The House of Favourite Newspapers

MAUA SAMA AFUNGUKA KUMWAGWA NA MZUNGU

Image result for MAUA SAMA
Maua Sama

KUNA wakati ukiufuatilia sana muziki wa Bongo Fleva utakuwa unaona unabadilika kwa kasi siku hadi siku. Kuna kipindi utaona unaenda kasi na kipindi kingine taratibu.  Ndani ya miezi miwili tumesikia Ngoma ya Jibebe ikiteka muziki huo na kumfanya kila mmoja kuucheza na kuusikiliza, wakati ngoma hiyo ikiwa bado ‘hot’ mwanadada mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni, Maua Sama ni kama ameizima Jibebe baada ya kuibuka na Ngoma ya Iokote.

Si mitandao, vibanda vya simu, redio, TV, miito ya simu, Bajaj, teksi na hata bodaboda masikio na macho yao yamekuwa kwenye Iokote. Nyuma ya Iokote kuna bwa’mdogo mmoja hivi ameshirikishwa ambaye ni mtoto wa kaka wa marehemu Banza Stone, Hassan Masanja ‘Hanstone’.

Ukimsikiliza dogo huyo ni kama amepita mulemule kwa Diamond Platnumz, kuanzia staili hadi ‘kijimelodi’ kidooogo. Yote kwa yote, Over Ze Weekend imefanikiwa kukutana nao wote wawili na kufanya nao exclusive intreview juu ya muziki wao, tujiunge nao;

Over Ze Weekend: Hongera kwa Iokote ni gumzo mitaani. Lakini imekuwaje umeiachia mapema wakati ngoma yako ya Amen uliofanya na Ben Pol ikiwa bado ipo hoti?

Maua: Asante sana! Kwanza mashabiki wanatakiwa kujua, Iokote ilivuja bahati mbaya, lengo lilikuwa ni kutoa pamoja na video lakini tukashangaa kusambaa, kwa kuwa ni hit tukauacha tu.

Over Ze Weekend: Idea nzima ya wimbo huo ilikuwaje?

Maua: Tulikuwa studio tu pale kwa Prodyuza Abbah, tukawa tunapiga stori na mwisho wa siku tukajikuta tukiongelea wimbo huo na kuutunga hapohapo.

Over Ze Weekend: Turudi nyuma kidogo, Ngoma ya Amen, imekuletea mafanikio yoyote?

Maua: Mengi tu. Kwanza wimbo huo tuliutunga spesho kwa harusi na hadi sasa nimesha-fanya shoo nyingi kwenye harusi kupitia wimbo huo.

Over Ze Weekend: Uhusiano wako na MwanaFA upoje kwa sasa?

Maua: Tupo poa sana, sina tatizo naye.

Over Ze Weekend: Nirudi kwako Hanstone, ilikuwaje ukakutana na Maua?

Hanstone: Ilikuwa kama zali tu. Nilikutana na Dairekta Hanscana pale Sinza-Vatican (Dar) nikamwa-mbia kipaji changu akanielewa na kunipeleka kwa Fadhili Kondo ambaye ni meneja wangu na baada ya hapo nikatengeneza nyimbo kadhaa, nikawa nawasaidia wasanii wengine kupita kwenye nyimbo zao na hatimaye Maua akaniona.

Over Ze Weekend: Lakini staili yako ya kuimba kama Diamond hivi au wasanii kutoka Wasafi (WCB), hii ikoje?Image result for MAUA SAMA

Hanstone: Hapana, ni wimbo tu ndiyo ulinifanya niingie staili ya vile, nashangaa sana wengi wanafananisha sauti yangu na wengine, lakini nipo tofauti sana.

Over Ze Weekend: Kwa nini unapenda sana kuimba staili ya Reggae?

Maua: Napenda tu tangu nikiwa mdogo.

Over Ze Weekend: Inasemekana idea ya Iokote na biti imeibwa kutoka Wimbo wa Kwan-gwaru?

Maua: Hakuna kitu kama hicho. Ukisikiliza nyimbo zote ni za aina moja na ndiyo Bongo Fleva ilivyo, siwezi kuiba na haitakuja kutokea kwani nina kipaji cha kuandika mwenyewe na kuimba.

Over Ze Weekend: Turudi kwa Maua, kuna madai kuwa umemwagwa na Mzungu wako ambaye uliwahi kumpeleka ukweni Moshi akakuvalisha na pete kabisa?

Maua: (anacheka) Hakuna kitu kama hicho. Ujue Wabongo bwana wape picha tu ‘caption’ wataandika wenyewe! Yaani wamejaa kufuatilia mambo ya mtandao na kuyaamini. Kwa sasa nipo katika uhusiano na sipendi kuuweka hadharani.

ANDREW CARLOS

Comments are closed.