The House of Favourite Newspapers

Mastaa Hawa Usishangae Kuwaona Wakikiwasha Bongo Msimu Ujao

0

 

                                                   Mshambuliaji wa Zanaco Moses Phiri

LIGI Kuu Bara msimu huu wa 2021/22 unazidi kupamba moto ukielekea ukingoni ambapo tayari baadhi ya timu tayari zimefanikiwa kucheza mizunguko 20 huku timu nyingine zikijiandaa kuingia kwenye mzunguko huo.

 

Achana na Yanga kuongoza Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya bingwa mtetezi, Simba ambaye yupo kwenye nafasi ya pili, stori kubwa kwa sasa ni kuhusu vita ya usajili.

Timu nyingi tayari zimeanza mapema vita hii ili kuwa na timu bora zaidi kwa msimu ujao.

Vita hii ni kali zaidi mitaa ya Kariakoo wanapopatikana watani wa jadi, Simba na Yanga ambapo wanahusishwa na majina makubwa kwenye soko la usajili na makala hii inaangazia baadhi ya majina yanayotajwa kutua katika klabu hizo, na haitashangaza kuona likitimia.

 

VICTORIEN ADEBAYOR

Kwa muda mrefu Simba wameonekana kuwa ‘serious’ na dili la staa huyu wa kikosi cha USGN ya Niger, ambapo uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ umekuwa na mazungumzo binafsi na mchezaji huyo pamoja na wakala wake ili kuona uwezekano wa kumsajili.

 

Adebayor ambaye alikuwa moto kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu baada ya kuweka kambani mabao 6 katika michezo sita aliyoichezea USGN mwenyewe pia ameonyesha kuvutiwa na mpango wa kujiunga na Simba, taarifa za karibuni zinaeleza kuwa vigogo wa Morocco, RS Berkane nao wametupa ndoano.

 

LUIS MIQUISSONE

Kwa nyakati tofauti kumekuwa na taarifa mbalimbali kutoka nchini Misri ambazo zikieleza kuwa mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Al Ahly wako kwenye mpango wa kumtoa kwa mkopo kiungo wao wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Miquissone ili nyota huyo akapate nafasi zaidi ya kucheza.

 

Na imeripotiwa kuwa tayari klabu kadhaa kutoka Mashariki ya Kati zimeonyesha nia ya kumhitaji, lakini taarifa kutoka watu wa karibu wa Luis ni kuwa mwenyewe ameshikilia msimamo wa kurejea Simba ikiwa Al Ahly watamtoa kwa mkopo. Luis msimu huu ameanza kwenye mechi nane tu na kufunga mabao matatu.

 

Baada ya Simba kufanikiwa kumrudisha Chama, bila shaka haitashangaza kumuona Luis ndani ya Bongo tena.

 

MOSES PHIRI

Nyota wa kikosi cha Zanaco ya Zambia ambaye amekuwa na wakati mzuri msimu huu, yeye anatajwa huenda akaibukia kokote miongoni mwa ‘majayanti’ wa Kariakoo, Simba na Yanga ambazo zote zimeonyesha nia ya kuhitaji huduma yake.

 

Inaelezwa kuwa tayari staa huyo amesaini mkataba wa awali wa kujiunga na Simba na anasubiri msimu huu uishe ili kujiunga nao kwenye dirisha kubwa la usajili, huku pia ikielezwa kwamba GSM nao wamefanya umafia wa kumsainisha.

 

Bila shaka dirisha kubwa la usajili litakuja na majibu sahihi juu ya ni yupi mwenye kisu kikali ambaye anakula nyama, msimu huu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Phiri ameichezea Zanaco michezo nane na kuhusika kwenye mabao manne akifunga mara tatu na kuasisti bao moja

 

IDUMBA FASIKA

Simba ipo kwenye tishio la kumpoteza mlinzi wao wa kati raia wa Kenya, Joash Onyango ambaye anamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu, huku ikidaiwa amegomea ofa ya mkataba mpya aliopewa Oktoba mwaka jana na timu mbalimbali zimeonyesha nia ya kuhitaji saini yake wakiwemo Yanga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

 

Katika kujihami na lolote ambalo linaweza kutokea Simba wameanza mchakato wa kumsajili mlinzi wa kati raia wa DR Congo anayekipiga Cape Town City ya Afrika Kusini. Idumba msimu huu amekua mhimili muhimu kwa Cape Town City akicheza michezo 18 na kufunga bao moja.

 

OUSMANE CONDE

Staa kinda wa klabu ya Milo de Kankan inayoshiliki Guinea Ligue 1 anahusishwa kujiunga na Yanga na taarifa za ziada zinaeleza kuwa tayari ameshasaini mkataba wa awali.

 

Conde ameifungia klabu yake mabao 11 kwenye mechi 13 alizocheza tangu kuanza kwa mwaka huu na kutajwa kama mchezaji bora wa mwezi Februari.

 

BIGIRIMANA ABEDI NA PITCHOU ISMAIL

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said hivi karibuni alifunga safari ya kwenda nchini Rwanda akiambatana na kocha msaidizi wa klabu hiyo, Cedric Kaze kwa ajili ya kukamilisha usajili wa viungo wawili wa Kiyovu ambao ni Bigirimana Abedi na Pitchou Ismail.

                                                                                 Stephen Aziz Ki

STEPHANIE AZIZ KI

Alikuja Tanzania na ASEC Mimosas akafunga bao moja kwenye kipigo cha mabao 3-1 walichopewa na Simba pale kwa Mkapa kwenye mchezo wa kwanza  wa kundi D Kombe la Shirikisho Afrika. Simba wakawafuata ASEC na Aziz Ki akamtungua tena Manula kule Benin wakati Simba ikiwa inakufa mabao 3-0.

Kuanzia hapo stori kubwa imekuwa ni vita ya Simba na Yanga kumnasa Mbukinabe huyo, Simba ilikuwa ya kwanza kuonyesha nia ya kumhitaji kama ingetokea wameshindwa kumpata Adebayor, lakini Yanga nao wameonyesha wanamtaka huku ikielezwa kuwa Injinia Hersi alisafiri mpaka Morocco pale ASEC walipovaana na RS Berkane ili kukamilisha mazungumzo ya awali, haitashangaza kumuona Aziz Ki Bongo msimu ujao.

Leave A Reply