The House of Favourite Newspapers

Mastraika wanne wafeli mtihani wa kwanza Simba

 

STORI: Omary Mdose, Arusha | CHAMPIONI

KATIKA hali iliyowashangaza wengi, mastraika wanne wa Simba, juzi Jumamosi wote walifeli mtihani wa kwanza wa kocha wao mkuu, Joseph Omog. Mastraika hao ambao ni Ibrahim Ajibu, Laudit Mavugo, Juma Liuzio na Pastory Athanas, walifeli mtihani huo pale walipopewa zoezi la kupiga penalti walipokuwa mazoezini.

Championi lilikuwepo katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa TGT jijiji Arusha, ambapo Omog aliwataka wachezaji wake wote wapige penalti kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa jana Jumapili wa Kombe la FA dhidi ya Madini FC.
Kati ya wachezaji 20 waliopiga penalti hizo, watano pekee ndiyo waliokosa wakiwemo mastraika hao na beki wa kulia, Janvier Besala Bokungu. Baada ya kushindwa mtihani huo wa kwanza, Omog aliwataka kurudia tena kupiga penalti mbili kwa kila mmoja na atakayekosa moja angezunguka uwanja kwa dakika tano na atakayekosa zote angezunguka mara mbili yake.
Walipopewa nafasi hiyo ya kurudia, Liuzio, Ajibu na Bokungu walipata zote huku Pastory akikosa moja na Mavugo akikosa zote. Hata hivyo Omog aliwasamehe kuwapa adhabu aliyoitangaza awali. Omog akaliambia Championi Jumatatu:

“Zoezi hili ni muhimu sana kwa sababu tupo kwenye michuano ambayo kama dakika tisini zikiisha kwa sare, basi mshindi atapatikana kwa mikwaju ya penalti, lakini pia hata katika ligi huwa inatokea tunapata penalti kwa hiyo sitakuwa tayari kuona tunakosa hasa kipindi hiki cha kuelekea kuchukua ubingwa.”

Comments are closed.