The House of Favourite Newspapers

Mateso ya Mtoto Huyu… Mungu Tenda Muujiza!

MUNGU tenda muujiza juu ya mtoto huyu! Ndiyo maneno pekee yanayoweza kukutoka baada ya kusoma mateso anayopitia mtoto huyu huku akipita kwenye bonde la mauti.

Mtoto Rehema Elisha (5), mkazi wa Mbagala-Mzinga jijini Dar yupo kwenye hali mbaya (koma).

Mtoto Rehema yupo kwenye hali hiyo baada kugundulika kuwa na kansa ya ubongo, jambo ambalo limemfanya ashindwe kuongea, kutembea, kula na pia haoni tena kwa sasa huku mama yake akiishia kulia kila kunapokucha.

 

Akizungumza kwa uchungu na gazeti hili, mama mzazi wa mtoto huyo, Salma Salumu au Mama Rehema alisema mtoto wake huyo alianza kuumwa tangu mwezi wa pili, mwaka jana.

Alisema alianza kusumbuliwa na tumbo ambapo kila akiamka alikuwa akimlalamikia tumbo linamuuma hivyo alimpeleka zahanati ya karibu, lakini kila alipopimwa, vipimo vilionesha hana tatizo.

 

“Rehema alianza kama utani tu. Alianza kulalamika tumbo linamuuma, nikajua labda ni minyoo hivyo nikampeleka hospitalini kumpima, lakini vipimo havikuonesha chochote na hali ikawa inaendelea kuwa mbaya sana kila kukicha,” alisema Mama Rehema.

Aliendelea kusema kuwa, akiwa anaendelea kutafuta tatizo la tumbo linasababishwa na nini ndipo akaanza tatizo jingine jipya la kulalamika kichwa kinamuuma.

Alisema kuwa, baada ya kuona hivyo alimpeleka Rehema hospitalini tena na kumpima kila kitu ambapo hali ilikuwa kama mwanzo kwani hakukutwa na ugonjwa huku akiendelea kulalamika maumivu ya kichwa.

 

“Kichwa kilikuwa kinamuuma sana kiasi ambacho alifikia hatua ya kushindwa kabisa kulala,” alisema mama Rehema.

Mama huyo alisema alipoona Rehema anazidiwa, alimpeleka kwenye Hospitali ya Temeke ambapo madaktari walimpima.

Alisema kama ilivyokuwa mwanzo, vipimo pia havikuonesha chochote hivyo walimwandikia kwenda kliniki kila wiki.

Alisema kuna siku mtoto wake huyo aliumwa hadi akapata degedege, akaanguka na kujigonga vibaya sakafuni.

“Baada ya hapo tulimkimbiza Hospitali ya Temeke na baada ya hapo tuliambiwa tumpeleke Muhimbili.

 

“Tulipofika Muhimbili alipumzishwa na kutakiwa kufanyiwa kipimo cha CT-Scan ambapo ilihitajika shilingi 210,000 ambazo hatukuwa nazo hivyo tulirejea nyumbani.

“Miezi miwili baadaye mateso ya mwanangu yalizidi huku nikimuona kabisa akipita kwenye bonde la mauti ndipo tukachangishana na kiasi tulichopata ndicho tukaenda nacho na kupima.

“Hata hivyo, majibu yalipotoka walisema Rehema ana uvimbe mkubwa kwenye ubongo,” alisimulia mama huyo.

 

Aliendelea kusema kuwa, baada ya vipimo hivyo kutoka ilikuwa ni lazima kumuona daktari bingwa wa kansa ambapo alimwambia mwanaye anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kichwa.

Alisema katika hatua hiyo aliambiwa kuwa kuna kufa au kupona, lakini ilibidi akubali.

Mama Rehema alisema walipokuwa wakimfanyia upasuaji walichukua vinyama na kwenda kuvipima ndipo alipogundulika kuwa na kansa ya ubongo.

 

“Nilipopewa majibu hayo nililia sana, lakini nilikuwa sina jinsi maana hospitalini waliniambia kabisa kuwa mwanangu hawezi kupona.

“Baada ya hapo hali ya Rehema ilizidi kuwa mbaya kwani alianza kupoteza uwezo wa kuona, kutembea na kula kwani alikuwa anang’ata meno hivyo ilibidi niwe ninamlisha kwa mpira.

“Hapo maisha ya Rehema yakawa yameharibika kabisa na kuanza kudhoofu sana wakati kabla ya tatizo alikuwa mchangamfu mno.

 

“Hapa nilipo nimepoteza matumani kabisa ya mwanangu kupona baada ya kuambiwa hawezi kupona tena, hapa nasubiri mapenzi ya Mungu yatimie,” alisema mama huyo akionesha kukata tamaa.

Alimalizia kuwa kwa sasa mwanaye yupo naye nyumbani ambapo amekuwa akifanyiwa kila kitu akiwa amelala kimya tu.

Kikubwa mtoto huyo anahitaji msaada wa hali na mali kama pampers, chakula, matibabu na vitu vingine kwa ajili ya uangalizi.

 

Kama umeguswa na habari hii ya mateso ya mtoto huyu unaweza kuwasiliana na mama yake huyo kupitia namba 0714 986 242 au 0719 840 890

Risasi Jumamosi linamsihi mama Rehema kutokata tamaa kwani kwa Mungu kila jambo linawezekana.

 

STORI: Imelda Mtema, Risasi Jumamosi

Comments are closed.