The House of Favourite Newspapers

MASTAA HAWA …‘WAMEROGWA NA NANI ?’

Sanchoka

MIAKA ya nyuma kujihusisha na muziki tu hasa huu wa Bongo Fleva, ilikuwa inaonekana ni uhuni pamoja na kukiuka maadili ya Kitanzania.

Wanamuziki wakongwe, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Joseph Haule ‘Professor Jay’, Abdul Sykes ‘Dully Sykes’, Ambwene Yessaya ‘AY’, Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’ na wengine wengi walifanya kazi kubwa mpaka ikafika hatua muziki ukaonekana si uhuni tena, bali burudani pamoja na ajira.

Kukua kwa muziki ikiwa ni pamoja na kupata mapokezi mazuri kwenye jamii kutokana na juhudi za wanamuziki hao, ilikuwa ni chachu kubwa ya kukua kwa sanaa kwa jumla Bongo, iliyoibua mastaa wengine wengi.

Hata hivyo, badala ya kupokea kijiti hicho na kudumisha utamaduni wetu mastaa hao wamebadilisha hali ya hewa. Kutoka kuimba muziki ni uhuni hadi maisha ya kistaa, ikiwemo shoo, video na picha wanazoposti kuwa ni uhuni na upotoshaji wa maadili ya Kitanzania.

Baraza la Sanaa la Taifa(Basata), limekuwa na kazi kubwa ya kupambana na mastaa mbalimbali wakiwemo wanamuziki, waigizaji na hata ‘mavideo queen’, kwenye suala zima la maadili.

Ni kweli suala la kupiga picha za utupu si utamaduni wetu, ni utamaduni wa nchi za Magharibi ambao mastaa wetu wanajaribu kuukopi na kuupesti. Desemba, mwaka jana, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli akizungumza na Jumuiya ya Wazazi, alitoa kero yake juu ya wasanii kujianika utupu.

Alisema, nanukuu; “Imefika wakati wa kukemea mambo haya. Tunawafundisha nini watoto wetu? Wakati mwingine unapokuwa unatazama televisheni ukakutana na vitu hivi hasa kutoka hapa nyumbani ni aibu kubwa.

“Vyombo vyetu husika vipo wapi kukemea haya? Baraza la sanaa, vyombo vya habari, vipo wapi?” Alihoji Magufuli.

Hata hivyo juu ya suala la kukemea juu ya mastaa kujianika utupu, Basata wameinuka mara kadhaa na kuwaonya, kuwapa adhabu na kuwazungumzia mastaa wanaofanya hivyo.

Basata wamewahi kuwapa adhabu na wengine kuwaonya kama vile wanamuziki Gigy Money, Pretty Kind, Amber Lulu na mwanamitindo, Sanchoka. Lakini juu ya hili tuna mambo ya kujadili na kujiuliza;

JE, HII NDIYO KAZI PEKEE YA BASATA?

Mara nyingi ukiwasikia Basata, wakiibuka basi watakuwa wanazungumzia juu ya mastaa kujiachia nusu utupu.

Lakini ukijirusha upande mwingine unaona ni kwa sababu mastaa wamekuwa wengi, wamekuwa vichwa ngumu utadhani ‘wamerogwa’, hawataki kukubaliana na matakwa ya Basata na taifa kwa jumla juu ya kulinda maadili yetu kama Watanzania.

SASA, NANI ALIYEWAROGA?

Ukitazama baada ya mwanamuziki Pretty Kind, kufungiwa kidogo kujihusisha na muziki kulienda vizuri. Mastaa wengi wakaa nusu utupu hawakuthubutu kufanya mchezo huo.

Wengi walitupia picha na video zenye maadili na hakukuwa na shida yoyote. Lakini kwa sasa mambo yameanza kurudi. Mastaa, wanashindana kufanya matukio ya aibu na kukiuka maadili.

Tukizungumzia hao ambao wamejaribu kuwabipu Basata, siku za hivi karibuni ni Maromboso ‘Mbosso’, ambaye ametupia mitandaoni video akicheza kihasarahasara na wanawake utadhani yupo faragha.

Kuna Jux na Vee Money. Hawa huko Mwanza kwenye ziara yao ya In Love With Money, wamepigana mabusu hadharani pia utafikiri wapo wawili tu chumbani. Bila kusahau aliyoyafanya Amber Lulu, huko Mwanza, ni aibu!

Amber Lulu, alipandisha mwanaume jukwaani kisha akaanza kufanya nao ‘mapenzi ya nguonguo’, Jukwaani kiasi kwamba ili uzitazame inabidi ujifungie chumbani peke yako.

NINI KIFANYIKE?

Kikubwa wasanii watambue nafasi yao kwenye jamii na dhamana waliyo nayo. Staa ana nafasi kubwa ya kuharibu au kuboresha jamii, kwa sababu matendo yake kwa namna moja au nyingine yanafuatwa na mashabiki wao.

Kuna msemo wa Waha kutoka Kigoma unasema mkataa kwao ni mtumwa. Waache utumwa huo usio wa lazima.

Wakifuata hayo hakika hata kwa vijana wengine wanaotumia mitandao ya kijamii watajifunza kwa kuona kama mastaa hawafanyi hayo na wao ni kina nani wajihusishe nayo? Lakini pia Basata, watapungukiwa mzigo wa kufukuzana na waanika nyeti, pengine wataanza kudili na haki zao au mambo mengine yatakayowapa faida wanasanaa kwa jumla.

Boniphace Ngumije

Comments are closed.