Mastaa Acheni Mbwembwe za Kufuturisha Fanyeni Haya Tu!

WAISLAM duniani kote wako kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kama ilivyo kawaida baadhi ya mastaa wamekuwa wakionesha kuuheshimu ipasavyo mwezi huu. 

 

Heshima ambayo wamekuwa wakiionesha ni katika kubadilisha mifumo ya maisha yao. Wapo ambao kabla ya Mwezi Mtukufu walikuwa wakifanya mambo ya ajabuajabu kama kunywa pombe, kuzini, kuvaa nguo za ajabuajabu na kutenda mambo mengine ambayo hayamfurahishi Mungu.

 

Lakini ulipoingia mwezi huu nimekuwa nikiona mastaa wakionesha kubadilika, ukiwaona wakati mwingine huwezi kuamini kama ni wao.

 

Kinachotia moyo zaidi ni kwamba, si waislam tu, hata baadhi ya mastaa wakristo wamekuwa wakiwasapoti wenzao katika kuupitisha mwezi huu kwa kufunga na hata kujiweka mbali na maovu. Niseme tu kwamba hili ni jambo jema sana.

 

Lakini pia inapofika wakati kama huu, wapo mastaa ambao miaka ya nyuma kidogo walikuwa na tabia ya kufuturisha watu. Wapo ambao wamekuwa wakitumia pesa nyingi kuandaa futari na kuwaalika watu majumbani kwao kama siyo kwenye kumbi mbalimbali.

 

Kwa taratibu za kiislam, kufuturisha ni jambo jema sana na endapo utafuata taratibu, lazima upate thawabu na katika hili wapo ambao wamekuwa wakifuata taratibu ikiwa ni pamoja na kuwafuturisha wale wasio na uwezo tena katika mazingira yasiyo na athari kiimani.

Lakini katika miaka hiyo; (hapa nazungumzia kipindi kile ambacho pesa ilikuwa siyo tatizo), mastaa walikuwa wakifuturisha kama fasheni tu. Baadhi walikuwa hawafuati hata utaratibu uliowekwa. Walikuwa wanafuturisha hata ambao hawajafunga, tena watu ambao wanao uwezo wa kujifuturisha.

 

Kwa kufanya hivyo ikafika wakati ikaonekana mastaa walichokuwa wanafanya wala hakikuwa kufuturisha bali kulisha watu chakula cha jioni kama siyo cha usiku. Kimsingi waliokuwa wakifanya hivyo dhawabu zilikuwa zikiwapitia pembeni na walichokuwa wakiambulia ilikuwa ni sifa tu.

 

Kipindi hicho cha kufuru za mastaa kufuturisha kikapita, kikaingia kipindi ambacho mastaa walikuwa na hali ngumu sana kipesa. Ile mianya ya kupata pesa kirahisi ilipozibwa na Rais John Pombe Magufuli, mbwembwe za mastaa kufuturisha zikazima.

 

Walioendelea kufuturisha wakawa ni wale ambao walifanya kwa ajili ya kupata thawabu na haikuwa kwa kufuru kama ilivyokuwa huko nyuma Mwaka jana kufuatia kukauka kwa zile mbwembwe za mastaa kufuturisha, baadhi walipoulizwa kulikoni wakafunguka hivi;

 

ZUENA MOHAMMED ‘SHILOLE’

“Mimi kwa sasa siwezi kufuturisha kwa sababu nina mgahawa wangu ambao watu wanafuturu, hivyo watu wanakuja kununua na mimi ndiye nawahudumia. “Pia hali ya sasa imekuwa tofauti na zamani, kwa sasa naangalia maisha yanaendaje, ila ningekuwa na pesa ya kutosha ningefuturisha nyumbani kwangu au katika ukumbi wowote ule.”

 

JACK WOLPER

“Mimi kwa sasa sipo Dar es Salaam, hata ningekuwepo ningeangalia mfuko wangu kama unatosha kufuturisha, maana haya mambo sasa hivi naona hakuna mtu anayeyaangalia sana, maisha ni magumu mno. “Kila mtu anatafuta jinsi ya kuishika shilingi na si vinginevyo, muhimu ni kuomba dua na kwenda kwa watoto yatima kutoa chochote kitu.”

 

IRENE UWOYA

“Mimi leo siwezi kuacha kufanya hivyo hata mara moja, nilikuwa nasubiria tu hili kumi la mwisho ili niweze kufuturisha, siwezi kukosa hizi thawabu.”

 

KAJALA MASANJA

“Unajua kufuturisha inabidi ujiandae, ila mimi kwa mwaka huu hali yangu kiuchumi haipo vyema, sina uwezo wa kufuturisha watu wengi kama nilivyofanya miaka ya nyuma, maana ukikurupuka unaweza kutowaridhisha watu unaowaalika.”

WEMA SEPETU

“Mimi sijashindwa kufuturisha, ila nilikuwa nasubiria muda nilioupanga ili nifanye, nategemea kufuturisha kwani bado Ramadhani haijaisha na ishu ya kusema hali ngumu, ni kweli ila mimi nitajitahidi ili niweze kualika watu ambao nitakuwa na uwezo nao.” Hayo ni maelezo ya mastaa kwa mwaka jana lakini leo hii waislam wakiwa kwenye chungu cha 8, sijasikia staa yoyote akizungumzia hili suala la kufuturisha.

 

Imani yangu ni kwamba, hata wakiulizwa kulikoni, majibu hayatatofautiana sana na yale ya mwaka jana. Sasa leo nina mambo nataka kuwashauri mastaa ili waweze kupata fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani badala ya kuumiza kichwa kwenye suala la kufuturisha.

 

La kwanza ni kufunga. Kama kweli unataka radhi za Mungu katika kipindi hiki, jitahidi kufunga. Nasema hivi kwa sababu mastaa wengine licha ya kwamba uwezo wa kufunga wanao, hawafungi lakini eti wanawaza kufuturisha, ukiwa miongoni mwao utakuwa ni mtu wa ajabu sana.

 

Pili fanya ibada! Kwenye ibada kuna mambo mengi sana, haiishii kwenda msikitini bali kujitahidi sana kufanya yale ambayo Mungu ametuamrisha kuyafanya na kuachana na yale ambayo ametukataza. Hiyo ndiyo ibada.

Katika hili la ibada linaingia suala la kusaidia wasio na uwezo. Hapa ndipo unaweza kufuturisha. Siyo lazima uite watu wengi nyumbani kwako, upike mapochopocho kibao.

 

Hapana! Andaa futari kulingana na uwezo wako, alika watu wenye uhitaji wa futari. Kama ukishindwa basi peleka futari kwenye vituo vya watoto yatima. Hili si kwa waislam tu, hata wale wakristo ambao wamekuwa na kasumba ya kufuturisha, utaratibu mzuri ni huu.

 

Ndiyo maana nikasema kwamba, kama mmeshindwa kufanya mbwembwe za kufuturisha kama mlivyokuwa mnafanya huko nyuma, bado kuna mambo madogo madogo ya kufanya yanayoweza kuwapa dhawabu kuliko kuwaza kufanya mambo makubwa ambayo hamna uwezo wa kuyafanya.


Loading...

Toa comment