Maumivu Makali ya Tumbo (Acute Abdomen)
Maumivu ya tumbo huwatokea watu wote wanaume na wanawake wakubwa na wadogo. Maumivu huanza taratibu au ghafla na kwa kasi. Tatizo hili huwa kali hadi wakati mwingine kusababisha mgonjwa kufanyiwa upasuaji.
Maumivu ya tumbo kwa ujumla wake yamegawanyika katika makundi manne; kwanza ni maumivu ya viungo vya ndani ya tumbo, maumivu yanayohusiana na mishipa ya fahamu, maumivu ya mbali katika mwili yanayosambaa na maumivu kuzunguka tumbo lote kwa ndani.
CHANZO CHA MAUMIVU
Maumivu huanza kwenye misuli ya tumbo na hapa hutokana na mzunguko wa damu kwenye misuli hiyo kutokuwa mzuri na kusababisha damu kuganda.
Maumivu pia huweza kuanzia katika mfumo wa mkojo na uzazi, mfano uvimbe au maambukizi ndani ya mfumo wa uzazi wa mwanamke, kuumia au maradhi yanayohusiana na korodani kwa mwanaume.
Maambukizi mbalimbali tumboni yanaweza kuleta maumivu makali mfano ugonjwa wa mkanda wa jeshi.
Matatizo katika kifua mfano magonjwa ya moyo, homa ya mapafu na maumivu ya chembe ya moyo yanaweza kusambaa tumboni.
Sumu mbalimbali mfano endapo mtu amekunywa madawa au kemikali kali, kuumwa na wadudu sehemu za tumbo mfano nge au tandu wanaweza kuleta maumivu makali.
MAGONJWA YANAYOSABABISHA MAUMIVU MAKALI YA TUMBO
Magonjwa haya yapo katika makundi mbalimbali kama tutakavyoona na huwa yanaanza taratibu au kwa ghafla na kuwa makali.
ACUTE MESENTERIC ISCHEMIA (AMI)
Ni ugonjwa unaosababishwa na kuziba kwa mishipa ya damu inayozunguka utumbo kutokana na damu kuganda au endapo damu haisambai vizuri kwenye utumbo, kwa hiyo sehemu inayotakiwa damu ipelekwe haiendi na kusababisha sehemu hiyo iharibiwe na hivyo mgonjwa kuhisi maumivu makali ya tumbo.
Tatizo hili hutokea tu lenyewe, halina chanzo maalum, huweza kumtokea mtu yeyote, uchunguzi wake ni mgumu kwa kutumia vipimo ndipo hapo inabidi mgonjwa apasuliwe kwa ajili ya uchunguzi na tiba ili tatizo linapoonekana wakati wa upasuaji litibiwe.
ACUTE PERFORATION (AP)
Hii ni hali ya kutoboka utumbo, sehemu yoyote ya utumbo inaweza kutoboka kutokana na sababu mbalimbali na kusababisha kilichopo kwenye utumbo kutokea katika sehemu isiyohusika.
Hapa mgonjwa hulalamika maumivu makali ya tumbo na tumbo linajaa. Tatizo hugundulika kwa kupiga picha ya X-Ray. Matibabu yake ni upasuaji, wagonjwa wengi wanaopatwa na hali hii hupoteza maisha kabla na hata baada ya tiba.
Utumbo unaweza kutoboka kuanzia juu unapomezea chakula moja kwa moja hadi katika mfuko wa haja kubwa, kwa hiyo sehemu yoyote inaweza kutoboka.Chanzo kikubwa cha kutoboka utumbo ni kuumia kutokana na ajali yoyote mfano kugonga sehemu yoyote ya tumbo, kuchomwa na kitu chenye ncha kali, kumeza vitu vyenye ncha kali kama vijiti hasa vya meno.
Kwa hiyo ni hatari kukaa na kijiti cha meno kinywani kwa muda mrefu, kumeza miiba ya samaki, sindano, mifupa na vyupa.
Itaendelea wiki ijayo.

