The House of Favourite Newspapers

Mastaa 10 Bongo Wanavuta Mkwanja wa Kutisha

0

KWA sasa muziki ni biashara kubwa mno na wateja wa biashara hii ni wasikilizaji na watazamaji kutoka kila pembe ya dunia kupitia teknolojia ambayo kwa wengine imekuwa ni fursa kubwa; achana na wale wanaoitumia vibaya na kuwapotezea muda.

 

Makala haya ya Gazeti la IJUMAA yanaangazia mitandao mikubwa minne ya kimataifa ya kusikiliza, kutazama, kuuza na kununua muziki inayotumiwa na mastaa wa Bongo Fleva na kutengeneza mkwanja wa kutisha.

 

Hii ni Spotify, Audiomack, YouTube na Boomplay; hii inaonesha kiwango cha wasikilizaji na watazamaji wanaofuatilia muziki na wasanii wanaowashabikia.

 

Ifuatayo ni listi ya mastaa 10 wa Bongo Fleva wanaouza zaidi kwenye mitandao hiyo; kumbuka, kadiri msanii anavyokuwa na streams na views nyingi, ndivyo anavyoingiza pesa za kutosha.

 

1; DIAMOND PLATNUMZ

Nasibu Abdul (Simba au Dangote) amezaliwa Oktoba 2, 1989. Ni staa mkubwa wa muziki Bongoland; mfanyabishara na mwanzilishi wa lebo ya muziki ya Wasafi Classic Baby (WCB) na pia ni mmiliki wa vyombo vya habari vya Wasafi Media.

 

Katika listi hii, yeye anashika namba moja akiwa na zaidi ya streams na views bilioni 1.6 ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya msanii yeyote Bongo; maana yake ni kwamba ukizigeuza kuwa pesa, basi ni mabilioni ya shilingi.

 

2; RAYVANNY

Raymond Shaban Mwakyusa (Rayvanny au Chui), amezaliwa mwaka 1993. Ni ni msanii aliye chini ya lebo inayomilikiwa na Diamond Platnumz. Chui anafanya vizuri huku katika mauzo ya mtandaoni, yeye anashika nafasi ya pili kilingana na watazamaji na wasikilizaji kwenye mitandao hiyo mikubwa minne.

 

Rayvanny ana zaidi ya wasikilizaji na watazamaji milioni 664 ambazo hizo zote ni mkwanja mzito.

 

3; HARMONIZE

Rajabu Abdul Kahali almaarufu Harmonize Konde Boy Mjeshi amezaliwa Machi 15, 1994. Ni msanii mwenye majina mengi kama Jeshi, Tembo, Chinga na mengine. Pia ni mwanzilishi wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide yenye wasanii kadhaa. Yeye anashika nafasi ya tatu akiwa na zaidi ya wasikilizaji na watazamaji milioni 661 wanaomuingizia mamilioni ya pesa.

 

4; MBOSSO

Mbwana Yusf Kilungi au Mbosso Khan ambaye ni masta wa ngoma za malavu ni miongoni mwa wasanii waliosainiwa chini ya WCB YA Diamond. Anashika nafasi ya nne kulingana idadi ya watazamaji na wasikilizaji wengi kupitia mitandao hiyo mikubwa minne ya kimataifa. Mbosso ana zaidi ya wasikilizaji na watazamaji milioni 440 ambao wanampa pesa za kutosha.

 

5; ZUCHU

Zuhura Othman Soud au Zuchu amezaliwa mwaka 1993. Ni mkali mwingine aliye chini ya Lebo ya WCB ya mtu mzima, Simba. Ni mtoto wa mwimbaji maarufu Afrika Mashariki na Kati, Bi Khadija Kopa. Mapema mwaka jana, Zuchu alitajwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC) kuwa ni msanii anayekuja kwa kasi na kuangaliwa zaidi mwaka 2021.

 

Yeye ana zaidi ya wasikilizaji na watazamaji milioni 324 wanaomfanya kuwa mrembo kinara anayeingiza mkwanja mrefu kupitia mauzo ya muziki wake kwenye mitandao hiyo.

 

6; KING KIBA

Anaitwa Ali Salehe Kiba au King Kiba. Amezaliwa Novemba 29, 1986. Ni lejendi wa Bongo Fleva ambaye haishi ladha maana ngoma zake huwa zinaishi. King Kiba anashika nafasi ya sita. Hii ni kulingana na idadi ya watazamaji na wasikilizaji katika mitandao hiyo. King kiba ana zaidi ya watazamaji na wasikilizaji milioni 184 wanamng’arisha kwa mkwanja wa kutosha.

 

7; LAVA LAVA

Abdul Juma Iddi almaarufu Lava Lava amezaliwa mwaka Machi 27, 1999. Ni miongoni mwa wasanii wa Bongo Fleva waliosainiwa chini ya Lebo ya Wasafi. Yeye anakimbiza akiwa nafasi ya saba na zaidi ya wasikilizaji na watazamaji milioni 171.

 

8; NANDY

Faustina Charles Mfinanga unaweza kumuita The African Princess. Anawawakilisha vyema akina dada akiwa nafasi ya nane kwenye listi hii ya kumi bora. Nandy amefanikiwa zaidi kwenye Bongo Fleva kwa muda mfupi kutokana na ladha na kipaji chake cha pekee kisha kutamba na tamasha lake mwenyewe la Nandy Festival. Nandy ana wasikilizaji na watazamaji zaidi ya milioni 168 ndani na nje ya Bongo.

 

9; DARASSA

Huyu ni Sharif Thabeet almaarufu Darassa ni miongoni mwa wasanii walioanza harakati za kimuziki kwa muda mrefu.

Darassa anajulikana kwa kufanya hit songs za kitaifa kama Muziki. Jamaa anashika nafasi ya tisa akiwa ni kati ya wasanii wachache wa Hip Hop Bongo waliosikilizwa zaidi.

Darassa ana zaidi ya wasikilizaji na watazamaji milioni 84 kwenye mitandao hiyo pekee.

 

10; MARIOO

Omari Mwanga au Marioo anatajwa kukamata gemu ndani ya muda mchache na kutoboa kupitia muziki wake wenye ladha ya kitofauti. Marioo anajulikana kwa ngoma zake za kuchezeka. Yeye anafunga nafasi ya mwisho kwa kuzingatia watazamaji na wasikilizaji katika mitandao hiyo minne mikubwa ambayo tumeifanyia uchambuzi. Marioo ana zaidi ya watazamaji na wasikilizaji milioni 72 wanaompa jeuri ya pesa za kutosha.

MAKALA; BAKARI MAHUNDU, BONGO

Leave A Reply