The House of Favourite Newspapers

Maswali 8 kuuawa Mwenyekiti wa Chadema Geita

0

mawazo (2)Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo enzi za uhai wake.

Dola isiache raia wauawe kirahisi katika mazingira tata namna hii!

TUKIACHA wananchi wauawe kila siku katika mazingira tata; tunavunja katiba inayotoa haki ya binadamu kuishi. Tunawapa kibari wauaji kutoa roho za wanyonge na  mwisho wa haya ni taifa kuanguka.

Ni karibuni tu Mchungaji Christopher Mtikila amepoteza maisha katika mazingira tata, ndugu jamaa na marafiki wamemuombolezea wajuavyo; machozi yao yamepokewa ardhini na inavyoonekana haki itapatikana kwa Mungu.

mawazo (1)Akiwa hospitali baada ya kuvamiwa na kupigwa.

Wakati mambo hayajapoa Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo naye ameuawa kinyama na watu waliopewa jina la ufuasi wa chama cha siasa. Simanzi nzito imetanda tena huku mgombea ubunge wa chama hicho Mkoa wa Arusha Godbless Lema, akikoleza maomboleo hayo kwa kusema: “Mungu tuoneshe tufanye nini?”

Kama ilivyokuwa kwa Mtikila, gazeti hili liliibua bila hofu mazingira tata ya kifo chake. Kwetu kama chombo cha habari ulikuwa ni wajibu mzito wenye vitisho lakini tulitaka kuuonesha umma kuwa tunapigania haki za watu bila hofu.

Kwa msingi huohuo nautwaa ujasiri wa kuhoji mauaji ya Mawazo kwa sababu yamejaa makengeza kutoka kwa watu waliokuwa naye, waliomuua na vyombo vyetu vya usalama kuwa wote hawakumtetea asiuawe.

Kwa nini hawakufanya hivyo? Majibu ni mawili wanahusika au walizembea. Pengine nitaulizwa tena; kwa nini? Ni kwa sababu mazingira na maelezo ya pande zinazohusika hayakidhi hesabu ya mtu kuuawa kirahisi mchana kweupe namna ile!

Pamoja na maelezo marefu yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari na mashuhuda juu ya tukio la mauaji ya mwenyekiti huyo wa Chadema bado kuna maswali yanayokosa majibu. Na hii ni kazi ya dola kutafuta majibu siyo mimi.

Mawazo hakuwa jambazi auawe mbele ya watu saa 5, asubuhi katika eneo lenye watu na asipate kusaidiwa. Mawazo siyo mzigo achukuliwe kirahisi na kupelekwa umbali wa nusu kilometa bila kujitetea hata kwa kupiga kelele.

Katika maelezo yake Katibu wa Chadema, Mkoa wa Geita, Rogers Luheja alinukuriwa na vyombo vya habari akisema kuwa baada ya mkutano wao wa ndani wa chama kuvamiwa na wafuasi aliowataja kuwa ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwenyekiti wao alipanda pikipiki kuelekea kusikofahamika.

Najiuliza, washiriki wa kikao cha Chadema wanakiri kuvamiwa, iweje mwenyekiti wao aondoke bila wao kujua aendako. Walichukua hatua zipi kuhakikisha kuwa atakuwa salama huko aendeko ilhali wanajua hali ilishakuwa tete?

Baada ya kuondoka waliokuwa kwenye kikao waliendelea kufanya nini? Maana inaelezwa kutoka saa 5 asubuhi alipojeruhiwa, Mawazo amefikishwa Hospitali ya Wilaya ya Geita saa 9 Alasiri na kwa maelezo ya Mganga Mfawidhi, Adamu Sijaona, mgonjwa alikuwa amecheleweshwa sana.

Kwa maelezo haya Mawazo alitetea maisha yake kwa zaidi ya saa 4 bila msaada. Kama hilo halitoshi inaelezwa mahali walipofanyia mkutano Chadema katika Ukumbi wa Makungu uliopo Mtaa wa CCM, mjini Katoro ni sehemu yenye mkusanyiko wa watu na isitoshe siyo mbali sana na kituo cha polisi.

Kwa hesabu zinazotengenezwa kwamba marehemu Mawazo alikutwa eneo la Njia Panda ya Katoro na Inyala, nusu kilometa kutoka eneo la mkutano. Bado hesabu hazisomi kama umbali huo unaweza kuwa sawa na mazingira ya picha za majeruhi zilizosambazwa mitandaoni wakati akiugulia maumivu.

Hata kama hesabu hizo zitalazimishwa waliomuona kwa nini wasimrejeshe Kituo cha Afya Katoro ili afungwe majeraha kabla ya kumpeleka wilayani ambako umbali wake ni kilomita 45, sawa na nusu saa kwa usafiri wa gari? Kingine mpiga picha za tukio hilo alilenga nini kuzisambaza?

Utata mwingine unaibuliwa na mashuhuda wanapodai kuwa Polisi wa Kituo cha Katoro walipewa taarifa za vurugu na kushambuliwa kwa Mawazo lakini hawakufika. Kilichowazuia hakifahamiki!

Nihitimishe makala haya kwa kuvitaka vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa vinawapa raia haki yao ya kikatiba ya kuishi, vikishindwa kufanya hivyo kwa kupuuza wanaouawa pengine kwa mtazamo wao, amani ya nchi haitadumu.

Leave A Reply