The House of Favourite Newspapers

Matumizi ya Teknolojia Yaongeza Ushiriki Masoko ya Mitaji

MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema katika mwaka 2024 kumekuwa na mafanikio makubwa ambayo yamewezesha pia thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji kuongezeka kwa asilimia 24.7 na kufikia Sh.trilioni 46.7 katika kipindi kilichoishia Desemba 2024, ikilinganishwa na Sh.trilioni 37.4 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023.

Akizungumza leo katika hafla fupi Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama amesema thamani ya uwekezaji katika hisa za kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa yaani imeongezeka kwa asilimia 22.3 na kufikia Sh.trilioni 17.87 katika kipindi kilichoishia Desemba 2024, ikilinganishwa na Sh.trilioni 14.61 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023

Ametaja baadhi ya mafanikio mengine ambayo yamepatikana ni uwepo wa Bidhaa Mpya na Bunifu ambapo amesema mwaka 2024 umeshuhudia utoaji wa bidhaa mpya na bunifu zinazovutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Amefafanua mathalani, Hatifungani ya kijani ya taasisi ya umma iliyotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Jiji la Tanga (Tanga-UWASA) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya miundombinu ya maji na utunzaji wa mazingira,ambayo ilikusanya Sh.bilioni 54.72, na kuvuka lengo la kukusanya shilingi bilioni 53.2, sawa na mafanikio ya asilimia 103


CPA.Mkama pia amesema mwaka 2024, umeshuhudia mwamko mkubwa wa utoaji bidhaa mpya na bunifu katika Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja, hivyo kuweka wigo mpana wa fursa za uwekezaji kwa watanzania wa kada mbalimbali, ikiwa ni Pamoja na vijana, wanawake na makundi maalumu.


“Vilevile, Zan Securities na Orbit Securities walizindua mifuko ya Timiza na Inuka, huku Alpha Capital ikianzisha Mfuko wa Halal. Aidha, Sanlam Investments East Africa ilizindua SUTS – SANLAM Unit Trust Scheme, ikijumuisha Sanlam Pesa Money Market Fund na US Dollar Fixed Income Fund.

“Kutokana na juhudi hizi, thamani ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (NAV) iliongezeka kwa asilimia 41.63, kutoka shilingi trilioni 1.84 mwaka 2023 hadi shilingi trilioni 2.61 mwaka 2024. Ukuaji huu umetokana na mikakati ya utoaji wa elimu kwa umma unaofanywa na wadau katika masoko ya mitaji na matumizi ya mifumo ya kidijitali, ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji mijini na vijijini.”Amesema.

Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano amesema imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza mauzo katika soko la hisa. Matumizi ya teknolojia ya Habari, ikiwa ni pamoja na matumizi ya simu za mkononi yameongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani, hivyo kuongeza ukwasi katika soko la hisa.