Mashindano ya Kusaka Vipaji Yaibua Timu 4 Zitakazoshiriki Safari Lager Cup
Timu nne zenye wachezaji 22 kila moja kutoka Mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam, zimetangazwa kushiriki katika mashindano ya Safari Lager Cup ambayo yana lengo la kuibua vipaji vipya katika soka.
Msemaji wa mashindano hayo, Mbwiga Mbwiguke amesema wachezaji hao wamepatikana baada ya mchujo kwenye mabonanza yaliyofanyika kwenye mikoa hiyo.
“Kama tulivyowaarifu hapo awali, zoezi hili lilishirikisha mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha na hatimaye Dar es Salaam ambapo makocha mahiri Jamhuri Kihwelo na Sekilojo Chambua walikuwa na kazi ngumu ya kuchagua kikosi cha wachezaji 22 kwenye kila mkoa kutokana na mabonanza mbalimbali waliyoshiriki baada ya usaili,”alisema.
Alisema hatua inayofuata sasa ni timu hizo nne kushindanishwa na kisha makocha watachagua timu moja itakayojulikana kama Safari Lager Champions ambayo hatimaye itacheza na timu mojawapo ya Ligi Kuu Tanzania.
Meneja wa Bia ya Safari Lager Pamela Kikuli, aliwapongeza makocha Jamhuri Kihwelo na Sekojo Chambua Kwa kuendesha zoezi Hilo Kwa weledi mkubwa na kutumia uzoefu wao kuchagua timu hizo.
Alisema bia ya Safari, ambayo ni ya mabingwa iliamua kuja ya kampeni hii ili kuibua vipaji vipya kabisa vya mpira wa miguu kwani wanaamini kuna vipaji vingi nchini ambavyo havijaibuliwa.
Aliongeza kuwa hatua inayofuata itakuwa na msisimko mkubwa kwani timu nne zilizochaguliwa zitachuana ili kupata timu moja ya wachezaji 22 itakayocheza na timu ya Ligi Kuu.
Kocha Kihwelo alisema zoezi limefanikiwa Kwa asilimia 90 hasa ikizingatiwa kuwa ndio mara ya kwanza na waliojitokeza walikuwa wengi zaidi na wao kama makocha walikuwa na kibarua kigumu kuchuja kwani katika mikoa yote minne kulikuwa na vipaji vya kipekee.
“Sio kwamba walioachwa ni wabaya, ni kwba tu walihitajika 22 lakini kiwango Cha vipaji Kiko juu na tunaishukuru Safari Lager Kwa kuona umuhimu wa kuibua vipaji vya mpira wa miguu kwani wengi walikuwa wanakosa nafasi ya kutoka,” alisema na kutoa wito Kwa vilabi mbalimbali vyenye programu ya U-20 kuwatumia vijana walioachwa Kwa kuwa wana vipaji vya hali ya juu.
Kocha Chambua alisema zoezi Hilo lilikuwa ya aina yake kwani limedhihirisha kuwa kuna vipaji vya hali ya juu katika mikoa mbalimbali na kutoa wito Kwa makampuni mengine yaige mfano wa Safari Lager na kutenga fedha na rasilimali Kwa ajili ya kuibua na kukuza vipaji.
“Zoezi lilikuwa gumu maana Kuna vipaji vya hali ya juu. Tulitamani tuwachukue wote lakini nafasi zilikuwa 22 tu Kwa kila Mkoa. Tumearifiwa kuwa zoezi hili ni endelevu Kwa hivyo tunaamino mwakani litakuwa kubwa zaidi ili Safari Lager iendelee kuibua vipaji zaidi.
Bia ya Safari Lager imewahi kudhamini mashindano ya Taifa Cup ambayo yalishirikisha mikoa yote ya Tanzania kwa lengo la kuibua vipaji.