The House of Favourite Newspapers

MAUMIVU TUMBONI YALETWAYO NA KIDONDA CHA TUMBO !

MAUMIVU tumboni ambayo huja mara kwa mara yanaweza kuwa yanasababishwa na kidonda cha tumbo.

 

Maumivu ya kidonda cha tumbo kwa kawaida yanakuwa kama vile yanaunguza au kukwaruza hasa kama una njaa na maumivu husikika sehemu ya kati ya tumbo upande wa juu. Mara nyingi, kidonda husababisha maumivu kwa wiki chache na hutoweka kwa wiki au miezi kadhaa kabla ya kurudi. Maumivu yanaweza kupungua mtu anapokula au kunywa. Au kula kunaweza kuzidisha maumivu, kutegemea na mahali kidonda kilipo.

 

Dalili za hatari

Ili kujua kama una vidonda vya tumbo chunguza iwapo kuna damudamu au vitu vyeusi vinavyofanana na mabonge ya kahawa ya unga kwenye matapishi kama unatapika.

 

Kinyesi pia kinaweza kuwa na damu au vitu vyeusi vinavyofanana na lami au mafuta mazito ya gari. Hii ni hatari. Tafuta msaada haraka kwa daktari. Ukigundulika kuwa una vidonda tumboni, acha kabisa kutumia dawa kama ibrofeni (ibuprofen), aspirini na dawa nyingine za kupunguza maumivu.

Matumizi ya dawa hizi mara kwa mara huumiza tumbo na ni miongoni mwa sababu za kutokea vidonda vya tumbo. Panado (Paracetamol) ni bora kwa watu wenye matatizo ya tumbo kwa sababu haiathiri tumbo, lakini haipaswi kutumika sana au kila siku. Ukigundulika kuwa una vidonda tumboni, usivute sigara.

 

Watu wanaovuta sigara huwa na vidonda zaidi na vidonda vyao huchukua muda mrefu zaidi kupona. Ulaji wa milo midogo na kunywa maji mengi siku nzima kunaweza kusaidia kupunguza maumivu.

 

Unaweza ukakuta vyakula vingine vikikuzidishia maumivu. Jaribu kuepuka vyakula vyenye asidi kama vile ndimu na kahawa, pilipili, vyakula vyenye mafuta na pombe huzidisha maumivu kwa baadhi ya watu.

 

Msongo wa mawazo unaweza kuwa sababu mojawapo inayochangia watu kupata vidonda vya tumbo na pia kuzidisha maumivu. Kama baada ya wiki chache za kufanya mabadiliko bado kuna maumivu mengi, jaribu kutumia dawa ya kupunguza asidi tumboni yenye bei nafuu.

Maumivu yanaweza kupungua kwa kutumia kalisiamu kaboneti (calcium carbonate), mara 4 kila siku kwa wiki moja. Dawa kwa ajili ya kudhibiti uzalishaji wa asidi tumboni ziitwayo proton pump inhibitors (PPI), kama vile omeprazo, hufanya kazi vizuri zaidi. Hupunguza asidi tumboni kwa kiwango cha kuweza kupunguza maumivu na mara nyingi kusaidia kidonda kupona.

 

Hata hivyo, kama maumivu yatarudia, utahitaji kutumia dawa ya antibiotiki kuponya vidonda hivyo kwa ushauri wa mtaalamu wa afya. Matibabu Kwa ajili ya vidonda vya tumbo ambavyo hupona na kuibuka tena, utahitaji kutumia kwa pamoja dawa za antibiotiki, dawa ya kudhibiti uzalishaji wa asidi tumboni (proton pump inhibitors), na dawa za kudhibiti asidi kwa wiki mbili.

 

Hizi ni dawa nyingi, lakini ikitumika kwa usahihi vidonda vya tumbo havitarudia tena. Kama kutakuwa na maumivu tumboni baada ya matibabu haya, huenda kuna tatizo lingine na siyo vidonda vya tumbo. Tafuta msaada kwa daktari.

USHAURI MUHIMU

Baadhi ya watu hutumia sodiamu baikaboneti (sodium bicarbonate) kwa ajili ya kutibu maumivu tumboni. Hii hufanya kazi haraka, lakini husababisha tumbo kutengeneza asidi zaidi baadaye. Hivyo, usiitumie mara kwa mara. Usitumie sodiamu baikaboneti kama una matatizo ya moyo au miguu ambayo imevimba. Inaweza kuzidisha matatizo hayo.

Comments are closed.