The House of Favourite Newspapers

MATIC AMETUA UNITED AISEE

0

MOJA ya usajili uliokuwa unasubiriwa kwa hamu kubwa ni wa kiungo wa Chelsea Nemanja Matic, kutua Manchester United. Mashabiki waliokuwa macho kila siku wakisubiri kujua ni lini usajili huo utakamilika baada ya porojo mbalimbali kuzagaa.

Lakini sasa mambo yamekamilika ambapo Nemanja Matic amesaini mkataba wa kuichezea Manchester United na kukata mzizi wa fitina.

Kiungo wa Chelsea Nemanja Matic.

Matic amesaini mkataba wa miaka mitatu na United kwa kitita cha pauni milioni 40, zaidi ya shilingi bilioni 130, huku akionekana kuwa atakuwa suluhisho la safu ya kiungo ya kocha Jose Mourinho, ambaye msimu uliopita hakufanya vizuri kwenye ligi pamoja na kwamba alitwaa ubingwa wa Kombe la Europa na Kombe la Capital.

 

Kiungo huyo ni kati ya wale ambao walifanya kazi nzuri sana kwenye kikosi cha Chelsea cha msimu uliopita, ambacho kilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England. Lakini baada ya msimu kumalizika kocha wa timu hiyo, Antonio Conte, alisema kuwa kiungo huyo kama akipata timu ya kwenda litakuwa jambo zuri kwa kuwa anaamini kuwa msimu ujao hatapata nafasi ya kutosha kwenye timu hiyo. Hata hivyo, chaguo la kwanza la kiungo huyo lilikuwa kwenda Manchester United ambayo pia ipo kwenye Ligi Kuu ya England.

 

Hata hivyo, Matic anaonekana kuwa kati ya viungo bora zaidi kwa sasa kwenye ligi hiyo na ndiye mchezaji pekee ambaye ametajwa kusajiliwa na kuungwa mkono na wachezaji wengi wa zamani wa timu hiyo. Juzi mchezaji huyo aliweka picha kwenye mitandao ya kijamii akionekana akiwa amevalia jezi ya Manchester United, kuonyesha kuwa anaiunga mkono timu hiyo na sasa dili hilo limekamilika.

Kocha Jose Mourinho (kulia) akimpongeza enzi wakiwa pamoja Chelsea.

United wamefanikisha usajili huu na kwamba watakuwa wamekamilisha usajili wa tatu mkubwa msimu huu baada ya awali kumsajili beki wa kati Victor Lindelof na mshambuliaji Romelu Lukaku. Mourinho ndiye ambaye alimsajili Matic kwenye kikosi cha Chelsea mwaka 2014 na sasa wanaungana tena wakiwa kwenye klabu tofauti. Kuonyesha kuwa mchezaji huyo anatarajiwa kuondoka, Conte alimuacha kwenye ziara yake ya michezo ya maandalizi ya msimu na alikuwa akifanya mazoezi peke yake kwenye klabu hiyo jijini London.

 

United wenyewe walikuwa wanasubiri kuona kama wakikamilisha usajili huo ndiyo watamuuza kiungo wao Marouane Fellaini, ambaye anatajwa kuwa anaweza kujiunga na timu kadhaa lakini Galatasaray ya Uturuki ndiyo inapewa nafasi kubwa sana ya kumtwaa ingawa kocha Jose Mourinho anaweka ngumu.

 

“Nasubiri taarifa, najua kuwa Matic anataka kujiunga na United, kama mchezaji anataka kujiunga na klabu yetu basi nafasi ya kuja inakuwa kubwa sana, lakini kama yeye hataki basi nafasi inakuwa ndogo,” alisema Mourinho alipohojiwa muda mchache kabla dili hilo halijakamilika. Matic  raia wa Serbia, mwenye umri wa miaka 28, anaaminika kuwa anaweza kumaliza tatizo la kiungo kwenye klabu hiyo ambayo msimu ujao itakuwa ikishiriki kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kiungo huyo ambaye alijiunga na Chelsea  akitokea Benfica hii ilikuwa mara ya pili kuitumikia timu hiyo ya London baada ya kukaa hapo tena mwaka 2011 na kuondoka. Pamoja na kwamba amekuwa mahiri kwenye timu ya taifa ya Serbia, katika maisha yake ya soka ameshacheza michezo 352 na kufunga mabao 22.

Leave A Reply