The House of Favourite Newspapers

Mashoga wambipu Makonda, wakiona

0

MakondaMkuu wa Mkoa, Paul Makonda.

Na Mwandishi wetu, RISASI MCHANGANYIKO

DAR ES SALAAM: Watu tisa wanaodaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja (mashoga), wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni wakituhumiwa kukusanyika kinyume cha sheria kwa lengo la kupinga amri ya Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda ya kupiga marufuku vitendo vya mapenzi ya jinsia moja jijini hapa.

MASHOGA (1)Watuhumiwa hao.

Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, watu hao walikamatwa baada ya polisi kuvamia kwenye Ukumbi wa baa ya Matema uliopo Kinondoni B ambako zaidi ya wanaume 200 wanaodaiwa kuwa mashoga, walikusanyika kwa lengo la kujadiliana kwa kina kuhusu amri ya Makonda ya kuwapiga marufuku ili kutoa tamko la pamoja.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake, alienda kuonana na uongozi wa Ukumbi kwa maelezo kuwa wanauhitaji kwa ajili ya kufanyia sherehe ya kuzaliwa (birthday) ya rafiki yao.

“Meneja wa ukumbi alimhoji anategemea kuwa na wageni wangapi ili apime uwezo wa ukumbi wake, akamjibu kwamba wanaweza kuwa kati ya 200 hadi 300, kwa kuwa ukumbi ni mkubwa, walikubaliana ambapo mwanamke huyo alifanya malipo kabisa,” kilisema chanzo chetu.

MASHOGA (3)SIKU YA TUKIO ILIVYOKUWA

Siku ya tukio, chanzo chetu kinasema meneja wa ukumbi, wahudumu na wateja wengine waliokuwa wakiendelea kupata vinywaji, walishtushwa na kundi la wanaume tata walioanza kuwasili ukumbini hapo kwa makundi.

“Walikuja na magari ya kifahari, watu wakawa wanahisi huenda kuna kiongozi au mtu maarufu anakuja, lakini tukawa tunashangaa wote wanaoshuka, wana dalili za ushoga,” kilisema chanzo chetu na kuongeza kuwa, uongozi wa ukumbi ulishindwa cha kufanya kwa sababu tayari ulishapokea fedha zote.

Inadaiwa baada ya muda mfupi, eneo lote lilikuwa limefurika, wakaingia ukumbini huku wengine wakiendelea kuwasili na wengine wakiwa kwenye magari yaliyokuwa yamepaki nje ya ukumbi huo.

MASHOGA (2)AJENDA YAO KUBWA

“Nasikia ajenda yao kubwa ya kukutana, ilikuwa ni kupinga amri ya mkuu wa mkoa ya kupiga marufuku mapenzi ya jinsia moja. Kabla ya siku hiyo, unaambiwa tayari walishakuwa na vikao vidogovidogo katika maeneo mbalimbali ya jiji na siku hiyo ndiyo walikubaliana kufanya kikao kikubwa ili kutoa tamko rasmi,” kilisema chanzo chetu kilichoshuhudia tukio hilo mwanzo mwisho.

Ni wakati huo ndipo kamanda mmoja wa kitengo cha OFM (Operesheni Fichua Maovu) cha Global Publishers alipotonywa, sambamba na askari Polisi ambao walipowasili, walilizingira eneo hilo.

Askari mmoja alimfuata meneja wa baa na kuzungumza naye, bila shaka akimhoji juu ya kilichokuwa kinaendelea. Ghafla polisi wenye silaha wakivamia eneo hilo na kuvunja kikao hicho pamoja na kuanza kuwakamata.

OFM ilishuhudia purukushani kali ya aina yake baina ya wana usalama na wanaume hao, lakini kwa kuwa watata hao walikuwa wengi, waliwazidi ujanja na wengi wao kufanikiwa kukimbia.

Baada ya kukamatwa, mmoja wa vijana hao anayedaiwa kuwa ni mtoto wa kigogo wa Polisi, alimpigia simu baba yake ambae kupitia simu ya mtoto huyo, aliomba kuongea na askari aliyeonekana kuwa kiongozi wa operesheni hiyo, aliyejulikana kama Afande Makomeo ili aangalie jinsi ya kumsaidia mtoto wake, lakini askari huyo alikataa akidai mbele yake kuna OFM huku pia akisema mkuu wa mkoa ameshaambiwa idadi ya waliokamatwa.

OFM iliwashuhudia vijana hao tisa wakipakizwa kwenye gari lililotumiwa na Polisi, Toyota Noah lililokuwa na namba za usajili T980 CMQ na kupelekwa katika kituo cha kidogo cha Polisi cha Mwinjuma, kabla ya baadaye kuhamishiwa Oysterbay.

Katika mtiti huo, inaelezwa kuwa meneja mkuu wa baa hiyo alitoweka akihofia usalama wake kwani mashoga hao walikuwa wakimtuhumu kwamba ndiye aliyewachoma kwa polisi.

Akizungumza na gazeti hili kwa niaba ya meneja mkuu, John Magazini, ambaye ni meneja burudani wa baa hiyo, alisema wakati wakichukua fedha za ukumbi huo, hawakuelewa kama utatumiwa na mashoga.

Gazeti hili lilimtafuta kwa simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, ambaye awali alipopokea na kusalimiwa, ikakatika. Kuanzia wakati huo (saa saba mchana Jumatatu hadi saa kumi jioni) simu yake haikuwa ikipatikana hewani ili kuzungumzia suala hilo.

Leave A Reply