The House of Favourite Newspapers

Mashindano ya Mbunge waMbulu Vijijini ni Mpasuano

MASHINDANO ya Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay maarufu kama Flatei Cup yameendelea kushika kasi katika Uwanja wa Shule ya Msingi Haydom huku yakitarajiwa kufikia tamati Jumapili hii.

Mashindano hayo yanashirikisha zaidi ya timu 12 kutoka Jimbo la Mbulu Vijijini ambazo ni Qubush FC, Young Boys FC, Endanachan FC, Santa Junior FC, Barazani FC, Maretadu FC, Hayedarer FC, Gidamadoy FC, Endagwe FC, Mewadan FC, Makuyuni FC, Home Boys FC, Mahaha FC na Mangafi FC.

 


Muandaaji wa mashindano hayo mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay amesema anachokifanya ni kuunga mkono juhudi za serikali kuendeleza michezo Lakini pia kutoa burudani kwa wakazi wa Mbulu.

Amesema ameanzisha kombe hilo kwa lengo la kuibua vipaji ili vijana wengi waweze kuiona sanaa na michezo kama kazi, kupinga matumizi ya dawa za kulevya, lakini pia kurejesha heshima ya soka ambayo kwa sasa imepotea katika Wilaya ya Mbulu.

 


Amesema mashindano hayo pia yanalenga kuwasaidia vijana kujiepusha na tabia hatarishi ikiwemo unywaji wa pombe, bangi, uasherati ili wajikite katika kufuatilia michezo hasa wa mpira wa miguu.

 

Flatei pia amewaomba walimu wa shule za msingi na sekondari za Wilaya ya Mbulu kutambua kuwa wanajukumu la kuhakikisha wanaibua vipaji vya michezo kuanzia shuleni ili kuwapa fursa vijana waweze kushiriki mashindano ya Umitashumta na Umiseta na wote wenye dhamana ya michezo wafanye kazi yao.

 


Mratibu wa mashindano hayo, Joseph Nikodemas ambaye ni katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Mbulu (MBDFA) alisema mashindano yalianza kufanyika Julai 13 mwaka huu ambapo michezo ya netiball, soka kwa wanawake na wavu inachezwa.

 

Amesema zawadi za mwaka huu zimeboreshwa zaidi tofauti na mwaka jana ambapo bingwa alijinyakulia kombe na kitita cha shilingi laki tano, seti ya jezi na mipira miwili, mshindi wa pili akapata fedha laki mbili na nusu, seti ya jezi na mipira miwili, wa tatu akaondoka na shilingi laki moja na nusu, jezi na mpira mmoja.

 


Amesema kwa sasa mashindano hayo yako katika hatua ya nusu fainali ambapo nusu fainali ya kwanza iliyopigwa jana timu ya Maretadu FC waliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Barazani FC, huku nusu fainali ya pili ikitarajiwa kupigwa leo kwa kuikutanisha Home Boys FC dhidi ya Endanachan FC.

 

Amewataka wadau wa soka na wachezaji watumie mashindano hayo ya Flatei Cup kujiandaa kuelekea Ligi ya Wilaya ya Mbulu itakayoanza hapo baadaye.

#Habari na Kennedy Lucas, Manyara

Comments are closed.