The House of Favourite Newspapers

Mastaa wawili wanaowindwa na Yanga…

0

 SIMBA-YANGA-12.jpg

Wilbert Molandi,Dar es Salaam

KIUNGO mshambuliaji, Farid Mussa na kiungo mkabaji, Mudathiri Yahya wanaoichezea Azam FC, wametibua dili la kutua Yanga.

Nyota hao ni kati ya wachezaji waliokuwa wakiwaniwa vikali na Yanga tangu kwenye usajili wa dirisha dogo la usajili msimu uliopita akiwemo Pascal Wawa na Kipre Tchetche ambao Azam iliwakatalia, licha ya uongozi wa timu hiyo kuwasilisha barua ya kuwaomba.

Viungo hao, hivi karibuni wamekuwa tegemeo kuanzia kwenye klabu yao ya Azam na timu ya taifa inayofundishwa na mzawa, Charles Mkwasa na msaidizi wake, Hemed Morocco.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, viungo hao wanatarajiwa kuelekea Sweden wakati wowote mara baada ya kumaliza majukumu ya Stars iliyokwenda kurudiana na Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia, iliyopigwa usiku wa kuamkia leo.

Chanzo hicho kilisema, wachezaji hao wanakwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini humo.

Kiliongeza kuwa, kuna makubaliano ambayo ni ya siri sana, lakini vijana hao timu ya kwanza watakayoichezea watacheza bure, huku wakisubiri kusajiliwa na timu nyingine ambapo Azam itapata asilimia hamsini ya mauzo yao.

“Mazungumzo yetu na hiyo klabu inayowahitaji yamekwenda vizuri kabisa na hivi sasa tupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha mpango huo wa kwenda Sweden.

“Makubaliano tuliyokubaliana nayo ni kuwa, watakwenda kwenye klabu hiyo bure, lakini tumeweka baadhi ya makubaliano maalum katika mikataba yao.

“Na kikubwa tumekubaliana kuwa; watakwenda huko bure, lakini kama ikitokea klabu ikawataka basi katika sehemu ya mauzo yao, Azam tutapata asilimia 50, ikitokea wakauzwa tena Azam tutapata asilimia 30 na huko alipokwenda kama timu nyingine ikivutiwa nao, basi katika sehemu ya mauzo yao tutapata asilimia 20 ya fedha zao za usajili kwa kila mchezaji,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa mtendaji mkuu wa timu hiyo, Saad Kawemba, kuzungumzia hilo, simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa lakini ofisa habari wa timu hiyo, Jafar Idd alipopatikana, alishtuka na kuuliza: “Hizo taarifa umezitoa wapi? Bado hakuna taarifa hiyo, ikitokea mtataarifiwa.”

 

Leave A Reply