The House of Favourite Newspapers

MATESO YA FAMILIA HII TEMEA MATE CHINI!

JE! Mungu mwenye upendo anawezaje kuruhusu mateso ya namna hii kuendelea katika ulimwengu aliouumba? Ndivyo unavyoweza kujiuliza baada ya kusoma habari hii kuhusu familia ya Mzee Sabili na kuishia kutemea mate chini ili yasikukute. 

 

Familia hii inayoishi wilayani Mkuranga, Pwani ipo kwenye mateso na masikitiko makubwa baada ya watoto wake wanne, mmoja ni marehemu kuzaliwa wakiwa walemavu wa viungo na akili. “Kwa kweli hakuna kinachoniumiza kama kila ninapobeba ujauzito na kuzaa watoto wangu wenye matatizo. Naumia sana huku wanawake wenzangu wakizaa watoto wao wakiwa wazima wa afya njema,” ndivyo anavyoanza kusimulia mama wa watoto hawa, Zena Sabili.

 

Katika mahojiano na Gazeti la Ijumaa hivi karibuni lilipoitembelea familia hiyo, mama huyo anasema mara nyingi anapopata ujauzito anakuwa yuko vizuri tu, lakini anapojifungua, watoto hukaa mwaka mmoja kisha wanaanza kubadilika.

 

BAADA YA MWAKA

Anasema baada ya mwaka mmoja, mtoto huanza kupata homa kali ya degedege kabla ya kupata ulemavu huo. “Unajua nilipozaa mtoto wangu wa kwanza Hamidu (20) na kupata matatizo hayo, nilijua wazi ni ugonjwa tu, lakini haiwezi kutokea tena kwa watoto wangu wengine.

 

“Lakini ndivyo ilivyotokea kwa mtoto wa pili, Rajabu (16) ambaye ni marehemu kisha akaja Hussein (13) na Shani (10), hali ikawa hivyohivyo. Nikawa sina jibu halafu pia huku kwetu ni kijijini sana na hakuna pa kukimbilia,” anasema Zena kwa uchungu.

Anaendelea kusema kuwa aliendelea kuzaa hivyohivyo hadi mtoto wa nne ambaye pia alikuwa ni mlemavu. Jambo hili linawaumiza na kuwachanganya mno yeye na mumewe.

 

HAWAWEZI LOLOTE

“Tunavyoongea hapa, hatujui la kufanya. Unavyoona watoto hawa wote hawajiwezi kwa lolote lile, si kutembea wala kuoga  wenyewe. Kubwa zaidi hawawezi kuongea kwa hiyo kila kitu ni hapohapo na sisi wazazi tunategemea kilimo hivyo tumepunguza kwa ajili ya hawa watoto maana kuwaangalia peke yangu ni shida kubwa sana,” anasema mama huyo wa watoto hawa.

 

Aliongeza kuwa, baada ya kuzaa watoto hao wenye matatizo baadaye alizaa tena na kwa bahati nzuri mtoto huyo akawa yupo vizuri, lakini aliposema ngoja aongeze wa mwisho ili waje kumsaidia ndipo yakajirudia yaleyale kwani huyo wa mwisho naye anaelekea kupata tatizo kama la ndugu zake.

 

ATAMANI KUNYWA SUMU

“Kuna kipindi kilifika nilitamani kabisa kunywa sumu kutokana na uchungu ninaoupata, kuona watoto wangu wako katika hali hii na bado hata chakula kupatikana ni shida sana maana tunakula mlo mmoja tu kwa siku. “Kila nikijaribu kwenda hospitalini, hakuna kinachoonekana na huku kulivyo mbali na mjini, huduma za afya hakuna hivyo ninabaki kumlilia tu Mungu, naamini ipo siku atasikia kilio changu,” anasema Zena akitokwa na machozi.

 

MUNGU ATAKULIPA

Kusema kweli familia ya Mzee Sabili iko kwenye mateso makubwa, kama umeguswa na tatizo la familia hii unaweza kuwachangia chochote kupitia namba 0713 612 533. Hata kama una nguo, godoro na kingine chochote, familia hii inakihitaji na Mungu atakulipa maradufu. -Mhariri

Comments are closed.