The House of Favourite Newspapers

Maumivu ya kiuno kwa wanawake

0

Kuna wanawake wengi ambao husumbuliwa na maumivu ya kiuno mara kwa mara hasa wakati wa hedhi na kisha kufifia, huugua kwa muda mrefu zaidi ya miezi mitano.

Zipo sababu nyingi za kuzuka kwa maumivu haya kama vile kuwa na matatizo kwenye via vya uzazi, kibofu cha mkojo, utumbo mkubwa au misuli ya nyonga kuwa na tatizo.
Maumivu yanaweza kuwa yanaendana na mzunguko wa hedhi au la, mara nyingi hujitokeza chini ya kitovu na kiunoni.

Kuna sababu mbalimbali ambazo zinaweza kusababisha mwanamke kupata maumivu haya ya kiuno kwa muda mrefu, kama vile kuwa na maumbukizi ya ndani ya kiuno ya muda mrefu kitaalamu huitwa Chronic Pelvic infection.

Maambukizi haya hutokana ugonjwa wa TB na huweza kusababisha maumivu ya kiuno. Au kuwa na Endometriosis, hii ni hali ambayo seli za ukuta wa uzazi huota sehemu nyingine za uzazi na itokeapo hivyo basi mwanamke hujikuta akipata maumivu makali wakati wa hedhi au kufanya mapenzi.

Wengine hupata maambukizi ya muda mrefu ya shingo ya uzazi au mji wa uzazi nayo husababisha maumivu ya kiuno wakati wowote na hasa wakati wa kufanya ngono.
Wanawake wengine hupata maumivu hayo kutokana na mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi kitaalamu huitwa Ectopic Pregnancy.

Baadhi ya wanawake hutokwa na uvimbe mdogomdogo wa kizazi ambao husababisha maumivu pale unapokua kwa haraka na kukandamiza viungo vingine. Maumivu yake huwa ya wakati, huja na kuacha.

Wengine hupata maumivu wakati wa kukojoa kutokana na kuwa na maambukizi kwenye njia ya mkojo ya muda mrefu huku baadhi yao wakipata maumivu baada ya kupata maambukizi ya via vya uzazi kitaalamu huitwa Pelvic inflammatory Disease – PID au wale wenye maambukizi ya Kibofu cha Mkojo yaani Interstitial cystitis.

Wale wenye hali hii hupata maumivu hasa chini ya kibofu cha mkojo ambayo hupungua pale anapokojoa na hujikuta akikojoa mara kwa mara na kushindwa kubana mkojo.
Lakini pia ugonjwa wa Kidole Tumbo yaani Chronic Appendicitis huleta maumivu upande wa kulia chini ya kitovu ambayo huwa hayatulii na dawa za kutuliza maumivu na wapo wanaougua kiunoni chini ya kitovu kutokana na kuwa na Saratani ya Utumbo Mpana.

Wapo wanaougua kiuno kutokana na kusagika kwa mifupa kwenye maungio yaani Degenerative Joint Disease na hali hiyo inapotokea husababisha maumivu makali maeneo ya kiunoni hasa wakati wa kutembea.TIBA

Matibabu ya kuumwa na kiuno hutegemea na kinachosababisha kama tulivyoeleza hapo juu. Daktari akigundua tatizo baada ya uchunguzi atampa dawa husika mgonjwa, au dawa za majira kama tatizo linahusiana na mzunguko wa hedhi au atamfanyia upasuaji.

Leave A Reply