Na Dk CHALE| GAZETI LA IJUMAA| AFYA
HALI hii hutokea mara tu mwanamke anapoanza hedhi yake, huwapata wanawake wengi walio katika umri wa kuzaa na maumivu huchukua wastani wa siku tatu. Maumivu huwa kwenye nyonga hasa upande wa chini wa tumbo. Hali hii huambatana na maumivu ya kiuno, kuharisha na kichefuchefu.
Kwa wasichana hali ya maumivu hutokea bila hata ya kuwepo sababu maalumu lakini kwa wanawake watu wazima endapo atakuwa na maumivu haya basi lazima kuna tatizo maalum.
Maumivu ya hedhi kwa wanawake wenye umri wa kati ya miaka ishirini na tano wakiwa bado wanapata hedhi husababishwa na uvimbe kwenye kizazi, kuvimba kizazi, hitilafu katika tabaka la ndani la kizazi. Hali hii husababisha mwanamke avurugikiwe na mzunguko wake, kupata damu nyingi sana ya hedhi na kwa muda mrefu na pia huwatokea wanawake ambao waliwahi kuvunja ungo kabla ya kufikisha miaka kumi na mbili au kwa wasichana wenye uzito mdogo sana kulinganisha na umri wao, aidha kutokana na kujinyima kula, kukosa lishe bora au kukonda kutokana na maradhi.
Kwa kawaida, kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa na tayari wameshaanza mahusiano, endapo watakuwa na tatizo hili, basi ni vizuri wafanyiwe vipimo kama Ultrasound mara wanapogundulika na maumivu haya kwa sababu dalili hizi za maumivu hufanana na matatizo mengine kama la mimba kutunga nje ya kizazi, magonjwa sugu au maambukizi sugu ya kizazi “PID” na maambukizi sugu ya kibofu cha mkojo. Maumivu wakati wa hedhi huwa hayatokei sana au yasitokee kabisa kwa msichana mwenye tabia ya kufanya mazoezi ya viungo au kushiriki michezo.
Inashauriwa watoto wa kike wawe na tabia ya kufanya mazoezi kama kukimbia, kucheza mpira, kuruka kamba na mchezo wowote wa kukutoa jasho. Maumivu haya hupungua au kuisha baada ya uchunguzi wa kina na kupata tiba ya dawa za kutuliza maumivu na dawa za homoni. Endapo kuna tatizo kama uvimbe, basi ni vema mgonjwa afanyiwe upasuaji kuondoa uvimbe.Kama hakuna tatizo ndani ya kizazi basi maumivu yataisha taratibu kadiri utakapoendelea kuzaa.
JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA
Maumivu wakati wa hedhi yamegawanyika katika sehemu kuu mbili. Moja ni Primary Dysmenorrhea
ambapo hapa mwanamke maumivu yanaanza pale anapovunja ungo na kuendelea nayo na huisha hapo baadaye anapokuwa mtu mzima. Pili ni Secondary Dysmenorrhea.
Hapa mwanamke anakuwa hana historia ya maumivu bali hutokea baadaye na chanzo kikubwa ni hitilafu katika tabaka la ndani, uvimbe ndani ya kizazi, kuvimba kizazi na uvimbe wa vifuko vya mayai.
DALILI ZA UGONJWA
Maumivu ya tumbo chini ya kitovu ndiyo dalili kuu ya tatizo hili wakati wa hedhi. Kwa ujumla dalili zote tumezielezea hapo katika utangulizi. Maumivu haya ya hedhi huwa yana tabia ya kusambaa kuzunguka kiuno, kulia na kushoto chini ya tumbo. Maumivu makali humfanya mwanamke ashindwe kuendelea na majukumu mengine na abaki amelala tu nyumbani au amelazwa hospitali.
UCHUNGUZI WA TIBA Hufanyika katika hospitali za mikoa kwenye kliniki za madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama. Mgonjwa baada ya uchunguzi wa kina atapatiwa matibabu.
Ni vizuri umuone daktari bingwa wa akina mama kwa uchunguzi. Epuka kutumia dawa bila ya ushauri. Zingatia kufanya mazoezi ya viungo na kushiriki michezo.
Kwa stori zote kali, Tu-follow
Facebook @Globalpublishers
Twitter @GlobalHabari
Instagram @GlobalPublishers
YouTube @GlobalTVTZ
Comments are closed.