MAUA SAMA THT ILINIONDOA UOGA!
MAUA Sama ni miongoni mwa warembo ambao Kibongobongo wanafanya vizuri. Amezungumza na Gazeti la Risasi Mchanganyiko mambo mengi yanayohusiana na muziki wake, karibu:
Risasi: Kitu gani kilikushawishi kufanya muziki?
Maua: Napenda muziki maana tangu utoto wangu nilikuwa napenda sana kuimba na kuna watu ambao nilikuwa napenda kuwafuatilia na kuimba nyimbo zao.
Risasi: Katika familia yenu kuna mtu mwingine ambaye ana kipaji cha kuimba?
Maua: Zamani aliwahi kuwa babu yangu ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa akiimbia Bendi ya Msondo Ngoma enzi hizo, hivyo katika familia yetu ni mimi na yeye tu ndiyo watu ambao tuna kipaji cha kuimba.
Risasi: Nani ambaye huwezi kumsahau katika maisha yako kimuziki?
Maua: Kiukweli kabisa MwanaFA ni mtu ambaye ana mchango mkubwa sana katika muziki wangu maana yeye ndiye aliyegundua kipaji changu, naweza
kusema yeye ndiye mzizi wa mafanikio yangu mpaka hapa nilipofikia.
Risasi: THT imekuimarisha vipi katika muziki wako?
Maua: Kwa upande wangu THT imenifundisha, imenikomaza nimejifunza vitu vingi kuhusiana na muziki maana kabla ya kuwa msanii nilikuwa muoga lakini nilipoingia THT nimepata vitu ambavyo vimeufikisha muziki wangu hapa ulipo.
Risasi: Umeshatoa albam ngapi mpaka sasa?
Maua: Hakuna albam ambayo nishatengeneza ila kwa mwaka huu nina mpango wa kuandaa album.
Risasi: Nyimbo zako unatunga mwenyewe ama unatungiwa?
Maua: Vyote nafanya, naweza kutunga mwenyewe pia natungiwa.
Risasi: Msanii gani unamtazama kama mfano wa kuigwa?
Maua: Mimi mwenyewe najitazama kama mfano wa kuigwa.
Risasi: Msanii gani wa nje ya Bongo ambaye unatamani kufanya naye kazi?
Maua: Napenda sana na ninatamani kufanya kazi na wasanii kama vile Tiwa Savage kutoka Nigeria, Rihana, Beyonce, Drake kutoka Marekani na wengine wengi siwezi kuwataja wote ila baadhi yao ni hao.
Risasi: Una mpango gani katika kuufikisha muziki wako kimataifa zaidi?
Maua: Mpango upo wa kufanya kazi nyingi za kimataifa zaidi kwa mwaka huu kama nilivyosema baadhi ya hao wasanii ndio nina mpango wa kufanya nao kazi.
Risasi: Kiki zinanyanyua muziki wako?
Maua: Kwanza mimi siyo mtu wa kiki kwa sababu hazisaidii kitu katika muziki wangu japo kuna baadhi ya watu ambao wanaona kiki zinawatoa.
Risasi: Nini siri ya mafanikio ya kazi zako?
Maua: Siri kubwa ya mafanikio yangu ni muziki mzuri, jitihada kwenye kazi na kujitambua hasa mimi ni nani.
Risasi: Mbali na muziki una kipaji gani kingine?
Maua: Kuigiza ni kipaji kingine ambacho najitazamia kuwa nacho japo sijawahi kukifuatilia kiundani zaidi.
Risasi: Neno kwa mashabiki wako.
Maua: Ningependa kuwaambia mashabiki wangu wakae mkao wa kula na wategemee mambo makubwa kutoka kwangu.
Risasi: Asante Maua.
Maua: Asante pia!
stori: HAPPYNESS MASUNGA