The House of Favourite Newspapers

MASTAA BONGO WAANDISHI WA HABARI KUTEMBELEA MRADI WA SGR

WASANII fani mbalimbali wamekutana na waandishi wa habari tarayi kwa ziara maalum ya kutembelea mradi mkubwa wa reli ya kisasa ya umeme (Standard Gauge Railway) unaotekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Reli nchini (TRC) unaojengwa na Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki.

 

Akizungumza katika mkutano huo Msanii wa filamu nchini ambaye pia ni mratibu wa msafara huo, Steve Nyerere amepongeza uongozi wa Shirika la Reli (TRC) kwa kuwapa fursa wasanii na kutambua mchango wao katika jamii.

 

Steve amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanikisha safari hiyo ambayo itawahusisha waimbaji wa muziki wa bendi, Bongo Fleva, Taarab, Singeli, Wigizaji wa Filamu , Bongo Movie, Komedi, Wachezaji wa zamani wa mpira wa miguu na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii.

Safari hiyo itaanza saa moja asubuhi kwa treni ya (TRC) kutoka Kamata jijini Dar es salaam na kupitia maeneo yote ambayo mradi huo unatekelezwa huku wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa mainjinia wa shirika la reli na wale wa kampuni ya Yapi Merkezi wanaojenga reli hiyo ya kisasa.

 

Steve pia ametumia mwanya huo kuwaambia wasanii hao kuhusu mikopo ambao inatolewa kwa wasanii kupitia Halmashauri za Mkoa wa Dar katika kutekeleza sera ya serikali ambayo inaziagiza halmashauri kutenga asilimia 10 ya fedha kwa ajili ya mikopo ya vijana, Walemavu na Wanawake.

 

“Mkuu wa Mkoa Paul Makonda anakaribisha maombi ya mkopo kwa wote wanaohitaji mikopo aliyohaidi wakati wa Mkutano wa wasanii mbalimbali, wanasoka wa zamani na waandishi wa habari nchini kuweza kupata mkopo huo utakaowezesha kufanya kazi kwa weledi na kukuza kipato kwa tasnia zote nchini.” alisema Nyerere.

 

Naye Kaimu Mkuu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa shirika la reli nchini (TRC) Jamila Mbarouk amesema ni fursa adhim kwa wasanii pamoja na waandishi wa habari kwa pamoja kupanda treni hiyo kwa lengo la kuangalia mradi huo na kuongeza kuwa safari hiyo itasaidia kutangaza utalii uliopo ndani hasa kuwepo kwa treni hiyo ya umeme ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo ya tani elfu 10 huku spidi yake ikiwa ni 160 kwa saa.

“Shirika la reli (TRC) limewapa kipaumbele wasanii ,Wacheza mpira,Ma MC ,Waimbaji,Wachekeshaji, Waigizaji wa Filamu na wengine ambao wanaweza kuwa mabalozi wazuri katika kuutangazia umma kuhusu mradi huo wa treni mpya ya umeme itakayotoka Dar es salaam -Morogoro hadi Dodoma ” alisema Mbarouk.

 

Aidha ameeleza kuwa reli hiyo inajengwa kwa fedha za watanzania wenyewe kutokana na kodi zinazokusanywa. Pia ametoa wito kwa wafanyabiashara kulipa kodi kwani mradi huo ukikamilika utasaidia kukuza uchumi pia kwa wafanyabiashara kwa kusafirisha bidhaa zao na mizigo mbalimbali kwa haraka zaidi.

Comments are closed.