Mastaa wa ‘Huba’ Wanogesha Maadhimisho ya Miaka 40 ya SGA

SGA, kampuni ya ulinzi binafsi inayoongoza nchini Tanzania, imeadhimisha miaka 40 ya huduma kwa kuandaa mashindano ya kuvutia ya soka yaliyowashirikisha waigizaji maarufu wa ‘Huba Series’.
Mashindano hayo ya kusisimua yalifanyika Jumatatu ‘Masaki Sports Park’ na kuzikutanisha timu 24 zilizochuana vikali, huku watazamaji wakishangilia kwa nguvu na kufanya ‘Masaki Sports Park’ kuwa kivutio. Waigizaji watano maarufu wa ‘Huba Series’, akiwemo Rammy Galis (a.k.a Dev), Ibrahim Omary (a.k.a Fabrizo), Tito Zimbwe (a.k.a Roy), Ben Kinyaiya (a.k.a Judi) na Haji Salum (a.k.a Chidi) walishiriki mashindano hayo chini ya timu yao, Klabu ya Soka ya ‘Huba Series’ na pia walijumuika pamoja na washiriki.

Timu ya Maendeleo Bank iliibuka na ushindi wa jumla baada ya kuicharaza Akiba Commercial Bank katika fainali ya kusisimua iliyomalizika 3-1 Kwa mkwaju wa matuta huku wakikabidhiwa kombe la mshindi.
Timu nyingine zilizoshiriki katika mashindano hayo ya kutwa nzima yayoambatana na muziki wa kusisimua kutoka kwa DJ, ni pamoja na Kampuni ya SGA, Dar es Salaam Inter Club, Ramada Resort Hotel, Benki ya Equity, Hospitali ya Kimataifa Sali, Benki ya KCB, Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala, Team Uganda, Mowara, Benki ya Afrika, Benki ya Exim, Benki ya Selcom, Inter Tek, Impala Terminals, Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc), Benki ya Absa, Benki ya NBC, Puma Energy, Shule ya Tusiime na Chuo Cha Hospitali ya Kairuki.
Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni Warda Abdallah Obathany aliipongeza Kampuni ya SGA kwa mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 40 ya utumishi wake nchini Tanzania hususani kuajiri wafanyakazi zaidi ya 5000 nchini Tanzania. Alisema hii ni hatua kubwa mno na kutoa wito Kwa wawekezaji wengine wawekeze kama SGA ili watengeneze nafasi nyingi za ajira Kwa watanzania.
“Kama Serikali tunawapongeza kwa mafanikio mliyofikia hadi sasa na tunatoa wito kwa makampuni mengine kuiga mliyofanya leo kwa kukaribisha taasisi nyingine kuungana nanyi katika kutimiza miaka 40 kupitia mashindano haya ya soka, ambayo pia yanaimarisha mwili na afya njema miongoni mwa wafanyakazi,” alisema.
Alitoa wito kwa Kampuni ya SGA kuhakikisha tukio hilo linafanyika kila mwaka ili kuzileta pamoja taasisi nyingi zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa SGA Tanzania Eric Sambu aliwashukuru wateja wote wa SGA kwa msaada wao na kuwawezesha kutimiza miaka 40 ya huduma kwa mafanikio.
“Tunafurahi kuadhimisha miaka 40 kwa kuzileta pamoja timu 23 katika mashindano haya ya soka ya kampuni ambayo yamekuwa ya kusisimua na yenye ushindani mkubwa. Tunawashukuru wafanyakazi wa ‘Huba Series’ kwa kukubali kuwa sehemu ya mashindano haya,” alisema.
Aidha, alibainisha kwamba mashindano hayo yamesaidia wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali kujiweka sawa na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yamekuwa tishio kubwa katika sehemu za kazi.
Mwakilishi wa Huba Series Rammy Galis (a.k.a Dev) aliipongeza Kampuni ya SGA kwa kutimiza miaka 40 na kuandaa mashindano hayo, ambayo yaliwaleta karibu na mashabiki wao kwani hawakucheza mpira tu, bali pia walishirikiana nao.
Kampuni ya SGA hutoa huduma za ulinzi binafsi, huduma ya mwitikio wa onyo la hatari, huduma za fedha taslimu, ufumbuzi wa masuala ya usalama kwa njia za kielektroniki, huduma ya usafirishaji wa barua na huduma nyinginezo. SGA ni kampuni pekee iliyothibitishwa na ISO18788 (Mfumo wa Usimamizi wa Uendeshaji wa Ulinzi Binafsi) ndani ya nchi. Ina pia vyeti vingine vitatu vya ISO – ISO 9001 (Ubora), ISO 14001 (Usimamizi wa Mazingira) na ISO 45001 (Afya na Usalama Kazini)