The House of Favourite Newspapers

MASTAA BONGO WALIVYOFUNIKA KWA TUZO

DAR ES SALAAM: Usiku wa kuamkia juzi Jumatatu uliweka historia nyingine baada ya mastaa wanawake Bongo kufunika kwenye tuzo zilizokwenda kwa jina la AWAFFEST zilizolenga kutambua mchango wa mwanamke katika sanaa na ubunifu barani Afrika zikisimamiwa na staa wa Bongo Muvi, Yvonne-Chery Ngatwika ‘Monalisa’. 

 

Tukio hilo lililopewa jina la Tuzo za Monalisa lilijiri katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa (National Museum) uliopo Posta jijini Dar ambapo tuzo hizo zilitolewa kwa mara ya kwanza Bongo. Tukio hilo lililoshuhudiwa na gazeti hili lilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wasanii wa tasnia tofauti kuanzia Bongo Muvi, Bongo Fleva, Taarab, utangazaji na nyinginezo.

 

Katika tukio hilo, mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla ambaye aliibua gumzo kutokana na usiku wa jana yake kukesha kwenye Kampeni ya Tokomeza Ziro Kisarawe chini ya mkuu wa wilaya hiyo, Jokate Urban Mwegelo katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar kisha usiku huo kuwa kwenye tuzo hizo.

 

Baadhi ya mastaa wanawake wa Bongo waliochomoza na tuzo ni pamoja na Vanessa Mdee ‘Vee-Money’ na Hellen George ‘Ruby’ kutoka kwenye muziki wa Bongo Fleva.

WENGINE ni mwigizaji wa Bongo Muvi, Riyama Ally, Mtangazaji wa E-FM, Dina Marios na Khadja Kopa aliyepata tuzo ya mwanamke mwenye heshima kwenye sanaa ambaye ni mfano wa kuigwa na wanawake wenzake.

 

Mbali na hao, wengine waliopata tuzo ni wanawake kutoka nje ya Bongo kama Afrika Kusini na Nigeria.

 

Shughuli hiyo ilitumbuizwa na Khadja Kopa mwenyewe, Banana Zorro na Bi Shakila aliyekonga nyoyo za wengi na wimbo wake wa Mapenzi Yananitatiza. Akizungumzia tuzo hizo, Waziri Kigwangalla alimpongeza mno Monalisa na kueleza umuhimu wa tukio hilo kwenye sekta ya utalii.

Kwa upande wake Monalisa au Mona aliwashukuru wote walioshiriki kukamilisha zoezi hilo huku akisema ni mara ya kwanza hivyo zitaboreshwa kadiri zitakavyoendea kufanyika. AWAFFEST ni tuzo ambazo zinasimamiwa na Monalisa ambaye pia ni Balozi wa Tamasha la Filamu la Afrika (AFF).

Stori: Mwandishi Wetu, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.