The House of Favourite Newspapers

Mastaa ‘Wagumba’ Waliopata Watoto

0

Makala: Andrew Carlos

Julai 25, 1978 inabaki kuwa katika vitabu vya kihistoria katika Mji wa Oldham, Uingereza baada ya mwanamama aliyeteseka na ugumba kwa muda mrefu, Lesley kuishtua dunia kwa kujifungua mtoto aliyeitwa, Louise Joy Brown.
Louise alizaliwa kwa njia ya upandikizaji kiinitete ambao kitaalam unajulikana kama In Vitro Fertilization (IVF) na kuwa binadamu wa kwanza kuzaliwa kwa kutumia njia hiyo ambayo hutumika kutibu ugumba kutokana na matatizo kwa mwanaume au mwanamke kama manii kuwa kidogo au kuziba mirija ya kupitisha mayai.
Katika njia hii, mayai ya kike hukusanywa kwa mwanamke, hupewa dawa za kusaidia kuyatoa kwa kifaa maalum kutoka kwenye ovari na kuchanganywa na manii kwenye kidishi maalum cha maabara na kurutubishwa, huachwa yakue kidogo kwa siku mbili hadi tatu kuwa kiinitete ambacho huchukuliwa kisha kupandikizwa kwenye mji wa uzazi wa mwanamke na kutengeneza ujauzito.
Wapo mastaa wengi wa muziki, mitindo na filamu ambao wamesumbuliwa kwa muda mrefu na tatizo hili la ugumba lakini baada ya kutumia njia hii ya IVF, wamebahatika kupata watoto na katika makala haya yanawachambua mastaa hao;

Tyra Banks
Mwanamitindo huyu kutoka Marekani ni miongoni mwa mastaa waliokabiliwa na tatizo la ugumba kwa muda mrefu.
Januari, mwaka huu, Tyra akiwa na mchumba wake, Erik Asla kwa mara ya kwanza kwa kutumia njia ya IVF, walifanikiwa kupata mtoto, York Asla.

Celine Dion
Mkongwe huyu wa Muziki wa Pop asiyechuja naye ni miongoni mwa mastaa walioteseka kwa muda mrefu na ugumba.
Akiwa na mumewe, Rene Angélil (sasa marehemu), Celine alihangaika kutumia njia hii ya IVF kwa zaidi ya mara sita bila mafanikio hadi pale alipojaribu tena mwaka 2000 na kufanikiwa kupata mtoto, René Charles. Mwaka 2010, alijaribu tena kutumia njia hii na kufanikiwa kupata watoto mapacha, Eddy na Nelson.

Mariah Carey
Staa huyu mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni, kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la ugumba. Akiwa na mchumba wake wa zamani, Nick Cannon walishajaribu mara kadhaa kutafuta mtoto bila mafanikio.
Mwaka 2011, aliamua kutumia njia ya IVF kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kupata watoto mapacha, Moroccan na Monroe.

Nicole Kidman
Nicole anayebamba katika filamu kibao kama vile The Hours na Eyes Wide Shut na nyingine nyingi, kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kutokupata mtoto.
Mwaka 2008 akiwa na mchumba wake wa sasa, Keith Urban, alifanikiwa kupata mtoto wa kwanza, Sunday Rose kwa njia ya IVF. Alijaribu tena njia hiyo mwaka 2010 na kufanikiwa kupata mtoto wa pili, Faith Margaret.

Emma Thompson
Emma ni mmoja wa mastaa wa filamu kutoka Uingereza ambaye aliwahi kubamba na Filamu ya Love Actually na Nanny McPhee. Staa huyu ni miongoni mwa walioteseka kwa muda mrefu na ugumba.
Akiwa na mumewe, Greg Wise, Emma alihangaika kwa muda mrefu kutafuta mtoto wa njia ya IVF ambapo mwaka 1999 alifanikiwa kupata mtoto wake wa kwanza na wa pekee, aliyemuita Gaia.

Leave A Reply