BAADA ya kuanza rasmi kambi ya kujiandaa na mchezo wao wa kusaka tiketi ya kufuzu mashindano ya AFCON, mastaa wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wameapa kuhakikisha wanapambana kufa na kupona kuitoa Uganda na kufuzu kushiriki mashindano hayo.
Stars kwa sasa wapo jijini Ismailia nchini Misri wakijiandaa na michezo miwili ya kusaka tiketi ya kufuzu mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika ‘AFCON’ 2023 ambayo yanatarajiwa kufanyika nchini Ivory Coast.
Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo unatarajiwa kupigwa keshokutwa Ijumaa ya Machi 24, mwaka huu kabla ya mchezo wa marudiano ambao unatarajiwa kupigwa Machi 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatano, kipa wa timu hiyo, Aishi Manula alisema: “Tumefika katika mazingira mazuri na kila mchezaji anaonyesha kuwa na ari ya kuutaka mchezo huu, Uganda ni timu ngumu hivyo ni wazi hautakuwa mchezo rahisi lakini tunataka kuhakikisha tunafanikisha hilo.
“Tulikuwa tunasubiri sehemu ya wenzetu ambao bado walikuwa hawajawasili kutokana na majukumu ya timu zao naamini wote kwa pamoja tukikamilika tutakuwa na tayari kuzungumza kiufundi.”