Mastaa Kumkacha Duma; ni Chuki, Wivu au Roho Mbaya?
MOJA kati ya vitu vilivyokuwa vikiwatafuna sana wasanii wa Bongo Muvi ni chuki, wivu, roho mbaya na ushirikina.
Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wasanii wameshawahi kukiri na kueleza kwamba hilo ndilo jambo linalowafanya washindwe kupiga hatua.
Inafika mahali, msanii anaweza kuwa na jambo lake lakini kutokana na roho mbaya, chuki basi tu wanaacha kumuunga mkono.
Ishu hiyo inaonekana kutokea kwa mastaa wawili, Salim Ahmed ‘Gabo’ na Daudi Michael ‘Duma’ ambao walifanya matukio mawili makubwa ya uzinduzi wa filamu zao kwa nyakati tofauti ndani ya Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.
Wakati wa uzinduzi wa muvi ya Gabo iitwayo Siyabonga uliofanyika Septemba Mosi, mwaka huu, mastaa wengi walihudhuria wakiwemo wa muziki kama vile Alikiba, Chuchu Hans, Jacqueline Wolper, Vincent Kigosi ‘Ray’ na wengine kibao.
Lakini mambo yalikuwa tofauti kwa Duma ambaye naye alifanya uzinduzi wa muvi zake mbili Septemba 28, mwaka huu; Kilio na Baba, watu waliohudhuria uzinduzi huo walikuwa wengi kulingana na ukaribu wao na Duma lakini wengi wao ni wageni katika macho ya watu wengi (sio mastaa), tofauti na kule kwa Gabo.
Baadhi ya wadau waliozungumza na mwandishi wa makala haya walisema, kinachofanyika kwa mastaa ni muendelezo wa mambo ya ubaguzi na roho mbaya kati ya msanii na msanii au wasanii fulani dhidi ya msanii fulani.
“Kwa mtazamo wangu mimi nadhani ni chuki na roho mbaya, wewe angalia watu waliokuja kwa Duma ni watu fulani hivi wa kawaida hata kimavazi lakini siku ile ya Gabo watu walikuja wale ambao ni mapedeshee, walikuja watu ambao walilipuka kwelikweli na mastaa kama wote.
“Haya mambo ndiyo yanayowafanya wasiendelee, hawana umoja na matokeo yake kila mtu anakuwa anafanya mambo yake na watu wake wa karibu basi,” alisema mdau mmoja ambaye alihudhuria matukio yote mawili.
Mdau mwingine ambaye aliongea na mwandishi wa makala haya, alisema baadhi ya wasanii ni wanafiki kwani walijifanya kumpostia matangazo Duma kwenye mitandao ya kijamii lakini siku ya tukio wakaingia mitini.
“Wanafiki sana, mtu anajifanya kukusapoti kumbe moyoni hana lolote. Wewe unafikiri hawa ambao hawajaja si kuna wengine waliposti kabisa hii event? Wako wapi sasa leo,” alisema mdau huyo.
Amani lilifanikiwa pia kumtafuta Duma ili kumsikia anazungumziaje ishu hiyo ambapo yeye hakutaka kuwazungumzia mastaa ambao hawajaja kwa sababu zao lakini zaidi akawataja wale ambao walitoa udhuru.
“Aaah ndugu mwandishi mimi ninachoweza kusema ni kuwa watu wengi niliwaalika na wapo waliotoa udhuru ni kama Uwoya aliniambia yuko kwenye ishu ya Dk Tulia Ackson, Wolper ambaye aliniambia ana safari ya Dubai hivyo asingeweza kuhudhuria, kwangu hakijaharibika kitu kwa watu waliohudhuria wanatosha sana na mimi nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwani hadi Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza aliweza kuhudhuria hivyo basi mimi nashukuru sana,” alisema Duma.
Na kwa upande wake Gabo alipopigiwa alisema yupo sehemu mbaya atumiwe ujumbe mfupi lakini licha ya kutumiwa, hakujibu!
Comments are closed.