visa

Mateso100% Binti adai KULAZWA KWENYE BANDA LA KUKU

PWANI: Mateso asilimia 100! Ndivyo walivyozungumza majirani wakati wakielezea tukio la binti anayedawa kulazwa kwenye banda la kuku, Amani linakushushia tukio zima!  Mwanadada Salma Ally, mkazi wa Kibaha-Kwa Mathias mkoani Pwani ameelezea kilio chake kwa kudai kulazwa kwenye banda la kuku wakati baba, mama yake wa kufikia na watoto wa mama huyo wakilala ndani ya nyumba kubwa ya baba yake.

Akizungumza na waandishi wetu, Salma ambaye alijifungua miezi miwili iliyopita na bado anahitaji msaada kama mama aliyejifungua, alielezea mateso makali anayopata ambayo amedai yanasababishwa na mama yake wa kufikia aliyemtaja kwa jina la Janeth Mathayo.

Awali, majirani wa eneo hilo waliwapigia simu makachero wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) wa Global Publishers na kumueleza mkuu wa kitengo hicho maisha ya mateso anayoishi binti huyo. Baada ya kuelezwa, makachero walifika na kukutana na majirani hao ambao walisema siku hiyo wamepanga kwenda ‘kumchana’ Janeth kwani wamemchoka na tabia zake za kumlanza binti huyo kwenye banda hilo la kuku.

“Haya ni zaidi ya mateso, hatuwezi kukubali,” alisikika mmoja wa majirani. Wakiwa eneo la tukio, makachero wa OFM walifika kwenye banda analoishi binti huyo na kumkuta akiwa amejipumzisha ndani ambapo walimgongea hodi na kujitambulisha kisha kuanza kuzungumza naye.

Salma alisema maisha ya mateso anayoyapata kutoka kwa mama yake huyo ndiyo yanayomfanya atangetange na dunia.“Kutokana na maisha ninayoishi hapa na mama yangu wa kufikia hataki niingie ndani kwenye hii nyumba ambayo ni ya baba yangu mzazi.

Baba naye alijaribu sana kunitetea japo nilale ndani lakini mama huyu wa kufikia amemwambia nikiingia ndani kulala basi yeye ataondoka na kumuachia nyumba hivyo baba akiambiwa hivyo naye anakuwa katika wakati mgumu.

“Hapa jirani kuna nyumba ya bibi yangu ambaye aliniambia nikalale na kula hapo lakini huyu mama aliposikia ukazuka ugomvi mkubwa akamfuata bibi na kumfokea kuwa ndiyo ananidekeza na mimi nikikaa hapo baba amekuwa akileta pesa ya matumizi na yeye amekuwa akiachiwa kiasi kidogo cha pesa kwa ajili ya kukigawa sehemu mbili.

“Hali hiyo ilisababisha bibi aogope kuishi nami na kuniambia nirudi kwa baba yangu hivyo nikalazimika kuishi kwenye hiki kibanda, wenzangu wakiishi ndani ambapo juu kuna sehemu imeezekwa makuti ya mnazi na sehemu nyingine haina hata makuti ambapo mvua imekuwa ikininyeshea, napigwa baridi kali na hivi karibuni nilijifungua baada ya kupata mimba isiyotarajiwa kutokana na kuishi maisha ya dhiki hata hivyo huyo mwanangu hakuweza kuishi alikaa siku chache na kuaga dunia.

“Nimejifungua hivi karibuni lakini sina hata mtu wa kunikanda maji ya moto. Kuna siku nilizidiwa na njaa nilimuomba mama anikorogee japo uji kidogo akakataa kabisa.

“Hali ilipozidi kuwa mbaya majirani walijikusanya na kuokota kuni na kutafuta sufuria ya kupika uji ambapo nao walikwenda kumuomba unga wanikorogee uji nao aliwakatalia ndipo wakaamua wenyewe kufanya walivyoweza na kunipikia uji,” alisema kwa uchungu binti huyo na kuendelea:

“Hapa sina pakula wala pakulala naomba msaada jamani maana hapa ninapolala hivi karibuni niliangukiwa na nyoka usiku na hiki kibanda hakina mlango wa kufunga hivyo naweza kufanyiwa ubaya wowote.”

Baada ya kuzungumza na Salma, wanahabari wetu walimfuata bibi wa binti huyo aliyejitambulisha kwa jina la Salma Khalfani ambaye alisema ameshawahi kumpokea mjukuu wake huyo ambaye ni wajina wake lakini ukaibuka mgogoro mkubwa ambapo na mama yake wa kufikia.

“Mama huyo ambaye ni mke wa mwanangu alianzisha mgogoro mkubwa akimtuhumu mumewe kuwa alikuwa akiniletea pesa ya matumizi kwa ajili ya mwanaye. Mjukuu wangu nampenda na kumuonea huruma lakini sikuwa na jinsi nilimwambia arudi kwa baba yake,” alisema.

Wanahabari wetu katika kuendelea kupata uzani wa habari walimtafuta mjumbe wa nyumba kumi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Athumani Pungu ambaye alikiri kupokea taarifa za mateso ya binti huyo na kuelezea jinsi alivyohangaika kuusuruhisha mpaka alipofikia.

“Taarifa za mateso ya huyu binti nimeshaletewa na mimi na kamati yangu tulishakaa kikao na mama yake wa kufikia anayedaiwa kumtesa lakini mama huyo aliendelea na msimamo wake wa kumkataa binti huyo ndani mwake.

“Nilizungumza na baba wa binti huyo anipe uamuzi wake lakini naye amesema binti huyo akirudishwa ndani basi mama huyo atamuachia nyumba na kuondoka hivyo jamaa hapo akawa amechanganyikiwa hajui afanyeje,” alisema mjumbe huyo.

Mama huyo baada ya kuhojiwa kwa nini alikuwa akimtesa binti huyo alisema huyo siyo mwanaye na kuwaonesha mapaparazi wetu watoto wake. “Hawa ndiyo wanangu huyo simtambui,” alisema bi mkubwa huyo. Alipoambiwa haoni kama mtoto wa mumewe ni mwanaye, mama huyo akasema;

“Nimeshasema huyo siyo mwanangu angekuwa mwanangu angeniheshimu. Mimi huyo wala siyo mwanangu simtaki kabisa,” alisema mama huyo na kuingia ndani. Ilielezwa kuwa, binti huyo mama yake mzazi yuko hai lakini naye anaishi na mwanaume mwingine ambaye naye hataki kulea mtoto ambaye si wake.

Waandishi: Richard Bukos na Neema Adrian.
Toa comment