Mashabiki wa Simba na Yanga, Nyaishozi Mkoani Kagera Wapiga Bonge la Dabi Kumaliza Ubishi

Afisa Tarafa wa Tarafa ya Nyaishozi Wilayani Karagwe mkoa wa Kagera, Kelvin Berege ameratibu ‘dabi’ ya mashabiki wa Simba na Yanga tarafani hapo.
Dabi hiyo mashabiki wa Simba na Yanga ilibeba Msemo wa “ Mtani eeeh Nyaishozi Derby haina Kipengele, labda Kipengele Uje Nacho wewe Mtani. “
Katika bonanza hilo mashabiki wa Simba waliibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya mashabiki wa Yanga na kujinyakulia zawadi ya mbuzi dume (Beberu).

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Ndg. Kelvin Berege amesema alifikiria kuandaa bonanza hilo ili kumaliza tambo na majigambo ya mashabiki wa Simba na Yanga kwenye vijiwe mbalimbali vya vijana na pia sehemu za kuangalizia mipira maarufu kama vibanda umiza, hivyo kuamua ubishi huo ikaonelewa Mwali awekwe kati, watani wapishane uwanjani.

Baada ya mchezo huo Berege aliwasifu mashabiki wa Simba kwa kuibuka na ushindi, huku akiwashukuru mashabiki wa timu zote mbili kwa ushindani wa kimichezo waliouonesha ndani na nje ya Uwanja.
Ameendelea kusema huwa michezo si vita bali ni sehemu ya kutuleta pamoja kwa amani na upendo na
kumalizia kwa kuwasisitiza wananchi wote kuendelea kudumisha Amani na Upendo kati yetu hasa tunapoelekea kipindi hiki cha uchaguzi, lakini pia aliwataka wananchi hao waliofurika kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la Uandikishaji na Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linaloendelea nchini, kwani ndiyo msingi wa uchaguzi bora.