The House of Favourite Newspapers

Mastaa: Lazima Tufunge Ndoa Mwaka Huu

0

LAZIMA tufunge ndoa mwaka huu!” Hii ni kauli ya baadhi ya mastaa nchini Tanzania wakionesha kuchoshwa na maisha ya uchumba na sasa kifuatacho ni ndoa, IJUMAA linaripoti.

Mastaa hao wameapa kuwa, inyeshe mvua au liwake jua, lazima mwaka huu wa 2022 wafunge ndoa.

WACHOSHWA NA PETE ZA UCHUMBA

Wakizungumza na Gazeti la IJUMAA kwa nyakati tofauti, baadhi ya mastaa hao ambao wamedumu na pete za uchumba kwa muda mrefu, wanadai kuchoswa na pete hizo na sasa wanahitaji kuweka heshima kwa kwa kufunga.

Baadhi yao wanadai kuwa, wamechoka kuulizwa watafunga ndoa lini hivyo jibu rahisi ni kwamba lazima wafunge mwaka huu.

Baadhi ya mastaa hao ni wale ambao tayari wamevisha na kuvishwa pete za uchumba na wengine wapo kwenye uchumba rasmi hivyo hatua inayofuata ni ndoa.

HARMONIZE NA BRIANA

Akiwa ziarani nchini Marekani, mwishoni mwa mwezi Novemba, 2021, staa wa muziki nchini, Harmonize aliingia kwenye mahaba mazito mrembo kutoka Australia aliyefahamika kwa jina moja la Briana.

Alipotua naye nchini Tanzania alimtambulisha kwa waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar na kuahidi kwamba mwaka ujao; yaani 2022 atafunga naye ndoa.

Baada ya hapo alikwenda kumtambulisha nyumbani kwao, Tandahimba mkoani Mtwara na huko inaelezwa taratibu na mipango ya kufunga ndoa ilianza na inaendelea.

Harmonize aliliambia Gazeti la IJUMAA; “Briana ndiye mwanamke wa maisha yangu!”

Briana ni mwanamke wa pili mwenye asili ya kizungu kuwa kwenye uhusiano na Harmonize baada ya kuachana Sarah Michelloti; raia wa Italia.

NANDY NA NENGA

Hivi karibuni msanii Nandy ameweka wazi kuwa, mwaka huu hautapita bila kufunga ndoa na mchumba’ke wa kitambo, rapa Billnass au Nenga.

Nenga alimvisha Nandy pete ya uchumba tangu Aprili, 2020 na kutambulishana kwenye familia zao na sasa mambo ni moto kwani wawili hao wamekuwa karibu zaidi na familia zao.

DOGO JANJA NA QUEEN LINA

Mara baada ya msanii Dogo Janja au Janjaro kuachana na aliyekuwa mkewe, Irene Uwoya ambaye ni staa wa Bongo Movies ambaye walifunga ndoa Novemba 2017, aliamua kutafuta mrembo mwingine ambaye siyo staa.

Februari, 2020, Janjaro alimvisha pete ya uchumba mrembo aitwaye Queen Lina ambaye ni mjasiriamali kutoka jijini Arusha.

Dogo Janja ameeleza kuwa, mwaka huu wa 2022 lazima afunge ndoa na mrembo huyo ambaye ni moto wa kuotea mbali.

WOLPER NA RICH MITINDO

Baada ya kujaaliwa mtoto wao wa kwanza aitwaye Paskali au P, Agosti, 2021, Jacqueline Wolper ambaye ni staa wa Bongo Movies alivishwa pete ya uchumba na mzazi mwenzake Rich Mitindo ambaye ni mfanyabiashara na mbunifu wa mavazi Bongo.

Wawili hao waliwahi kuwa pamoja kisha wakaachana na kila mmoja kuwa na maisha yake kabla ya kurudiana na sasa kifuatacho ni ndoa.

Mara baada ya kuvishwa pete hiyo ya uchumba, Wolper aliliambia Gazeti la IJUMAA; “Mwaka ujao (2022) lazima nifunge ndoa na Baba P…”

ROSA REE NA KING PETROUSSE

Septemba, 2021, rapa namba moja wa kike Bongo, Rosa Ree alivishwa pete ya uchumba na mpenzi wake wa kitambo tangu wakiwa sekondari anayetambulika kwa jina la King Petrousse ambaye alimtambulisha miezi kadhaa iliyopita mbele ya macho ya mashabiki wake.

Miongoni mwa mipango ya Rosa Ree kwa mwaka huu ni kufunga ndoa na mchumba’ke huyo.

VANESSA NA ROTIMI

Septemba 2021, aliyekuwa staa wa muziki nchini Tanzania, Vanessa Mdee au Vee Money alijaaliwa mtoto wa kiume na kumpa jina la Seven.

Lakini kabla ya hapo, Desemba, 2020, Vee Money alivishwa pete ya uchumba na mpenzi wake, Rotimi ambaye ni msanii wa filamu na muziki mwenye asili ya Nigeria aliyelowea nchini Marekani.

Wawili hao kwa sasa wanaishi wote nchini Marekani, mtindo wa maisha yao umekuwa maarufu mtandaoni na kuvutia vijana wengi.

Kwa mujibu wa Vanessa wanatazamia kufunga ndoa mwaka huu kutokana na hisia za mashabiki wao huku wengi wakitaka kujua ni lini watafunga ndoa.

POSHY QUEEN NA JOHN

Poshy Queen ni mrembo maarufu kwenye mitandao ya kijamii inayotumiwa zaidi na wabongo (sosholaiti).

Julai, 2020 alifunga safari kutoka Dar hadi nyumbani kwao jijini Mbeya na mpenzi wake na huko alivishwa pete ya uchumba na tayari wamejaaliwa mtoto mmoja.

Septemba 2021, ziliibuka tetesi za Poshy Queen kuachana na mchumba’ke huyo aitwaye John ambaye ni raia wa nchini Nigeria akiwa na maskani yake Dubai na ndiyo sababu mara nyingi hawaonekani pamoja.

hata hivyo, miongoni mwa malengo ya Poshy Queen kwa mwaka huu ni kufunga pingu za maisha na baba huyo wa mtoto wake.

STORI; WAANDISHI WETU, DAR

Leave A Reply