The House of Favourite Newspapers

Matokeo uchaguzi… Lowassa mbishi

0

Stori: Erick Evarist

MBISHI! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Ngoyai Lowassa kuonekana kujibu mashambulizi ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Joseph Magufuli katika matokeo ya uchaguzi mkuu yanayoendelea kutangazwa nchini, Risasi Mchanganyiko linakupa ‘full’ stori.

Mpaka tunakwenda mitamboni jioni jana, Lowassa alionekana kupangua matokeo kwa kumkaribia Magufuli aliyekuwa akiongoza katika ambayo yanaaminika ni ngome ya Lowassa na Ukawa, alichanua makucha yake na kumfunika Magufuli licha ya matokeo ya jumla kuonesha Magufuli anaongoza kwa asilimia 58 dhidi ya 41.

MAENEO ALIYOTINGISHA

Katika jimbo la Katavi kwa mfano ambako  Magufuli alipata kura 31,413 dhidi ya 6046 za Lowassa, mgom bea huyo wa Ukawa alionekana kufanya vizuri katika jimbo la Mtwara, ambako alishinda kwa kura 19,017 dhidi ya 33, 699 za mgombea wa CCM.

Wakati wawili hao wakionekana kufuatana kwa wastani mzuri katika baadhi ya maeneo, wagombea wa vyama vingine walikuwa wakipata kura chini ya 500 kwa kila jimbo.

Kama hiyo haitoshi, katika Jimbo la Kisarawe, Lowassa alifanikiwa kupata kura 13,230 na kumkaribia mpinzani wake Magufuli aliyepata kura 24860. Kuonesha Lowassa mbishi, katika Jimbo la Mbinga Mjini, mkoani Ruvuma hakuwa mbali ya mpinzani wake, licha ya kuwa ni ngome ya chama tawala, kwani aliweza kupata kura  11,000 dhini ya 29295 za Magufuli.

Kwenye Jimbo la Nanyamba huko Mtwara ambalo Magufuli alipata kura 24904, Lowassa naye alionesha ujemedari wake kwa kupata kura 16992.

NGOME ZAKE

Kuonesha kwamba Lowassa alikuwa mbishi kuhakikisha hachezi mbali na mshindani wake, katika maeneo yanayoaminika kama ni ngome zake, Lowassa alimkimbiza vibaya Magufuli katika maeneo kama Moshi Mjini ambapo alishinda kura 49379 dhidi ya 28909 za Magufuli.

ARUSHA MJINI USIPIME

Katika Jimbo la Arusha Mjini, Lowassa alijitwalia kura 150,786 na kumuacha mbali mpinzani wake Magufuli ambaye aliambulia kura 65107.

Ukiachana na maeneo ambayo yanaaminika ni ngome ya Lowassa, mpaka jana wakati tunakwenda mitamboni, matokeo ya jumla yalionesha Magufuli alikuwa akiongoza katika majimbo mengi huku kukiwa na matumaini makubwa ya mgombea huyo wa CCM kuibuka kidedea na hivyo kuwafanya wafuasi wa vyama vya upinzani nchini kupoa.

MAGUFULI ATABIRIWA USHINDI

Wananchi mbalimbali ambao walitoa maoni yao baada ya Magufuli kuongoza kwa asiliamia 58 dhidi ya 41 za Lowassa hadi tunakwenda mitamboni jana, waliliambia Risasi Mchanganyiko kuwa licha ya ubishi wa Lowassa, kuna uwezekano mkubwa wa Magufuli kuibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha urais.

Wananchi hao walianisha kuwa kuna majimbo mengi ambayo yanaaminika ni ngome ya Magufuli hayajatangazwa huku yale ambayo ni ngome ya Lowassa yakibakia machache.

“Hakuna ubishi, Magufuli ndiyo ataibuka kidedea maana fikiria kuna majimbo mengi ya Kanda ya Ziwa ambayo ni ngome yake bado hayajatangazwa. Uzuri ni kwamba Magufuli ameshapenya katika maeneo hatari ya Lowassa ikiwemo Pemba na Arusha na bado anaongoza,” alisema Juma Hajj, mkazi wa Dar.

MTAJI WA VIJIJINI WATAJWA

Mkazi mwingine wa Arusha ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alisema;

“Magufuli ana mtaji mkubwa sana katika maeneo mengi aliyoweza kuyafikia wakati wa kampeni hususan vijijini, tofauti na Lowassa ambaye amefanya mikutano michache katika maeneo ya mjini pekee.”

MAJIMBO YALIYOTANGAZWA

Mpaka tunakwenda mitamboni, majimbo 87 kati ya 264 yalikuwa tayari yameshatangazwa huku baadhi ya majimbo ya mikoa kama Tanga, Morogoro, Iringa, Tabora, Singida ambayo inaaminika ni ngome ya CCM ikiwa bado haijatangazwa.

Kama hiyo haitoshi, kuna mikoa inayounda Kanda ya Ziwa kama Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Bukoba, Mara na  Geita, nyumbani kwa Magufuli ambayo inaaminika ina wapiga kura wengi zaidi wanaomuunga mkono, hadi tunakwenda mitamboni ilikuwa bado haijatangazwa hivyo kuzidi kumpa nafasi kubwa ya ushindi.

Wakati huohuo, katika majimbo ya mkoa wa Dar es Salaam, ule msemo wa mende kuangusha kabati ulitimia, baada ya wagombea wawili walioonekana kuwa na nguvu kubwa, Abbas Mtemvu wa Temeke na Didas Masaburi wa Ubungo, waliangukia pua baada ya kujikuta wakibwagwa na wapinzani wao wa Ukawa.

Masaburi alishindwa mbele ya Saeed Kubenea wa Chadema wakati Mtemvu, alishindwa kutetea kiti chake mbele ya Abdallah Mtolea wa Cuf. Hata hivyo, Faustine Ndungulile wa Kigamboni (CCM) na Halima Mdee (Chadema) wa Kawe wamefanikiwa kutetea majimbo yao.

Leave A Reply