Mastaa wa Kike Wafungukia Mastaa wa Kiume Kuoa Nje!

DAR ES SALAAM: Kufuatia upepo wa mastaa wa kiume Bongo, kuwa na uhusiano na hata kuoa warembo kutoka nje ya Bongo, baadhi ya mastaa wa kike nchini, wamefungukia suala hilo na kueleza maoni yao.

 

Hivi karibuni, mastaa wa kiume wameonekana ‘kuwafia’ warembo kutoka nje, akiwemo Ali Saleh Kiba ‘AliKiba’ aliyeoa mrembo Amina Khalef kutoka Kenya, Abwene Yesaya ‘AY’ (Rehema Soud Suleiman, Rwanda) na Boniventure Kabobo ‘Staminaliyemchumbia Veronica, raia wa Rwanda.

 

Kufuatia upepo huo, watu walikuwa na mitazamo tofauti mitandaoni. Kuna ambao walisema mapenzi hayaangalii nchi lakini wengine walidai kuwa kitendo cha mastaa hao kufanya hivyo ni kama kuwadharau wanawake wa Kibongo.

Kutokana na mvutano huo, Amani lilizungumza na baadhi ya mastaa; Wema Sepetu, Halima Yahaya ‘Davina’, Shamsa Ford na Aunt Ezekiel ambapo kila mmoja alikuwa na mtazamo tofauti kuhusu suala hilo.

WEMA SEPETU

“Mimi kwa kweli naona ndoa hupangwa na Mungu, hivyo kama imepangwa utaoa nchi nyingine utafanya hivyo na ukiangalia mke mwema haijalishi mpaka utoke naye nchi moja, inategemea huyo mtu amejuanaje na mkewe huyo hivyo sioni kama kuna shida.”

AUNT EZEKIEL

“Kwa upande wangu mimi sioni shida kabisa wala sidhani kama kuna mwanamke atalalamika hapa kwetu hajaolewa yeye maana mke anatakiwa mmoja tu na muoaji anachagua aoe wapi hata kama angeenda Marekani, lakini kikubwa wawe wanapendana.”

DAVINA

“Kwanza watambue kuwa wale wanamuziki wanatembea sehemu mbalimbali za dunia hivyo ni rahisi kupata huko nje kwa sababu hata mimi sijui kama nitaolewa na Mbongo na mapenzi ni majani huota popote tu.”

SHAMSA FORD

“Mimi sioni kama kuna jambo baya jamani kwa sababu mapenzi hayachagui wapi pa kuota hivyo hata wao waliona ua lao la kuweka ndani siyo la kuchuma hapa nchini naona sawa kabisa kwa sababu kila mtu anaangalia vigezo vya mke anayetaka kumuoa.”

Ukiachana na Stamina, AY, na Kiba ambao watu wao ni raia wa kigeni, staa mwingine aliyetopea kwenye uhusiano na raia wa kigeni ni Nasibu Abdul ‘Diamond’ ambaye amezaa watoto wawili na Mganda, Zarina Hassan ‘Zari The Boss Lady’ na kisha kuachana.


Loading...

Toa comment