Maua Chenkula Adai Kusingiziwa Kifo Kulimpoteza Kwenye Ramani ya Muziki
MSANII wa nyimbo za Asili Maua Chenkula ambaye amekuwa akifanya mahojiano katika studio za 255globaradio na Global TV kwenye kipindi cha Mapito amesema kitendo cha kuzushiwa kuwa amefariki kimemuathiri kwa kiasi kikubwa katika tasnia yake ya muziki.
Maua amebainisha kuwa ilifikia kipindi akawa hapigiwi simu hata na marafiki wake wa karibu kwani wengi walijua kuwa amefariki, amedai kuwa ilikuwa vigumu kwa yeye kupata kazi au mialiko mbalimbali ya kufanya matamasha kwani ilifahamika amefariki.
Maua amedai kuwa mwanzo alichukuliwa jambo hilo kawaida, lakini kadri muda ulivyozidi kwenda ndivyo alivyoona athari hasi katika muziki wake.
“Walivyosema umekufa ukawa huonekani tena kwenye macho ya watu, lakini mimi ulitangazwa msiba nikawepo kwenye macho ya watu! Lakini bado ukienda sehemu nyingine tofauti mtu mwingine akikuona anauliza mbona umefanana na Maua ni ndugu yako? Nilikuwa Napata wakati mgumu sana kuwaelewesha kama ni mimi sijafa.” Alisema Maua.
Kwasasa Global Media kupitia kipindi chake cha Mapito imetoa rai kwa wadau wa muziki na watu mbalimbali wenye kuguswa na Maua Chenkula kufanya jitihada mbalimbali za kuwasiliana naye ili aweze kupata msaada wa kurudi tena na kuwika katika tasnia ya muziki kwani tayari ana nyimbo zake (Audio) nne ambazo tayari ameshaziandaa.