The House of Favourite Newspapers

MATESO MTOTO HUYU USIPIME

IMEANDIKWA kwamba, kuna wakati wa kucheka na wakati wa kulia, wakati wa furaha na wakati wa huzuni; alipozaliwa lssaya Merikion mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu, wazazi wake walifurahi lakini sasa wanahuzunika kutokana na mateso anayopitia mtoto wao.  

 

Chanzo cha mateso ya Issaya ni kuchomwa sindano na daktari aliyekuwa akimuongezea damu wakati alipofikishwa kwa matibabu katika hospitali moja (jina linahifadhiwa) iliyopo mjini Morogoro ambayo baadaye inadaiwa kuathiri mzunguko wa damu na kuufanya mkono wa mtoto huyo ukauke.

 

Mama wa mtoto huyo aitwaye Regina Hassan akiwa mkoani Morogoro aliliambia Uwazi hivi karibuni kuwa: “Mimi naishi Mzumbe Wilaya ya Mvomero, mwanangu alikuwa ana tatizo la upungufu wa damu mwilini. “Zahanati ya Mzumbe walituambia kuwa tumlete kwenye hospitali kubwa hapa mjini ili apatiwe tiba zaidi.

 

“Tulipofika tulilazwa na kuandikiwa matibabu ikiwemo kuongezewa damu, daktari alipomchoma sindano ya kuongeza damu mkono ulianza kubadilika rangi baadaye ukakauka kama kuni.”

WAHAMISHIWA MUHIMBILI

Baada ya hali ya Issaya kuwa mbaya, baadhi ya wauguzi wa hospitali hiyo walimwambia mama huyo kuwa atulie na kwamba mwanaye watamsafirisha kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya tiba zaidi. “Nilijua pengine wangeniwezesha kwenda Muhimbili kwa gharama zao lakini nimejikuta natumia fedha zangu na hapa kila kitu najihudumia,” alisema mama wa Issaya ambaye kwa sasa amelazwa katika wodi ya watoto.

 

MAJIBU YA MADAKTARI

Mama wa Issaya aliliambia Uwazi lililofika Hospitali ya Muhimbili kumjulia hali kuwa, bado hali ya mwanaye ni mbaya na kwamba yuko kwenye mateso ambayo hayaelezeki.

Alisema, muda wote amekuwa kwenye matumaini kuwa huenda kufika kwake Muhimbili kungebadilisha majibu ya awali aliyopewa na daktari wa Morogoro kuwa upo uwezekano mkubwa mkono wa mtoto ukakatwa. “Namuangalia mwanangu nabaki nalia, nimemzaa akiwa mzima na mwenye afya njema, leo akatwe mkono, naumia sana.

 

“Bora basi angeugua huo mkono wenyewe, lakini mtu unampeleka mtoto hospitali kwa ugonjwa mwingine matokeo yake anapewa kilema cha maisha, ukiuliza unaambiwa ni makosa ya daktari,” alisema mama huyo huku akibubujikwa na machozi.

 

Aliongeza kuwa majibu ya awali aliyopewa na daktari wa Muhimbili mara baada ya kufanyiwa vipimo vya awali ni kwamba hakuna njia nyingine ya kuurudisha mkono wa Issaya katika hali yake ya kawaida na kwamba wanachosubiri hivi sasa ni siku ya kuukata.

DAKTARI ASISITIZA MKONO LAZIMA UKATWE

Daktari maarufu mkoani Dar es Salaam ambaye amefanya kazi katika hospitali mbalimbali za mkoa huo aitwaye Godfrey Chale alisisitiza kile alichosema wiki iliyopita kuhusu matibabu ya mtoto huyo ni kwamba lazima mkono ukatwe.

 

“Kama nilivyosema ule ugonjwa unaitwa Dry Gangrene kitalaam, sasa kama yalifanyika makosa katika kutoboa mishipa ya damu wakati wa kuongeza damu na kusababisha madhara, tiba yake huwa ni kukata sehemu iliyoharibika. “Nadhani hata sasa madaktari wanasubiri kuona ni wapi tatizo limekomea katika mkono huo ili kujua sehemu wanayoweza kuukatia,” alisema Dk. Chale.

 

Aliongeza kuwa, mara nyingi tatizo kama hilo hutokea pale daktari anayeshughulikia zoezi la kuongeza damu anapoiongeza kimakosa kupitia mishipa inayosafirisha damu nyepesi (artery) kutoka kwenye moyo kwenda mwilini na kuacha mishipa inayosafirisha damu nzito kuelekea kwenye moyo kisha kusambaa mwili mzima yaani veins.

 

MAMA AILILIA SERIKALI

Akiongea na gazeti hili mama huyo alisema hawezi kupingana na makosa ya kitabibu lakini kinachomuuma ni kuona waliosababisha tatizo hawasaidii chochote katika kugharamia matibabu.

 

“Mimi naomba sana serikali ibebe uchungu nilio nao kuhusu mwanangu; inisaidie katika matibabu maana nina hali ngumu. “Nashinda hapa hospitalini sina hata fedha ya chakula mimi na mwanangu, ni mateso juu ya mateso huku unaoguza huku huna hata fedha ya kuweza kujikimu, inaniuma sana,” alisema mama huyo.

 

UWAZI LASAKA MAJIBU YA HOSPITALI

Tangu tatizo la mtoto litokee katika hospitali hiyo kubwa iliyopo mkoani Morogoro, Uwazi limekuwa likimsaka bila mafanikio mganga mkuu wa hospitali hiyo ili kujua tatizo ni nini na wao wanalishughulikiaje.

 

Hata hivyo jitihada za kumtafuta bado zinaendelea licha ya kwamba uchunguzi wa awali unaonesha kuwa ipo mikakati ya kutaka kulizima jambo hili kiaina. Aidha, baada ya kupatikana kwa msemaji wa hospitali hiyo ndipo gazeti hili litapata nafasi ya kuanika jina la hospitali hiyo pamoja na kutafuta majibu ya wizara inayoshughulikia masuala ya afya hapa nchini.

Kwa mtu yeyote ambaye anagushwa na mateso ya mtoto Issaya anaweza kuwasiliana na mama wa mtoto huyo kwa namba za simu 0719 777093, Waswahili husema kutoa ni moyo si utajiri.

STORI: MEMORISE RICHARD, UWAZI

Comments are closed.