Matatani kwa kumpa kichapo Mbunge wa CCM
NA Mayasa Mariwata, UWAZI
DAR ES SALAAM: Kimenuka! Mlinzi wa Kituo cha Mafuta cha Big Bon (wengine huita sheli) kilichopo Sinza-Mori, Dar yu matatani akidaiwa kumpa kichapo Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini (CCM), Prosper Mbena, Uwazi limeinasa.
Mlinzi huyo aliyetajwa kwa jina la Mack Yusuf, anadaiwa kutenda msala huo, Alhamisi iliyopita kwa kisa cha kuegesha gari eneo lisiloruhusiwa na uongozi wa kituo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, siku ya tukio, saa 3 usiku, mbunge huyo alifika kituoni hapo na kuegesha gari kwenye eneo la ‘supermarket’ iliyopo mahali hapo, ndipo mtiti ukatokea.
“Baada ya kuegesha gari supermarket, mbunge alitoka nje na kuongea na mtu ambaye alifika hapo naye akiwa na gari. Yeye alikuwa akiongea na huyo mtu akiwa nje. Ghafla, nikamwona mlinzi anamshushia kichapo mheshimiwa kisha akampora simu.
“Hata hivyo, mbunge alijifanya mpole, akambembeleza na kurudishiwa simu yake,” alisema shuhuda mmoja.
Uwazi lilimtafuta mbunge huyo kwa njia ya simu ya mkononi ambapo alikiri kutokea kwa timbwili hilo na kusema kitendo alichofanyiwa na mlinzi huyo hakikumstahili kwa sababu aliegesha gari nje ya supermarket hiyo ili afanye manunuzi.
“Nilijaza mafuta pale kituoni kisha nikapaki gari mbele na kuingia supermarket. Nikiwa ndani, kabla sijamaliza manunuzi, nikapigiwa simu na jamaa aliyekuwa anapita eneo lile, nikatoka nje. Ndipo mlinzi akaja na kuniambia nitoe gari nilipopaki siyo mahali sahihi.
“Nilimweleza nipo supermarket na aliniona tangu naingia, ndiyo akanirushia ngumi ya uso na mkononi japokuwa sikupata jereha huku akinitupia matusi mazito. Ilibidi niende polisi,” aliongeza.
Kutokana na sekeseke hilo, mtuhumiwa mpaka juzi Jumapili, alikuwa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’, Dar kwa jalada la kesi namba KJN/RB/13045/15 SHAMBULIO.