MASTAA BONGO WANAVYOHENYA CHINA

MASTAA Bongo ambao ni wafanyabiashara wanaokwenda nchini China wamekuwa wakihenya pale wanapokwenda kusaka biashara ingawa wakifika hapa Bongo, hakuna anayeweza kujua mpaka wakujuze, hivi ndivyo Risasi Jumamosi lilivyochimba na kubaini ripoti kamili. 

 

Wamekuwa wakionekana kutanua na kuendesha magari makubwa wawapo hapa nchini lakini siri ya mafanikio yao ni huko China ambako wengi huenda kwa ajili ya kufanya biashara mbalimbali lakini kubwa ni hii ya kuchukua mizigo ya nguo, viatu na vifaa mbalimbali ambavyo wakati mwingine hulazimika kujitwisha kichwani.

 

USISTADUU PEMBENI

Risasi Jumamosi limebaini wawapo huko nje kibiashara huweka kando usistaduu na kubeba mizigo yao wenyewe badala ya kukodisha watu wa kubeba kwa malipo. Chanzo chetu kutoka China, kumetutonya kuwa mastaa wa kike tunaowaona huku Bongo wakiwa sopsop, wakienda kule hujitoa fahamu na kuwa makini na kubana matumizi ili kuingiza faida katika biashara husika.

 

“Mastaa wenu hapa China wakija huwa wanavuja jasho vilivyo kwani huja na pesa kidogo na kuamua kubeba mizigo wenyewe.

“Utawakuta mtaani kama si wao, tofauti na wakiwa Kariakoo ambako hutamani kila mahali kutumia usafiri au kubebesha watu mizigo, huku wao ndiyo huwaomba Wachina wawatwishwe mizigo yao,” alisema msichana anayetambulika kwa jina la Jamila aliyepo nchini China ambaye wakati mwingine mastaa wa huku humkodi ili awasaidie kwenda madukani.

 

Jamila alidai kuwa ukiwa China si rahisi sana kuyajua maduka yenye nguo nzuri na mali za bei nafuu hivyo hulazimika kuwakodi watu kwa kuwalipa ili wawafahamishe maduka hayo. “Suala la kubeba mizigo pia huwa ni jukumu ambalo watu hulipa pesa ili wabebewe, sasa kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuja na bajeti ndogo, hubeba wenyewe mizigo,” alisema Jamila.

 

Aidha alisema kuwa, wengi wao wakiwa Bongo huonekana wana pesa na kutembelea magari, lakini wakiwa China hupanda pikipiki na kutembea kwa muda mrefu kwani yapo maduka mengine ambayo huweka nguo kwa siku nyingi kitu ambacho usipopata wa kukuelekeza utanunua bidhaa ambazo zimechakaa zikiwa dukani.

 

MASTAA WAFUNGUKA

Baada ya Risasi Jumamosi kubaini mastaa hao kuhenya na kupata ushahidi wa picha kutoka kwa watu wa karibu waliopo huko, mwandishi wetu alifanya mahojiano na baadhi ya mastaa ambao walifunguka juu ya msoto wanaokutana nao huku China.

 

RUCKY BABY

Msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye anatamba na kibao cha Watabisha na staili yake ya kuvaa mavazi ya kihasarahasara, Rukia Jumbe ‘Rucky Baby’ alisema, China kuhenya ni kawaida sana labda kama mtu hataki kuwa na maisha mazuri.

 

“Mimi sidanganyi, nimeshabeba mizigo mingi sana ya watu kwa ajili ya kujiingizia pesa. Huko hakuna kuremba eti wewe ni staa, kule ni kazikazi kisha tukija Bongo tunatanua.

 

“Mimi nimeshaingiza pesa ndefu kwa kuwasaidia tu watu kuwapeleka madukani, lakini linapokuja suala la kubeba mizigo pia nimefanya sana na unalipwa pesa nzuri tu,” alisema Rucky. Rucky mbali na muziki amekuwa akifanya biashara za nguo na viatu kutoka China.

KHADIJA SHAIBU ‘DIDA’

Dida amewahi kuonekana akiwa amebeba mzigo akiwa nchini China ambapo aliandika ujumbe na kusema kuwa:

 

“Ukitaka kutafuta usiangalie watu wanasema nini juu yako, wewe zitafute tu na usikate tamaa maana Mungu hawezi kukuacha, Mungu awabariki watu wote wasiokata tamaa na bado wanaendelea kuzitafuta.” Dida aliandika maneno hayo hivi karibuni alipokuwa China ambapo alikwenda kuchukua bidhaa za kuuza dukani kwake wakati wa Sikukuu ya Pasaka.

 

FAIZA ALLY

Alipotafutwa Faiza alisema kuwa katika kitu ambacho hawezi kukionea aibu ni pale anapokuwa anasaka pesa, kwani hukidhi mahitaji ya wateja wake kwa kubeba mizigo bila kuona aibu na hapendi kulipa watu kwa ajili ya kumbebea mizigo ambayo yeye anaweza kuibeba.

 

“Nimekuwa nikibeba mizigo bila kuona aibu yoyote na ninaporejea Tanzania natumia pesa kwa sababu ya jasho langu, mimi ni mtafutaji hivyo ninapofika China naweka ustaa pembeni, nafanya kazi,” alisema Faiza.

 

Mbali na Faiza mwanadada anayejiita Doty (pichani akiwa kwenye pikipiki ukurasa wa mbele) naye ni miongoni mwa wafanyabiasha wakubwa ambao wamekuwa wakihenya nchini China wakati wa kufuata bidhaa za kuleta Bongo.

 

PONGEZI KWAO

Hata hivyo Risasi Jumamosi linawapongeza mastaa ambao huweka ustaa kando wakati wa kutafuta pesa na kuurejesha kwenye matumizi. Katika siku za hivi karibuni mastaa wengi wamekuwa wakienda China kwa shughuli mbalimbali, hivyo kuweza kutumia fursa zinazopatikana huko kama ambavyo Wachina wanavyokuja Bongo kutumia fursa zikiwemo za kufanya biashara ndogondogo.

Toa comment