Mauaji ya Watu Weusi: Trump Hali Tete Marekani – Video

MCHAMBUZI wa Masuala ya Kidiplomasia, Dkt. Goodluck Ng’ingo, amesema kuwa kifo cha George Floyd ni mauaji ya kukusudia, yule askari amemkandamiza shingo pale chini zaidi ya dakika nane, watu walimsihi amuachie kwa sababu hata kupumua alishindwa lakini jamaa aligoma mpaka watu wa huduma ya kwanza walivyofika kumtoa.
Dkt. Ng’ingo amesema hayo wakati akifanya mahojiano ya moja kwa moja na kipindi cha Front Page cha Global Radio leo Ijumaa, Juni 5, 2020.
“Trump kama rais wa nchi hakulaani moja kwa moja tukio la mauaji ya George Floyd kwa sababu hajataka kuwaudhi Wazungu wenzake ambao wengi wao wanamuunga mkono. Tukio hili lipo kitabaka kwani aliyeua ni mweupe, aliyeuawa ni mweusi.
“Kufuatia mauaji ya Floyd, gavana a Minneapolis, aliagiza askari mmoja akamatwe wakati walikuwa wanne, hata mashtaka yenyewe ni ya kuua bila kukusudia, kwa sheria yao anaweza kufungwa miaka 25 jela au kulipa faini isiyozidi dola 40,000 ama kuachiwa huru.
“Mauaji ya watu weusi yamemtia doa Rais Trump, kumekuwa na mvurugano. Katiba ya Marekani inawaruhusu kuandamana, yeye anatumia nguvu, amewatawanya waandamanaji kwa kutumia risasi za mpira ili apige picha katika kanisa bila kubughudhiwa.
“Marekani imekuwa kinara kuwanyooshea vidole wengine kuwa wanakiuka haki za binadamu, lakini yeye ndiye kinara wa kukiuka haki za binadamu. Nchi za Afrika zikifanya jambo fulani utasikia ubalozi wa Marekani umetoa tamko la kulaani, lakini kwao hawafanyi hivyo,” amesema Ng’ingo,.

