The House of Favourite Newspapers

Matatizo yanayowafanya watoto waugue mara kwa mara-2

0

Three kids giving thumbs up signWiki iliyopita nilianza kuzungumzia mada hii, leo nitaendelea kuanzia pale nilipoishia. Ikumbukwe kwamba, mtoto anaweza kupata Kifua Kikuu au ajali za utotoni kama kuungua, kuanguka au kumeza vitu kama sarafu n.k.

Baada ya miaka mitano, mtoto husumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza, minyoo ya safura na mengine, utapiamlo, malaria, magonjwa ya ngozi kama mapunye na ukurutu au muwasho wa ngozi na magonjwa ya njia ya hewa kama tulivyoona hapo awali.

DALILI ZA MATATIZO KWA MTOTO
Pamoja na mtoto kuwa mgonjwa, dalili kuu za ugonjwa hujitokeza baada ya ugonjwa kuwa mkali. Dalili za awali ambazo mtoto huonesha hutegemea na umri, lakini hapa nitazielezea kwa ujumla kwa hiyo utalinganisha na umri wa mwanao;

Mtoto hulia sana hata ukimbembeleza hatulii, mtoto hulialia tu mara kwa mara, kuonesha dalili kuwa hana raha na kuwa mnyonge, kukataa kula na kujaza chakula mdomoni au kutema, kutulia sehemu moja na kutocheza na wenzake, kulala kila wakati au muda mwingi na mwili kulegea.

Pia kushtukashtuka na kuogopaogopa wakati mwingine hutaka ashikwe na mtu mmoja tu, kulia sana anapoguswa sehemu fulani za mwili. Hizi ni baadhi tu ya dalili ambazo mzazi anatakiwa azifuatilie kwa umakini kwa mtoto.

MAMBO YA KUZINGATIA KWA MZAZI
Kumlea mtoto ili awe na afya nzuri ni jukumu la wazazi wote wawili, yaani baba na mama lakini pia ni jukumu la jamii na serikali kwa ujumla.

Mzazi ahakikishe mtoto anapata chakula bora siyo bora chakula ili kumuepusha au kumkinga asipate utapiamlo ambao utamdhoofisha katika ukuaji na maendeleo yake kwa ujumla. Chakula bora ni kile chenye protini, wanga, vitamini na mafuta kiasi.

Katika mlo wa mtoto hakikisha kuna mboga za majani na matunda kwa kuzingatia na umri wa mtoto. Mtoto apate maji safi kwa matumizi yote na aishi katika mazingira safi na yaliyo bora, mtoto apate chanjo zote zinazotakiwa kulingana na utaratibu wa kitaifa ili kumuepusha na maradhi yanayoepukika kama surua, kifua kikuu au TB na kifaduro.
Mtoto apate matibabu sahihi baada ya uchunguzi kulingana na umri wake, matibabu apate hospitali.

MAENEO YA UBORESHAJI
Ili kumfanya mtoto wako awe na afya bora na mvuto katika jamii ni jambo rahisi na ambalo halina gharama. Wengi tunadhani afya bora ya mtoto ni kumpeleka hospitali anapoumwa, pamoja na hilo lakini katika kuboresha afya ya mtoto ni vema tukazingatia mambo yafuatayo;

Kwanza ni upande wa lishe, hapa ni lazima tuangalie aina ya chakula kinachopatikana katika eneo unaloishi na ubora wake, kama chakula hakipatikani cha kutosha au hakina ubora, basi mtoto hawezi kuwa na afya nzuri hivyo ni rahisi kuandamwa na maradhi na akipata magonjwa yanakuwa makali. Vile vile lishe duni ya mtoto hudumaza mwili na akili.

Pili ni upande wa mazingira ambayo mtoto anaishi, muhimu mtoto alale mahali pazuri na salama, pia acheze mahali pazuri na salama, ale chakula kizuri na chenye ubora, maji safi ya kunywa na kuoga pia yawe salama. Mtoto apate hewa safi muda wote siyo maeneo yenye uchafuzi wa hewa kama harufu mbaya, joto kali, moshi, mavumbi, au hewa nzito huathiri afya ya mtoto.

Mtoto atumie choo safi na salama, avae nguo nzuri na safi muda wote, acheze na watoto wenye tabia nzuri na mahali pazuri.

Mwepushe mtoto na maambukizi mbalimbali ambayo tumeshayaona au mazingira yanayosababisha maambukizi. Maambukizi yoyote kwa mtoto hutibika hospitali. Maambukizi huzuilika kwa chanjo, lishe bora na kuwahi uchunguzi na tiba hospitali.

Tuwe makini na imani za jadi kwa watoto kama kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji badala ya hospitali, kuepuka baadhi ya vyakula kwa mama mjamzito na mtoto ni imani potofu, tuepuke ukataji vimeo na ukeketaji.

Leave A Reply