The House of Favourite Newspapers

Mashine mpya Yanga kuanza kazi dhidi ya Ruvu Shooting

HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba yule kiungo wao mshambuliaji wa kimataifa aliyetua hapa nchini hivi karibuni akitokea DR Congo, Reuben Bomba, anadaiwa kumalizana na uongozi wa klabu hiyo na ataanza kuitumikia timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting.

 

Yanga itapambana na Ruvu Shooting katika mchezo wa ligi kuu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wiki ijayo.

 

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo Championi Ijumaa limezipata zimedai kuwa, Bomba tayari ameshamalizana na Yanga na kesho ataanza mazoezi na kikosi cha timu ambacho kitakuwa kikijiandaa kwa ajili ya mechi dhidi ya Biashara United ya Mara itakayochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar. Mechi hiyo Bomba hatacheza.

 

“Wakati tulipokuwa Mbeya katika mechi yetu na Prisons, Bomba tulimuacha Dar akiwa na viongozi wetu wengine kwa ajili ya mazungumzo naye, wamefika sehemu nzuri.

 

“Kwa lugha nyingine tunaweza kusema kuwa tumemalizana naye na kilichobakia ni yeye kusaini tu, lakini mpango uliopo sasa kama mambo yatakuwa sawa basi tunataka mechi dhidi ya Ruvu Shooting aweze kuanza kuitumikia timu yetu,” kilisema chanzo hicho cha habari.

 

Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika alisema: “Kila kitu kuhusiana na Bomba kinaenda vizuri lakini mambo mengine yote yatajulikana hivi karibuni kwani tulikuwa Mbeya na baadaye Rukwa.

“Ila mazungumzo yetu naye yamefikia sehemu nzuri kwa hiyo kila kitu kuhusiana na yaye kitajulikana hivi karibuni.”

GIGY MONEY; Mimi ni mzuri wanaume wanapagawa

Stori Sweetbert Lukonge | Championi Ijumaa

Comments are closed.