The House of Favourite Newspapers

MASHEHE WAPONDA SADAK A YA DIAMOND!

LICHA ya kuonekana kuwa na dhamira njema ya kutoa sadaka/ zaka katika Sikukuu ya Idd, baadhi ya mashehe waliozungumza na Ijumaa Wikienda wamemkosoa mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ wakidai kuwa hakupaswa kufanya kwa staili ile ya ‘maonesho’.

NI IJUMAA ILIYOPITA

Diamond aliendesha zoezi la kugawa sadaka/zaka (mwenyewe aliita mkono wa Idd) kwa wakazi wa Tandale jijini Dar, Ijumaa iliyopita (wakati wa Sikukuu ya Idd) ambapo mamia ya watu walionekana wakiwa wamepanga mstari kufuata sadaka hiyo aliyokuwa akitoa Diamond.

‘FULL MAKAMERA’

Jambo hilo Diamond alilifanya huku kamera mbalimbali zikimulika ambapo siku iliyofuata, picha za tukio hilo zilipamba vyombo mbalimbali vya habari yakiwemo magazeti.

WADAU WAHOJI

Mara baada ya picha hizo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya wafuasi wa mitandao hiyo walihoji kitendo hicho cha Diamond kufanya jambo hilo la kiimani kwa kujionesha.

Wachangiaji wengi walisema kama alikuwa na dhamira njema, alipaswa kutoa kwa siri kwani kwa kufanya maonesho ni kuonesha kwamba unajivuna kwa kuwa na fedha nyingi. “Hii anayoifanya ni sifa. Angeweza kutoa sadaka ama zakatul fitri kimyakimya na kila mmoja angemuelewa kuliko hivi alivyofanya,” alichangia mdau mtandaoni na kuongeza:

“Mimi ni muislam na ninachofahamu ni kwamba, sadaka na zaka vinatolewa kwa watu wasio na uwezo na inashauriwa kuwa, ili kutoonekana unamdhalilisha yule unayempa, basi ufanye kwa siri na Mungu atakulipa, lakini mwenzetu huyu kafanya kama wanavyofanya mapedeshee kule mtaani.”

WENGINE WAMPONGEZA

Pamoja na wafuasi wengi kumkosoa, wapo baadhi ya wachangiaji wa mitandao ya kijamii waliompongeza kwa kusema amefanya sahihi na hawakuona tatizo.

“Kutoa ni kutoa, inategemea unatoa baada ya kutia nia gani. Sidhani kama Diamond alipokuwa anatoa alikuwa na nia ya kujionesha kuwa anazo sana, ninachoamini aliona kwa kuwa ni siku ya Idd awasaidie wengine kwa staili ile, mimi sioni tatizo,” alisema Sadik Jumbe ambaye ni mmoja wa walionufaika na sadaka hiyo ya Diamond.

MASHEHE SASA

Mara baada ya kukusanya maoni mbalimbali ya wadau mitandaoni, Ijumaa Wikienda lilizungumza na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislam wakiwemo mashehe ili kupata mtazamo wao kwa kitendo hicho alichokifanya Diamond.

Shehe Abdulhaman Jumaa wa msikiti mmoja uliopo Makongo Juu jijini Dar, alisema kitendo cha kutoa sadaka ama zaka kwa kuweka matangazo si kizuri kwani sadaka inapaswa kutoka moyoni na hata mtu wa pembeni yako asijue.

“Sadaka inabidi uitoe kwa siri ndio maana tunaambiwa kwamba ikiwezekana kama mkono wa kulia ndio unaotoa basi mkono wa kushoto hata usijue. Mimi nimeona alichofanya Diamond, kiimani haikuwa sahihi. “Unajua pale watu wengi sana watamsifia kwa kufanya kile alichofanya lakini kwa Mungu hana chake, ile tunaita ria. Yaani ni sawa na kwenda msikitini, unasali kisha unajipiga selfie halafu unaposti, hapo huwezi kupata dhawabu,

“Ndicho alichofanya Diamond, tena sana ingekuwa labda wakati anatoa ile sadaka ama zaka, waandishi wakambabatiza lakini yeye hakuwa tayari kujianika, hapo ingekuwa kitu kingine, lakini pale unaona hadi TV yake ilikuwepo, ina maana alikuwa kajiandaa kujitangaza, siyo sawa ” alisema Shehe Jumaa.

SHEHE MWINGINE

Aidha, shehe Nassor wa Buguruni aliponda vitendo vya namna hiyo huku akielezea suala hilo kwa upana zaidi.

“Sio huyo Diamond tu. Siku hizi naona kuna watu wanakwenda kwa watoto yatima sijui wanakusanya kabisa wanahabari, wanaweka picha zao mitandaoni jambo ambalo halimpendezi Mwenyezi Mungu.

“Sadaka ama zaka toa bila kujionesha, itoe bila kufanya sifa ya aina yoyote. Sadaka ni wewe, moyo wako na Mungu wako. Hata sisi mashehe hatupaswi kujua ulichotoa wewe,” alisema shehe Nassor.

Mashehe wengine waliozungumza na Ijumaa Wikienda wakiomba kutotajwa majina yao walisema wazo la Diamond kuwakumbuka ndugu zake wa Tandale lilikuwa zuri lakini alikosea kujianika.

“Angepata thawabu nyingi sana kama jambo lile la kuwapangisha watu foleni lingekuwa limefanyika kwa siri.

“Unajua kumsaidia mtu kitu halafu ukamuanika ni kumdhalilisha, kama kweli una moyo wa kumsaidia, msaidie bila kumuanika hadharani,” alisema mmoja wa mashehe hao.

DIAMOND ALIITA ‘MEDIA’?

Licha ya kutopatikana na kuzungumzia hilo lakini kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliweka ‘bango’ lililowataka watu kujitokeza kupokea mkono wa Idd.

“Leo kuanzia saa tano asubuhi nitakuwepo nyumbani Tandale nikitoa mkono wa Eid Mubarak kwa ndugu jamaa na marafiki…tafadhali nawakaribisha wote…,” aliandika Diamond.

Hata hivyo siku hiyo Diamond alitoa mifuko iliyodaiwa kuwa na nyama na mchele (mara nyingi zakatul fitri inakuwa ni vibaba viwili vya chakula, hasa mchele ama pesa inayotosha kununulia chakula hicho). Wengine Wengine waliofika eneo hilo waliambulia pesa kiasi cha buku tano tano.

SHEHE MKUU ANENA

Kwa upande wake shehe Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salim alipozungumza na Ijumaa Wikienda alisema hajaziona picha na kusema, kama atakuwa ametoa sadaka inayokubalika atapata thawabu zaidi.

“Ukitoa sadaka kama hivyo hata kama alikuwa amefanya kitu kibaya kwa kutoa sadaka anakuwa amesafishika,” alisema Alhad

STORI: Mwandishi Wetu, DAR

Comments are closed.