The House of Favourite Newspapers

Matatizo Katika Uzalishaji wa Mbegu za Kiume

0

Na DK. CHALE | IJUMAA | AFYA

TATIZO hili kitaalamu huitwa Sperm Disorders na kiasi kikubwa husababisha ugumba kwa mwanaume. Matatizo haya ya uzalishaji wa mbegu za kiume huathiri ubora na kiwango cha mbegu zinazotoka. Uchunguzi wa kuhakikisha kwamba mwanaume ana tatizo hili ni kupima mbegu kutoka katika manii na vinasaba.

JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA

Kwa kawaida katika maisha ya mwanaume, mbegu za kiume huzalishwa kila siku na kila mbegu baada tu ya kuzalishwa huchukua siku 72 na 74 hadi ziwe zimekomaa na kuwa na ubora unaofaa kurutubisha yai la mwanamke. Mbegu huzalishwa katika nyuzi joto thelathini na nne ndani ya kiwanda ambacho ni korodani katika sehemu iitwayo Seminiferous Tubules.

Chembe hai za sertoli zinazopatikana humo ndizo hufanya kazi ya kuzikomaza. Chembe hai ya Ley Dig ambayo pia imo katika korodani ina kazi kubwa ya kuzalisha vichocheo vya kiume viitwavyo Testosterone. Katika korodani kuna sehemu ya vifuko vya kuhifadhia na kuzalisha sukari ya Fructose viitwavyo Seminal Vesicles. Sukari hii ndicho chakula kikuu cha mbegu za kiume zikiwa bado hazijatoka. Mbegu za kiume huhifadhiwa katika Seminal Vesicles na wakati wa kutoka hutoka katika mirija maalumu iitwayo Ejaculatory Ducts.

 

Kasoro katika uzalishaji wa mbegu kama tulivyoona huathiri kiwango yaani zinatoka chache sana ambapo kitaalamu huitwa Oligospermia na athari katika ubora wa mbegu ni kama vile kasoro za maumbile ya mbegu na mbegu zinatoka lakini hazitembei.

CHANZO CHA TATIZO

Vyanzo vya tatizo hili tunaweza kuvigawa katika makundi makubwa mawili: Kwanza ni matatizo katika uzalishaji wa
mbegu za kiume kitaalamu tunaita Impaired Spermatogenesis. Hapa vinavyosababisha ni uwepo wa joto kali katika korodani, kasoro katika viungo vya uzazi vya mwanaume mfano kutokuwa na korodani au kuwa na korodani moja, matatizo katika vinasaba, matumizi ya baadhi ya madawa mfano dawa za kulevya, kemikali za mashambani. Vilevile baadhi ya dawa za hospitali zinaweza kuchangia.

Tatizo lingine linahusiana na kutotoa mbegu au kitaalamu linaitwa Impaired Sperm Emission, hapa mwanaume hatoi kabisa mbegu au zinatoka kidogo sana. Utoaji huu ni pamoja na kutotoa manii. Wakati mwingine zinaweza kutoka lakini hazielekei nje zinaishia kwenye kibofu cha mkojo.

Hali hii kitaalamu inaitwa Retrograde Ejaculation na inaweza kusababishwa na ugonjwa wa kisukari, matatizo ya mishipa ya fahamu hasa katika uti wa mgongo, upasuaji wa tumbo kuondoa tezi za ugonjwa wa Hodgkin’s Lymphoma na upasuaji wa kuondoa tezi dume.

Hapo tumeona tatizo la mbegu na manii kutotoka kabisa, lakini inawezekana mwanaume akatoa manii tu bila mbegu za kiume. Hii husababishwa na kuziba kwa njia za kutolea mbegu, kasoro za kutokuwepo kwa njia hizo yaani tatizo la kuzaliwa nalo na kutokuwa na vifuko vya kuhifadhia mbegu au Seminal Vesicles.

UCHUNGUZI

Upimaji wa manii kuangalia kiwango na ubora wa mbegu, vipimo vingine ni vile ambavyo daktari ataona vinafaa kama vya kuangalia vichocheo vya uzalishaji mbegu, Ultrasound na vinginevyo.

MATIBABU

Hutibiwa katika hospitali kwa daktari wa matatizo ya uzazi. Tiba hutolewa baada ya uchunguzi wa kina. Mojawapo ya dawa ni za kawaida za hospitali na ikishindikana basi upandikizaji utafanyika ili kukuwezesha upate watoto.

Leave A Reply