Kartra

Mashabiki Yanga Watamba Hamtuwezi – Video

HAMTUWEZI! Hiyo ndiyo kauli waliyotoka nayo Wanayanga jana Uwanja wa Mkapa, Dar baada ya timu yao kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba, ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.

 

Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nassredine Nabi, ushindi huo umewafanya kutibua sherehe za ubingwa kwa Simba ambapo vinara hao wangeibuka na ushindi au sare, basi wangekuwa mabingwa kutokana na wingi wa pointi na idadi kubwa ya mabao.

 

Mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyekuwa uwanjani hapo, ilishuhudiwa kiungo wa Yanga, Zawadi Mauya dakika ya 12 akiwainua mashabiki wa timu hiyo vitini kwa shuti kali lililomchanganya Aishi Manula na kutikisa nyavu.

Kabla ya mpira haujaingia nyavuni, ulimgonga beki wa Simba, Shomari Kapombe na kumpoteza Manula.Huu unakuwa ni mchezo wa tatu kwa Simba kupoteza ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu tena kwa idadi sawa ya mabao.Ilianza kufungwa 1-0 na Prisons, kisha 1-0 na Ruvu Shooting na jana ni 1-0 dhidi ya Yanga.

 

Jana Simba ilikuwa na uhitaji mkubwa wa kushinda mchezo huo ili kutangaza ubingwa mapema, lakini Yanga imetibua sherehe zao hizo ambapo sasa wanasubiri hadi Jumatano ijayo watakapocheza dhidi ya KMC uwajani hapo kufufua matumaini yao ya ubingwa.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, katika mchezo wa jana waliingia kwa kujiamini zaidi kutokana na ubora wa kikosi chao kulinganisha na kile cha Yanga.Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 70 ambazo kwa asilimia kubwa, zinawapa nafasi ya kumaliza juu ya Azam iliyopo nafasi ya tatu kwa sasa. Azam ina pointi 64, zote zikibakiwa na mechi mbili.

Simba inaendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 73, imebakiwa na mechi nne kumaliza msimu huu ambapo inahitaji pointi nne kwa sasa kuwa mabingwa.Timu hizo msimu huu mpaka sasa zimekutana mara tatu, mbili ikiwa Ligi Kuu Bara na moja Fainali ya Kombe la Mapinduzi ambapo Yanga imeshinda mechi mbili na sare moja.Julai 25, mwaka huu, wakongwe hao wa soka Tanzania, watakutana katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ikiwa ni mara ya nne msimu huu kukutana.

 

NABI AVUNJA REKODI YA GOMES

Kocha Nabi anakuwa wa kwanza kuifunga Simba ndani ya Ligi Kuu Bara tangu iwe chini ya Didier Gomes ambaye alikabidhiwa mikoba hiyo Januari 26, mwaka huu akichukua mikoba ya Sven Vandenbroeck.Gomes aliongoza Simba kwenye mechi 14 bila ya kupoteza, akajikuta ya 15 akifungwa katika Dabi ya Kariakoo.

Wakati Nabi akivunja rekodi hiyo ya Gomes, kwa upande wake ushindi huo ni mwendelezo wa matokeo mazuri ndani ya Ligi Kuu Bara tangu alipopoteza mechi ya kwanza dhidi ya Azam.

 

Kocha huyo aliyeanza majukumu ndani ya Yanga Aprili 25, mwaka huu akichukua mikoba ya Cedric Kaze, mpaka sasa ameiongoza timu hiyo kucheza mechi sita, ameshinda nne, sare moja na kupoteza moja.

 

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Gomes alisema: “Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri sana, vijana wangu walipata nafasi nyingi wakashindwa kuzitumia, hivyo sina wa kumlaumu zaidi ya lawama zote nazichukua mimi.

 

Tunajipanga kwa mchezo ujao, huu ushapita.”Kwa upande wa Nabi, alisema: “Niliingia kwenye mchezo huu nikiwa najiamini sana kwa sababu niliwahi kukutana na Simba nikiwa Al Merrikh, hivyo nawafahamu vizuri. Nawapongeza vijana wangu kwa kazi kubwa waliyoifanya.


MZEE MPILI ATAJWA NYOTA WA MCHEZO

Mashabiki wengi wa Yanga, jana walimtaja shabiki na mwanachama wa klabu hiyo, Mzee Mpili kutoka Ikwiriri mkoani Pwani kama ndiye nyota wa mchezo kutokana na maneno yake ya kishujaa aliyokuwa akiyatoa kabla ya mchezo.

Mzee Mpili aliyejizolea umaarufu mkubwa kwa siku za karibuni, aliwahi kusema ana uhakika mchezo huo watashinda kwani ana watu wa kuifanya kazi hiyo, na ikawa kweli.Kauli ya Mzee Mpili aliitoa wakati mashabiki wengi wa Yanga wakiwa na hofu juu ya kwenda kuikabili Simba iliyoonekana kuwa hatari.Kitendo cha jana Yanga kuibuka na ushindi, sasa kila mmoja ameibuka na kusema Mzee Mpili ndiye nyota wa mchezo huo.

STORI NA WILBERT MOLANDI, DAR ES SALAAM | SPOTI XTRA


Toa comment