi ya wanamuziki waliofanya vizuri mwezi Aprili iliyotoka kwenye Mtandao wa Swahili Times, mikakati yako iko vipi ya kuwa kileleni kwa mwezi Mei?
MARIOO: Kwangu naona si mbaya kuwa katika nafasi hiyo, kwani nimewafunika wasanii wengi wakubwa, kwa hilo namshukuru Mungu, nimeonekana kuwa na uwezo, kikubwa nitaongeza jitihada ili niwe kileleni miezi mingine.
OVER ZE WEEKEND: Kwa upande wako kama mwanamuziki, janga la Corona limekupotezea mapato kiasi gani kwenye shoo ulizotarajia kufanya?
MARIOO: Mwaka jana mimi ndiye msanii niliyefanya shoo nyingi zaidi, naweza kusema nilipata pesa nyingi. Siwezi kuzungumzia vibaya janga hili, ninachoamini huu ni mtihani wa Mungu, utaisha na mambo mengine yataendelea.
OVER ZE WEEKEND: Unaonekana kuwa karibu sana na Harmonize. Je, kuna ishara za kusainiwa Konde Gang?
MARIOO: Hapana, suala la kusainiwa chini ya lebo yake halina ukweli, ukaribu wetu ni kwa ajili ya kazi tu.
OVER ZE WEEKEND: Unaizungumziaje menejimenti yako?
MARIOO: Menejimenti yangu ina manufaa makubwa, ni watu wenye upendo, wanaotaka nifike mbali tangu mwanzo mpaka sasa wako na mimi.
OVER ZE WEEKEND: Kwa kipindi hiki, ni ngoma gani inakubamba sana?
MARIOO: Ngoma yangu mwenyewe ya Unanikosha, ni bora zaidi.
OVER ZE WEEKEND: Una mikakati gani ya kubaki kwenye chati, kutokana na gemu kuwa tafu?
MARIOO: Mikakati ni mikubwa, lengo langu ni kuitangaza Tanzania, mashabiki wangu najua wananipenda sana, kuzidi kupanda yote ni mipango ya Mungu tu.
OVER ZE WEEKEND: Mipango ya ndoa na watoto kwa upande wako imekaaje?
MARIOO: Kwa sasa sijajipanga kwa hilo, kwa sababu nina mambo mengi, bado natafuta maisha, muda mwingi nakesha studio, siwezi kuoa ili nimtese mke wangu, mambo yakikaa sawa, nitafanya hivyo.
OVER ZE WEEKEND: Mbali na muziki, unajishughulisha na nini?
MARIOO: Muziki ni kazi pekee inayoniingizia kipato, hakuna nyingine.
OVER ZE WEEKEND: Unawaambia nini mashabiki wako?
MARIOO: Nawapenda sana, wategemee vitu vizuri zaidi kutoka kwangu, wazidi kunipa sapoti maana bila wao mimi si kitu.