Mastaa Yanga Wawekwa Kitimoto

KABLA ya kuanza safari ya kuelekea Mkoani Mbeya, uongozi na benchi la ufundi la Yanga lilifanya kikao kizito na wachezaji wake kambini kwao Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Yanga inayongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 16, jana saa kumi na mbili asubuhi ilisafiri kuelekea Mbeya kwa ajili ya mchezo wa ligi dhidi ya Mbeya Kwanza utakaopigwa Sokoine mkoani huko.

Mara baada ya mchezo huo, Yanga itacheza mchezo wake wa ligi dhidi ya Simba utakaochezwa Desemba 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Mmoja wa mabosi wa timu hiyo, ameliambia Championi Jumatatu kuwa katika kikao hicho, viongozi na benchi la ufundi chini ya Nasreddine Nabi na Cedric Kaze liliwasisitiza wachezaji wake kucheza kwa nidhamu kubwa mchezo wao dhidi ya Mbeya Kwanza.

Bosi huyo alisema kuwa lengo la kucheza kwa nidhamu ni kuepuka adhabu za kadi nyekundu na njano ambazo huenda zikawasababishia kuukosa mchezo ujao dhidi ya Simba.

Aliongeza kuwa pia wachezaji wameonywa kutoongea au kujibizana na waamuzi wa mchezo huo kwa hofu ya kupata adhabu hizo za kadi.

“Kariakoo Dabi ina mambo mengi ya ndani na nje ya uwanja, hivyo ni lazima uongozi na benchi la ufundi liwe na tahadhari katika kuelekea mchezo huo ambao muhimu kwetu.

“Kikubwa tunataka kupata pointi tatu zitakazotufanya tuendelee kukaa kileleni, tuweke historia pamoja na kuwafurahisha mashabiki wetu kwa ushindi na sojka safi la kuvutia.

“Hivyo ili tutimize vyote hivyo katika dabi, basi ni lazima wachezaji wote muhimu wawepo katika dabi ambao ni Aucho (Khalid), Bangala (Yannick), Diarra (Djigui), Mayele (Fiston), Djuma (Shaban), Moloko (Jesus) na wengine wote,”alisema bosi huyo.

Akizungumzia hilo Ofisa Habari wa timu hiyo, Hassani Bumbuli alisema kuwa “Ni lazima tuwe makini katika mchezo wetu dhidi ya Mbeya Kwanza kwa hofu ya kuwakosa wachezaji wetu muhimu katika dabi.

“Tunataka wachezaji wote wawepo katika dabi, hivyo tumewataka wachezaji wetu kucheza kwa tahadhari ya kupata majeraha na kadi, tutaingia uwanjani katika mchezo wetu dhidi ya Mbeya Kwanza kwa ajili ya kupata ushindi pekee kabla ya kukutana dhidi ya Simba.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam702
SWALI LA LEO

Kupanda Kwa Bei ya Mafuta Nchini, Nini Kifanyike Kupunguza Bei?
Toa comment