The House of Favourite Newspapers

MAUMIVU YA MGONGO BAADA YA KUJIFUNGUA KWA UPASUAJI

UZAZI kwa njia ya upasuaji kitaalam huitwa cesarean delivery au hospitalini huifupisha kwa kuita c-section na mtaani tumezoea kuita siza.  Upasuaji huu unafanyika kwa lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto. Upasuaji hufanyika kwa umakini na daktari bingwa wa afya ya uzazi au wa upasuaji.

Upasuaji hufanyika hospitalini kukiwa na timu ya wataalam waliobobea, mmojawapo ni mtoaji wa dawa za ganzi au usingizi au nusu kaputi ambao kitaalam utoaji wa dawa hizi za kuondoa maumivu ya upasuaji tunaita administration of anaesthetic. Hapa sindano huchomwa katika sehemu maalum ya uti wa mgongo wa mama mjamzito anayesubiri kupasuliwa dakika chache kabla daktari hajaanza kupasua na kumtoa mtoto.

Sindano inapochomwa ili kuingiza dawa ya ganzi hupenya kwenye ngozi, misuli, ligaments na mishipa ya fahamu. Sehemu zote hizo inamopita sindano huumia. Wakati wa kuchoma sindano hiyo, majimaji ya uti wa mgongo hutoka kidogo na kusababisha huyu mama baadaye apate maumivu ya kichwa na shingo. Mara nyingi maumivu huanza kujitokeza saa kumi na mbili baada ya mtoto kuzaliwa au yakaanza siku ya tatu hadi ya nne baada ya upasuaji huo na kumtoa mtoto.

MAUMIVU YA MGONGO HUDUMU KWA MUDA GANI?

Maumivu haya ya mgongo kutokana na sindano ya ganzi ya mgongo ya nusu kaputi hudumu kwa muda mrefu kidogo, hata kwa zaidi ya wiki moja na hata miezi, sababu kubwa ni ile sindano ikipenya inaumiza mishipa ya fahamu. Kuzunguka uti wa mgongo.

Hali ya maumivu huwa zaidi endapo utachomwachomwa sana kupata sehemu yenye maji ya mgongo ili kuingiza dawa, kukosa kupata majimaji ya mgongo kwa mara moja wakati wa kuingiza dawa husababishwa na mambo kadhaa, mojawapo ni endapo mgonjwa hatatulia wakati wa kuchomwa sindano, hili litamfanya daktari anayetoa nusu kaputi akuchome kila wakati.

NINI CHA KUFANYA?

Mwanamke anayepatwa na maumivu ya kichwa, shingo na mgongo baada ya siza, ni vema asaidiwe kwa karibu kushikiwa mtoto ili apate muda wa kupumzika na kupunguza maumivu. Hakikisha baada ya operesheni usinyanyue kichwa wala shingo hadi ganzi iishe kabisa angalau baada ya saa nane hadi kumi na mbili. Maumivu haya yanapotokea wakati mwingine huwa hayasikii dawa na kukufanya uteseke.

Zipo hatua nne zinazoweza kukusaidia kukabiliana na maumivu haya; Kwanza ni kuoga maji ya moto. Maji ya moto ni dawa nzuri sana kwa mwili, zimua maji ya moto katika joto unaloona linakutosha, maji haya yatatuliza haraka sana maumivu ya kichwa shingo na mgongo, unaweza kuongeza chumvi kidogo na kuiacha iyeyuke, chumvi kwenye maji itapenya kwenye ngozi na kufika sehemu zenye maumivu na kupata nafuu kubwa. Endapo sehemu ya kidonda bado hairuhusiwi kulowa, basi uoge maji hayo kwa kujifuta na kitambaa au kukandwa mwili mzima hasa kichwa, shingo na mgongo. Pili ni kufanya mazoezi mepesi, hii inatokana na mwili kupitia mabadiliko mengi wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.

Pata maelekezo ya mazoezi kutoka kwa daktari wako ili usije ukafumua nyuzi za mshono wa kidonda na kutokea matatizo mengine. Tatu ni kuhakikisha unalalia godoro zuri lisilokusumbua. Daktari atakushauri aina ya godoro la kutumia endapo umetoka kwenye siza halafu una maumivu ya mgongo.

Kama unaweza kupata godoro linalojazwa upepo, basi ni zuri zaidi kwani litafanya mgongo wako ukae vizuri zaidi unapolala. Nne unaweza kutumia barafu ‘ice pack’ sehemu zenye maumivu makali, lakini pia unaweza kutumia ‘heat pads’ kuweka kwenye maumivu makali ili kuamsha mzunguko wa damu na kuondoa maumivu.

USHAURI

Maumivu ya mgongo, baada ya upasuaji yamekuwa ni tatizo sugu hivyo usisite kurudi haraka kwa daktari wako, hakuna maumivu ya kawaida, maumivu yoyote ni mateso

Comments are closed.