MASTAA NA WENYE NYUMBA WALIYOWAPANGISHA, WAPO LAWAMANI!

SERIKALI za mitaa kote nchini zimekuwa zikisisitiza wananchi wanapohamia katika makazi mapya, wao au wenye nyumba wao kwenda kutoa taarifa kwa viongozi wa mitaa kwa sababu za kiusalama lakini uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, mastaa wengi Bongo wameingia lawamani kwa kutofuata utaratibu huo.

 

Gazeti hili limebaini hilo baada ya kupita kwenye makazi ya baadhi ya mastaa ambapo ilionekana wengi wao wanapohamia kwenye nyumba za kupanga ama walizojenga, hawatoi taarifa hadi pale watakapokuwa na shida.

 

“Nyie fuatilieni mtagundua mastaa wengi hawafuati hizi taratibu za serikali za mitaa kwamba wakihamia sehemu wakatoe taarifa, hata wenye nyumba wao hawafanyi hivyo, wao wanaingia tu kimyakimya, jambo ambalo siyo sahihi linapokuja suala la taratibu za makazi.

 

“Unajua serikali ya mtaa inawakilisha serikali kuu, sasa kama taratibu zinawekwa na watu hawafuati, haiwezi kuleta picha nzuri, inaweza kuwa ni dharau au kupuuza mambo ambayo ni ya msingi sana.

“Na hili si kwa mastaa tu, wengi sana hawafuati utaratibu huu na ndiyo maana kwenye mtaa wanaweza kuhamia majambazi mjumbe hajui,” alisema mkazi mmoja wa Sinza jijini Dar, Hamza Twalibu. Kufuatia madai hayo, waandishi wetu walianza kupita kwenye nyumba za mastaa mbalimbali waishio jijini Dar na kuwaona viongozi wao wa mitaa ili kujua kama kinachoongelewa kina ukweli.

 

Nyumba ya kwanza kutembelewa ilikuwa ni ya msanii wa Bongo Fleva, Ali Salehe Kiba ‘Alikiba’ iliyopo Tabata Sanene na kufanikiwa kuongea na mwenyekiti wa mtaa aliyejitambulisha kwa jina la Mariam Machicha ambaye alisema: “Mimi huwa nashirikiana vizuri na mama yake na siyo Alikiba kwa kweli. Kila kitu kinachotokea huwa ananipigia na mimi huwa nampigia. Tunashirikiana vizuri.”

KWA IRENE UWOYA

Staa huyo anayeishi Makongo Juu, yeye na mama mwenye nyumba wake wameonekana kukiuka ule utaratibu wa kutoa taarifa baada ya kuhamia eneo hilo ambapo afisa mtendaji wa mtaa aliyejitambulisha kwa jina moja la Subira alipoongea na waandishi wetu alieleza kutokuwa na habari ya uwepo wa staa huyo katika eneo lake.

 

Baada ya kutaarifiwa  kuwa Uwoya yuko eneo hilo kwa muda mrefu kwenye nyumba ya mama aitwaye Bibi Mboto, kiongozi huyo alimpigia simu na kumuuliza uwepo wa staa huyo kwenye nyumba yake ambapo aliambiwa ni kweli yupo. Baada ya majibu hayo, kiongozi huyo alisema: ”Sijawahi kumuona na wala sijui kama anaishi huku. Hamna sheria ya moja kwa moja kuhusu mpangaji kuja kujitambulisha serikalini, mwenye nyumba ndiyo anayetakiwa kuja kutoa taarifa kuwa amepangisha mpangaji mpya.”

KWA ESHA BUHETI

Msanii wa filamu, Esha Buheti yeye anaishi Kijitonyama na gazeti hili lilipomfikia mwenyekiti wake wa mtaa aliyefahamika kwa jina la Filipo Piusi Komanya alisema hamtambui kwani mtaa wake una watu takriban elfu tano hivyo hawezi kumjua kila mtu.

 

“Katika mtaa wangu watu ni kama elfu tano kwa hiyo yeye mwenyewe angekuja kujitambulisha ndio ingekuwa sawa lakini mimi sijawahi kumuona wala kujua hiyo nyumba anayoishi, huwa namuona kwenye TV tu jambo ambalo siyo sahihi,” alisema kiongozi huyo.

KWA WEMA SEPETU

Naye mwenyekiti wa mtaa uliopo Mbezi Beach alikokuwa anaishi staa wa filamu, Wema Sepetu alisema kuwa, hakuwahi kumuona na walikuwa wakimuita kwenye ofisi ya serikali ya mtaa lakini alikuwa hafiki. “Kwa kweli hatuna uhusiano mzuri na Wema, kuna malalamiko ambayo yamekuwa yakiletwa kwetu juu ya kuishi na wanaume tata na kupiga muziki sauti ya juu usiku wa manane lakini tukipeleka barua ya wito haji,” alilalama kiongozi huyo.

KWA AUNT NA GABO

Wasanii wa filamu, Aunt Ezekiel na Salim Ahmed ‘Gabo’ wanaishi sehemu moja Mtaa wa Bwawani, Mwananyamala jijini Dar ambapo mwenyekiti wa mtaa, John Masele alisema anawatambua na amekuwa akishirikiana nao kwenye mambo mbalimbali tofauti na mastaa wengine.

 

“Huwa tunashirikiana vizuri katika shughuli zote za kiserikali, hata tukiitisha mikutano kama hawaji wao wanawatuma wawakilishi wao na hata wakitaka kufanya mambo yao ya kiserikali huwa wanakuja hapa ofisini,” alisema Masele.

Mbali na mastaa hao, kuna wengine ambao mara kadhaa wamekuwa wakilalamikiwa kwa kutoshiriki kwenye shughuli za kijamii katika maeneo wanayoishi hali inayowafanya waishi kivyaovyao.

Stori:WAANDISHI WETU, RISASI MCHANGANYIKO


Toa comment