The House of Favourite Newspapers

MASTAA BONGO: UTAJIRI HAUAMBUKIZWI KUPITIA TENDO LA NDOA

KUNA mwanaume mmoja alikuja nchini miaka michache iliyopita na ‘kuwaburuza’ dada zetu mastaa kama akatavyo. Kwa masikio yangu alinitamkia kuwa hakuna staa wa kike anayeweza kumgomea asitembee naye. “Nani? Labda nikuambie huyo nimeshatembea naye na siyo huyo tu…” alijisifu mbele yangu mwanaume huyo aliyejulikana kwa jina la Mkongo.

 

Kusema kweli wakati akisema hivyo na kuniunganishia na orodha ya mastaa wa kike aliotembea nao na wanaomtafuta kwa udi na uvumba niliumia. Nisiwekewe sababu kwamba; niliumizwa na wivu kwa yeye ‘kuwapitia’ mastaa hao, hapana! Nilihisi alitumia fedha kuwadhalilisha dada zetu.

 

Kwa muda mfupi Mkongo alitikisa nchi kwa ufuska wake, mwenyewe alikuwa bingwa wa kujigamba kwa orodha ndefu ya mastaa ‘aliowapitia’. Yote hayo Mkongo aliyafanya kwa sababu fedha zilimgeuza kuwa ‘chatu’ ambaye ‘mbwa’ hujipeleka mwenyewe kunaswa mtegoni.

 

Hadi leo sijui yuko wapi anafanya nini na endapo fedha bado anazo au alishafilisika na kubaki na picha za utupu za dada zetu wengi alizokuwa amejaza kwenye simu yake kama ushahidi kwamba kawachezea. Kimsingi nilikuwa nimesahau ishu ya ufuska wake; aliyenifanya nikumbuke yote hadi kuandika makala haya ni maneno ya mwanamitindo na mfanyabiashara kutoka Nairobi, Kenya, Huddah Monroe aliyoyatoa hivi karibuni.

Huddah aliwashauri wanawake wenzake masikini kwa kusema wasijirahisi kwa wanaume wenye fedha na kukubali kudhalilishwa kwa kudhani kwamba nao watatajirika kwa kufanya mapenzi na matajiri. Kupitia mtandao wake wa Instagram, Huddah aliandika maneno yaliyonigusa sana:

 

“Nimejihusisha kimapenzi na mabilionea, lakini sijawahi kuwa bilionea, utajiri haumbukizwi kupitia tendo la ndoa.” Mwanamitindo huyo alikwenda mbali na kuwashauri wanawake wenzake hasa maarufu kuwa wawe watumwa wa kazi zao na kamwe wasiwe watumwa wa ngono za matajiri kwa sababu hazitawatajirisha.

 

Maneno haya ni kweli kwa sababu mastaa ambao walikuwa wakipigana vikumbo kumgombea Mkongo leo hii hawana mbele wala nyuma. Enzi hizo kila staa aliyejirahisisha kwa Mkongo aligeuka pedeshee wa kike; tuliwashuhudia kwenye kumbi za starehe wakimwaga fedha majukwaani kutunza wanamuziki.

Ama kweli utajiri hauambukizwi kwa tendo la ndoa! Mkongo kaondoka Bongo na aibu ya dada zetu na kuwaacha wakiwa masikini. Kwangu mimi Huddah ni shujaa na mfano kwa wanawake wengi ambao wakiona fedha basi huchanganyikiwa kiasi cha kuwa tayari hata kuharibiwa heshima yao mbele ya jamii.

 

Ukisoma neno kwa neno ujumbe wa Huddah utagundua kuwa mwanadada huyo mrembo amejutia vilivyo makosa yake, ndiyo maana anawaasa wenzake wawe watumwa wa kazi zao binafsi na siyo ngono. Ujumbe huu ni ukombozi tosha kwa mastaa na wanawake ambao wanaamini kuwa maisha mazuri ni kuwa na bwana mwenye fedha atakayeweza kukufanya uishi maisha ya anasa na kusahau kuwa utajiri hauambukizwi kwa ngono.

 

Mara nyingi nimekuwa nikiwashauri mastaa wetu ambao wamefanikiwa kukuza majina yao katika jamii wageuze fikra zao kuhusu maisha yao yajayo. Uzuri ni maua uchanua na kunyauka, leo kama wanajiona wanaweza kumhudumia Mkongo na wenye fedha kwa kuwaridhisha kimapenzi; kesho uwezo huo hautakuwepo lakini maisha yao yatakuwepo na watatakiwa kuyaishi.

 

Nisiwe mwingi wa lawama na kusahau kuwapongeza wanawake wanaojituma na kuwa watumwa wa kazi zao bila kutegemea fedha za wanaume. Natambua jitihada za Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ambaye mbali na muziki anaendesha biashara ya kuuza chakula. Rita Paulsen, Mkurugenzi wa Benchmark Produduction, mwanamke mpambanaji, mbunifu na mwanzilishi wa Shindano la Bongo Star Search ‘BSS’ heshima iwe kwake.

Mwingine ambaye anaonekana kuanza kujitambua kwa sasa ni Wema Sepetu ambaye kutokana na mapito aliyopitia huenda amejifunza kupitia dunia ambapo kwa sasa anafanya biashara ya kuuza nguo. Orodha ya wasichana na mastaa ambao wanajitambua ni ndefu lakini nimalizie kwa kusema heshima kwa kila mwanamke anayeuheshimu utu wake na kutokuwa tayari kudhalilishwa na mwanaume kisa tu ana fedha.

 

Naomba mwaka 2019 uwe mwaka wa kufuta makosa yote yaliyotokea huko nyuma, uwe mwaka wa kila mwanamke kutumia kukataa kutumikishwa kingono ili apate fedha. Ujumbe wa Huddah ni kuwa, utajiri hauambukizwi kwa tendo la ndoa.

Comments are closed.