Mastaa Hawa Wanaweza Kutoboa Bila Kujianika Nusu Utupu

Gift Stanford ‘Gigy Money’.

NAMKUBALI sana Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jay Dee’. Namkubali kutokana na muziki wake anaoufanya lakini pia namna ambavyo ametengeneza ‘status’ yake kwenye jamii, kwamba ni mwanamuziki wa heshima na huwezi kukuta ametupia picha za nusu utupu kwenye mitandao ya kijamii au video zake ili apate ‘kiki’.

 

Kwa Lady Jay Dee kiki ni muziki wake. Tofauti na wanamuziki wengi, mavideo queen na hata waigizaji ambao suala la kutupia picha za utupu kwenye mitandao ya kijamii limekuwa fasheni siku hizi. Wanafanya hivyo ili tu kuzungumziwa na kuteka ‘atensheni’ ya watu kwenye mitandao hiyo. Jambo la ajabu mpaka wanamuziki wa kiume na wanamitindo nao wamejikuta wakilivaa ‘pepo’ hili.

Pretty Kind

Swali la kujiuliza ni kwamba watu hawa hawawezi kutoboa mpaka wajianike nusu utupu? Ina maana maungo yao ya ndani ndiyo yanaeleza kile ambacho wanakifanya? Au sanaa ndiyo imebadilika, inahitaji mtu kusukuma kazi zake kwa kutumia utupu wake! Bila shaka majibu ya maswali haya yote ni ‘hapana’. Si kweli kwamba bila picha za nusu utupu wanamuziki hawa hawawezi kuzungumziwa na wala kufanya vizuri.

 

Ni suala tu la ‘paradigm shift’, yaani kubadilisha namna ya kufikiri kuhusu thamani yao, kazi wanazofanya pamoja na nguvu walizonazo kwenye jamii. Kwa mfano mwanamuziki Gift Stanford ‘Gigy Money’. Alianza kufahamika zaidi kwenye mitandao ya kijamii kwa kutupia picha za nusu utupu mitandaoni pasipo kuwa na kazi zilizosimama.

 

Nini alivuna katika picha hizo zaidi ya kufanyishwa kazi kwa malipo ya chini? Mtakumbuka mgogoro wake na Nay wa Mitego wa kushutishwa kwenye video na kupewa pesa isiyofikia hata shilingi 30,000 za Kibongo. Hiyo ilionesha nini? Thamani yake ipo chini bado pamoja na picha za utupu alizokuwa anatupia mitandaoni. Lakini kwa sasa Gigy Money baada ya kufanya kazi zinazoeleweka ukiwemo Wimbo wa Papa thamani yake ipo vipi? Jibu ni kwamba ipo juu.

Amber Lulu.

Kwa hiyo niwashauri tu hawa wanaofikiri picha za utupu zitawafanya wafanye vizuri wabadilishe mtazamo. Wanaweza kujifunza hata kwa watu wengine. Mfano mwanamitindo wa daraja A, mwenye asili ya Sudani ya Kusini, ambaye anaishi Marekani, Alek Wek, 40. Alek ni mwanamitindo ambaye kwa miaka mingi amekuwa akipamba majarida makubwa duniani yakiwemo Elle, Cosmopolitan na Glamour huku akiwa ‘inspiration’ kwa watu wengi hasa kutokana na kujikubali namna alivyo na kutumia tu kipaji chake cha mitindo kuifanya duniani kumuelewa. Alek hakuweza kutumia kitu cha ziada ili kuwaonyesha wanadamu kwamba Mungu amembariki kipaji.

 

Pengine kwa sababu ni ‘mweusii’ angeweza kujiona havutii na kuamua kutumia namna kama ambavyo wanamuziki wengi na mavideo queen wamekuwa wakifanya Bongo kwa kupiga picha za nusu utupu, lakini hakufanya hivyo na kwa sasa ni kioo kwa watu wengi. Zaidi amewafanya wanawake wengi duniani weusi kujikubali bila kujibadilisha ngozi zao wawe weupe Oprah Winfrey mwenyewe amewahi kukiri kwa kauli yake kwamba wakati akikua angebahatika kumuona Alek Wek kwenye majarida basi hata mtazamo wake jinsi alivyokuwa akijichukulia ungebadilika. Hii ndiyo kauli yake; “If (Alek) had been on the cover of a magazine when I was growing up, I would have had a different concept of who I was.

 

” Mbali na Alek kuna wanamuziki kama Anne Marie ambaye ameimba Wimbo wa Rockabaye, mbona ni mwanamuziki anayefanya vizuri duniani bila kujianika nusu utupu? Yupo Adele, Tatiana Manaois na wengine wengi, wanafanya vizuri wanaheshimika bila kujianika utupu. Kwa hiyo dada zetu kina Gigy Money, Amber Lulu, Sanchi, Pretty Kind na wengine ambao wanatumia miili yao kufosi watu waelewe wanachokifanya wana haja ya kubadili mtazamo. Kipaji ni kila kitu, kinajiuza na kinaweza kuongea zaidi ya kila kitu na watu wakawa mashabiki wako wa damu bila hata kujianika nusu utupu.

BONIPHACE NGUMIJE | RISASI JUMAMOSI


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Loading...

Toa comment