The House of Favourite Newspapers

MASTAA WAPINGA WEMA KUPEWA TUZO!

DAR ES SALAAM: BAADA ya wiki iliyopita staa wa filamu za Kibongo, Wema Sepetu kushinda tuzo mbili katika hafla ya Tuzo za Sinema Zetu zilizofanyika ndani ya Ukumbi wa Mlimani City, mambo yamekuwa mambo kutokana na baadhi ya wadau pamoja na mastaa wenzake kupinga ushindi wake huo.

 

Mara baada ya Wema kukabidhiwa Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike na ile ya Msanii Bora Chaguo la Watazamaji hapo ndipo minong’ono ilianza ambapo iliendelea pia katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwamba mrembo huyo hakustahili kwani wapo wasanii wengi wa kike ambao wanajua kuigiza kuliko mwanadada huyo.

 

“Kiukweli Wema hakustahili kupata hiyo tuzo maana wasanii kama Riyama Ally ndiyo wanastahili maana wanajua kuigiza jamani lakini nashangaa amepewa yeye inawezekana watu wanavutiwa tu na umaarufu wake na siyo kazi yake maana hata filamu zenyewe anacheza mara chache sana siyo kama wengine,” alisema mmoja wa mastaa ambaye hakutaka jina lake lichorwe gazetini.

 

Akizungumza na Amani, msanii wa filamu Kulwa Kikumba ‘Dude’ alisema Wema amepata ushindi kwasababu kura alikuwa akipigiwa na mashabiki ambao wengi hupiga kutokana na jinsi wanavyomuona au kumsikia mtu kwa muonekano wa nje lakini hawaangalii kazi zao husika.

 

“Mpoki aliwahi kuibuka mwimbaji bora wa nyimbo za asili Kili Music Award akawashinda manguli wa muziki huo kama Wanne Star na Mrisho Mpoto, hiyo ndiyo faida ya kura za mashabiki, sasa hapo ndipo kwenye tatizo. Sikatai Wema kushinda lakini tatizo linakuja, waandaaji wa tuzo wa nje, wanaweza kumsikia Wema ameshinda nchini, wakimpeleka kule, atafeli maana ni ukweli ulio wazi kwamba Wema hawezi kuwazidi waigizaji wengine kama Riyama,” alisema Dude.

 

Kwa upande wake Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ yeye alihoji mastaa wengine kama JB, Rich, Aunt Ezekiel, Shamsa Ford, Duma, Ray na wengine wengi walikuwa wapi hawakuonekana kwenye tuzo hizo.

“Nitaongea nilichokiona jana kwenye tuzo ,kwani Ray, JB, Rich, Aunt Ezekiel, Shamsa Fodi, Duma, Weru, Hemedi, Tausi Mndengela, Mainda, Johari, Uwoya, Marian Ismail, Batuli na wengine wanaofanya vizuri wapo wapi?” alihoji Steve kuonesha hakubaliani na ushindi wa Wema.

 

UWOYA, BATULI WARUSHA VIJEMBE

Hata hivyo wapo mastaa wengi walioonekana kupinga tuzo hiyo kutokana na kuandika vijembe kwenye kurasa zao za Instagram akiwemo Irene Uwoya ambaye alisema ‘maumivu yakizidi muone daktari’ pia Yobnesh Yusuph ‘Batuli’ naye aliandika ‘mvuvi haogopi mawimbi ya bahari’ ambapo mashabiki waliwashambulia kwa maneno makali yasiyoandikika gazetini.

 

ESHA AMTETEA

“Jamani tuwekane sawa mbona kama tunagombana? Ipo hivi.. hawa watu waloandaa tuzo walianza kupiga kelele mwaka jana mwezi wa kumi kama sikosei na waliitisha mkutano wakaomba jamani leteni muvi zenu kuna tuzo zinakuja, tatizo ni kwamba wengi wenu muvi mlimuuzia Steps na walichokuwa wanaeleza washindani watapatikana kutokana na muvi zilizopokelewa hapohapo na siyo washindani kutoka nje ya hapo” aliandika Esha katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Amani lilimtafuta Zamaradi ambaye ndiye msemaji wa Azam Media kuhusu malalamiko ya tuzo hizo ambapo simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.

 

Lakini pia lilijaribu kumtafuta msaidizi wake ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa siyo msemaji yeye alisema kwanza waliangalia hakimiliki kwa hiyo filamu ambazo hakimiliki siyo za msanii walikuwa hawazichukui, pili mchakato ulichukua miezi sita na walitoa miezi mitatu wasanii kupeleka kazi zao lakini wengi walipuuzia na Wema ndiye aliyepeleka.

Stori: Mwandishi Wetu, Amani

Comments are closed.